Makala

KIKOLEZO: Ngoma ikichacha…

August 16th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

NI kawaida sana kusikia taarifa za wanasiasa au watu mashuhuri wanaotoroka mataifa yao kwa kuhofia maisha yao na kuishi uhamishoni nchi zingine.

Mara nyingi vitendo vyao huchochewa na kuogopa kuuawa na serikali ya siku kwa sababu ya kupinga sera zake au baada ya kutoa siri chafu za serikali husika.

Hapa nchini baadhi ya watu waliowahi kukimbia nchi na kuishi uhamishoni ni kama vile mwanasiasa Koigi Wa Wamwere aliyetorokea Norway baada ya kuchefuana kisiasa na Rais wa zamani Daniel Moi.

Mtumishi wa umma na mwanahabari wa zamani John Githongo alitorokea Uingereza wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki baada ya kufichua kashfa ya ufisadi ya Anglo-Leasing.

Aliyekuwa Kamshina wa IEBC Roselyn Akombe alijiuzulu wadhifa wake siku saba kabla ya marudio ya uchaguzi wa 2017 na kutorokea Marekani kwa kuhofia yaliyomkuta marehemu Chris Musando yatamkuta pia.

Lakini pia wapo wasanii hasa wanamuziki ambao wamejipata wakiyakimbia mataifa yao kutokana na tungo zao zilizoishia kukwaruza serikali vibaya wakizikosoa. Na kwa kuhofia usalama wa maisha yao, wakaenda uhamishoni.

GENERAL DEFAO (DRC)

Uhamisho: Kenya

BAADA ya kuishi uhamishoni mjini Nairobi, Kenya kwa miaka 18, mkongwe huyu wa Lingala kutoka Congo, alirejea kwao Jumapili iliyopita.

General Defao alitorokea Nairobi 2001, kipindi ambacho Rais wa zamani Joseph Kabila alipochukua mamlaka kutoka kwa babake Laurent Kabila baada ya kuuawa mwaka huo huo.

Kipindi hicho, Defao alikuwa ameachia nyimbo nyingi zilizofanya vizuri sana kutokana na ujumbe mzito wa kuukashifu utawala wa kiimla wa marehemu Laurent.

Hivyo baada yake kuuawa na mlinzi wake, na mwanawe kuchukua usukani, General Defao alihofia Rais Kabila angeyaandama maisha yake kwa kusudi la kumwangamiza hivyo akachukua uamuzi wa kukimbilia Kenya.

Hata hivyo baada ya Rais mpya Felix Tshisekedi kushika hatamu, kumekuwa na kampeni kubwa katika mitandao ya kijamii kutoka kwa mashabiki wake wakimtaka arudi nyumbani na ndicho alichokifanya.

Akiondoka, Defao alisema alichukua uamuzi huo kufuatia mwaliko wa Rais Tshisekedi ikiwa ni ishara kwamba alimhakikisha usalama wake.

HUGH MASEKELA (Afrika Kusini)

Uhamisho: Amerika

Nguli huyu wa muziki wa Jazz alifariki dunia Januari 2018 akiwa na umri wa miaka 79. Kifo chake kiliwashtua wengi duniani na wengi walimwomboleza kuanzia wanasiasa hadi mashabiki.

Masekela alianza sanaa yake akiwa kijana mdogo sana enzi za utawala wa ubaguzi wa rangi katika miaka ya hamsini katika karne iliyopita.

Hata hivyo akiwa na umri wa miaka 21, kijana barobaro, alilazimika kulitoroka taifa lake kufuatia maafa ya Sharpeville Massacre, Machi 1960.

Kipindi hicho Wafrika Afrika Kusini walikuwa wakipingana na utawala wa ubaguzi wa rangi. Kwenye maafa hayo ya Sharpeville, jumla ya Wafrika 69 waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano dhidi ya utawala huo dhalimu.

Tayari Masekela alikuwa ameshaanza muziki, tungo zake nyingi zikiwa ni za uwanaharakati wa kupinga utawala ule wa kiimla. Kwa kuhofia kuuawa, alitorokea zake Marekani na kwa miaka 30 aliishi uhamishoni. Alirejea nyumbani Afrika Kusini Septemba 1990 mambo yakiwa yamepoa na miaka minne baadaye Nelson Mandela akachaguliwa kama Rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo.

MIRIAM MAKEBA (Afrika Kusini)

Uhamisho: Amerika

Zenzile Miriam Makeba alikuwa mmoja wa wanamuziki maarufu kutoka Afrika Kusini staili yake ikiwa ni Afro-Pop na Jazz. Alikuwa pia mwigizaji. Makeba alifariki dunia Novemba 2008 nchini Italia, akiwa na umri wa miaka 76.

Makeba alianza sanaa yake enzi za utawala wa ubaguzi wa rangi na nyimbo zake nyingi zilikuwa za kupinga utawala huo. Mnamo 1959 aliigiza kwenye filamu fupi Come Back Africa iliyosimulia dhuluma walizokuwa wakipitia Waafrika mikononi mwa mzungu. Filamu hiyo ilipata umaarufu mkubwa sana duniani na kumfanya kujulikana na hata kumpelekea kupata shoo nje ya nchi. Na pia kwa kuhofia usalama wake, aliondoka Afrika Kusini na kuenda Marekani na kukita kambi mjini New York.

Kazi zake akiwa kule zikazidi kumfanya kuwa maarufu hata zaidi. Baada ya kifo cha mamake, 1960, alizuiwa na kurejea nchini humo kumzika. Serikali ilihofia ushawishi wake ungezidisha vurugu ambazo tayari walikuwa wanajitahidi kukabiliana nazo.

Nyimbo zake tayari zilikuwa zimepigwa marufuku Afrika Kusini zikitajwa kuwa za kichochezi.

Hugh Masekela ambaye alikuwa mume wake alimfuata huko New York ila ndoa yao ilivunjika 1966.

Makeba alirejea Afrika Kusini baada ya Nelson Mandela kuchukua madaraka na kumsihi arudi nyumbani.

Aliishi uhamishoni kwa miaka 31.

THE BEN (Rwanda)

Uhamisho: Marekani

Ben Mugisha al-maarufu The Ben ni staa mkubwa wa muziki wa kizazi kipya nchini kwao Rwanda licha ya kuwa anaishi uhamishoni kule Marekani. Staili yake ya RnB imemfanya kupendwa na kuhusudiwa na wengi sana.

Ukiongeza sifa hizo na utanashati wake pamoja na sura ya mvuto, inakuwa ni tatizo hata zaidi. Licha ya kupendwa na wengi hasa vijana nchini Rwanda , The Ben kashindwa kurudi nyumbani kwa kuhofia maisha yake, kutokana na kuikosoa serikali ya sasa.

The Ben alihamia New York 2010 na amekuwa akiishi huko kwa zaidi ya mwongo sasa.