Makala

KIKOLEZO: Ni zamu ya Bien na Chiki 2020?

January 10th, 2020 2 min read

Na THOMAS MATIKO

MWAKA huu mpya sijui tutarajie kuona nini kwenye mahusiano ya Showbiz hapa nchini.

Mwaka 2019 ambao tumeupa kisogo siku tisa zilizopita, tulishuhudia mahusiano ya kimapenzi ya maceleb yaliyoishia kwa wao kuhalalisha kwa ndoa.

Na pengine katika kujikumbusha tu kabla ya kusonga mbele, hawa ndio maceleb walioamua kulishana yamini 2019 na mwaka huu pengine itakuwa ni zamu ya Bien Aime na Chiki Kuruka, Vivian na Sam West na sijui kina nani tena. Hebu tujikumbushe.

NYASHINSKI NA ZIA BETT

Baada ya mahusiano ya miaka mingi na kichuna Zia Jepkemei au ukipenda Zippy, miezi miwili iliyopita msanii Nyashinski ambaye hupenda sana kuficha mahusiano yake alimwoa mbunifu mavazi huyo.

Ndoa ilikuwa ya kitamaduni na ni watu wachache sana wenye ukaribu na Nyash ndio walialikwa. Hao ni kama vile Bien Baraza wa Sauti Sol na Nameless.

BAMBOO NA ERICA MUKISA

Rapa Bamboo toka aliporejea nchini aliamua kuishi maisha ya ukimya. Aliachana na muziki na kuamua kuzamia kwenye uchungaji. Katika harakati hizo, alikutana na binti wa Kiganda Erica na kuanzisha mahusiano naye. Baada ya takriban miaka sita ya uchumba, alimbeba Erica mzima Februari mwaka jana wakifunga ndoa mjini Ruiru katika kanisa la babake.

DJ STYLEZ NA WANJIRU KIRITU

DJ Stylez ni mmoja wa MaDJ wakongwe hapa nchini. Ndiye mmiliki wa lebo ya CodeRed Deejays ambayo hutoa mafunzo kwa MaDJ chipukizi.

Baada ya miaka mingi kwenye biashara hizo, DJ Stylez alijitoa ili kukimbizana na biashara zingine. Hata hivyo bado yupo kwenye Showbiz. Pengine sasa ndio atapotea hata zaidi baada yake kufunga ndoa ya kimya kimya Februari mwaka jana.

Harusi yake iliwakusanya mastaa wa nguvu akiwemo CEO wa Sportpesa, Ronald Karauri pamoja na CEO wa KICC, Nana Gecaga.

JALANG’O NA AMINA CHAO

Mvunja mbavu Felix Odiwour al-maarufu Jalang’o naye aliamua kuasi ukapera kwa kumbeba mtoto wa Kiswahili Amina Chao Oktoba 2019. Ndoa ilikuwa ya kimyakimya tena ya kitamaduni. Ni watu wachache sana wenye ukaribu naye kama vile msanii wa zamani Gidi Gidi walioalikwa.

RUTH MATETE NA JOHN APEWAJOYE

Mshindi huyu wa Tusker Project Fame 5, naye aliridhia kuolewa na mpenzi wake kutoka Nigeria, John Apewajoye Novemba mwaka jana. Ndoa hiyo ilikuwa ya kanisani na Ruth ambaye amekuwa kimya sana, aliwaalika wanafamilia tu.

Ruth alipata umaarufu baada ya kushinda shindano hilo na kuondoka na hundi ya Sh5 milioni. Aligonga vichwa vya habari baadaye kwa madai kwamba alisota haraka baada ya kushindwa kutumia vyema fedha hizo. Taaluma yake ya muziki vile vile imekuwa ya wasiwasi.

ANYIKO OWOKO NA TOMAS MAULE

Kichuna Anyiko alianza kama mtangazaji wa Showbiz kabla ya kubadilisha upepo na kuanzisha kampuni ya PR ambayo imejikita zaidi kwenye Showbiz.

Novemba 2019 Anyiko naye aliamua kuwa mke wa mtu baada ya uhusiano wa muda mrefu na mpenzi wake Mzungu Tomas. Ndoa ilikuwa ya kitamaduni tena ya watu wachache na ilifungiwa Molo, Nakuru.