Habari Mseto

KIKOLEZO: Sasa wataji-nice bila presha

September 6th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

BAADA ya listi ya waigizaji wa kiume waliolipwa mkwanja mnene mwaka huu (Juni 2018 hadi Juni 2019) kutoka, sasa imefuata yao vichuna.

Scarlett Johansson

Kipato: Dola 56 Milioni

Unaambiwa siku hizi Scarlett kawa mjanja wa kupiga bei kwa kila atakayemwitia kazi.

Ujanja huu ndio umemwezesha kudumu kwenye listi hii kwa miaka kadhaa sasa. Kwa mara nyingine, kagandia kileleni.

Mwaka 2019 alikuwa mmoja wa wahusika wakuu wa filamu ya Avengers: End Game iliyotengeneza faida ya dola 2.8 bilioni.

Licha ya kuwepo na mastaa kibao wa kiume, Scarlett alihakikisha anajitetea vizuri kwenye suala la malipo.

Filamu hiyo pekee ilimwingizia dola 35 milioni. Tayari anasubiri mpunga mwingine wa maana mwaka ujao kutokana na uhusika wake kwenye filamu ya Black Widow itakayoingizwa sokoni Aprili mwakani.

Taarifa za Hollywood zinaarifu kwamba atalipwa kiasi kisichopungua dola 20 milioni. Kwenye listi ya pamoja ya waigizaji wa kike na kiume waliokusanya mkwanja mrefu zaidi mwaka huu, anakamata nafasi ya nane.

 

Sofia Vergara

Sofia Vergara. Picha/ Maktaba

Kipato: Dola 44.1 Milioni

Sehemu kubwa ya mkwanja wa Vergara haukutokana na filamu lakini vipindi mwendelezo vya televisheni hasa Modern Family ambavyo vimekuwa maarufu sana Amerika.

 

Reese Witherspoon

Kipato: Dola 35 milioni

Naye kama tu Vergara, sehemu kubwa ya kipato chake cha mwaka imetokana na malipo ya kipindi cha televisheni Big Little Lies. Kwa kila episodi ya kipindi hicho, alilipwa dola milioni moja.

 

Nicole Kidman

Kipato: Dola 34 Milioni

Reese hakuachana mbali na mwigizaji mwenzake kwenye kipindi hicho cha Big Little Lies. Wawili hawa ndio wahusika wakuu na kama tu mwenzake, Kidman, alilipwa dola milioni moja kwa kila episodi.

 

Jennifer Aniston

Kipato: Dola 28 Milioni

Kwa ujumla utajiri wa Aniston unakadiriwa kuwa wa dola 200 milioni. Aniston aliwahi kuongoza listi hii kwa muda mrefu kabla ya kushuka bei. Hata hivyo bado soko lake lipo na ndio sababu angali anao uwezo wa kuitisha mshahara mkubwa kwa ajili ya huduma zake.

Kipato chake cha mwaka huu kilitokana na vipindi vya televisheni na pengine kama angehusika kwenye filamu, basi hesabu zake zingefunika za Scarlett.

Mojawapo ya vipindi hivyo ni Untitled Morning Show Drama anachosemekana alilipwa dola 1.1 milioni kwa kila episodi. Hesabu hizi ziliongezeka zaidi kutokana naye pia kupewa kibarua cha kuwa produsa wa kipindi hicho.

 

Kaley Cuoco

Kipato: Dola 25 Milioni

Ana zaidi ya miaka 20 kwenye uigizaji. Cuoco ni mmoja wa waigizaji waliotawala komedi maarufu ya Bing Bang Theory. Series hiyo ilitamatika Mei mwaka huu baada ya kupeperushwa kwa jumla ya ‘Seasons’ 11.

Cuoco ni mmoja wa wahusika waliolipwa vizuri na komedi hiyo. Alilipwa dola milioni kwa kila episodi ila wakati wa kuelekea kuisha, tonge lilipunguzwa hadi laki 900,000 ili kuwasapoti waigizaji walioongezwa. Pato la Cuoco nalo lilitokana na malipo ya vipindi vya televisheni.

 

Elizabeth Moss

Kipato: Dola 24 Milioni

Moss alipata umaarufu kupitia vipindi vya televisheni tangu miaka ya 70 ila kwa sasa kajitosa kwenye filamu ambapo anapiga posho la maana.

Mwaka 2019 alihusika kwenye filamu ya US ambayo mzalendo Lupita Nyong’o aliigiza kama mhusika mkuu. Filamu hiyo iliishia kutengeneza faida ya dola 254 milioni kutoka bajeti ndogo ya dola 20 milioni.

Faida hiyo iliwawezesha waigizaji wote waliohusika kulipwa mkwanja mrefu akiwemo Moss. Hesabu zake zingine zilitokana na malipo ya vipindi vya televisheni anavyohusika navyo.

 

Margot Robbie

Kipato: Dola 23.5 Milioni

Ndiye mwigizaji mchanga zaidi kwenye listi hii akiwa na miaka 28. Kwa ujumla utajiri wake kabla ya kutoka kwa listi hii, ulikadiriwa kufikia dola 12 milioni.

Sasa ni dhahiri shahiri kuwa thamani itapanda licha ya kipato alichoingiza mwaka huu kuwa hesabu ya ujumla kabla ya makato ya kodi.

Mwaka 2018 aliigiza kama malkia kwenye filamu ya Mary, Queen of Scots. Kutumika kama mhusika mkuu kulimwezesha kuingiza mihela zaidi.

 

Charlize Theron

Kipato: Dola 23 Milioni

Theron ni mwigizaji wa miaka mingi sana akiwa amehusishwa kwenye filamu kubwa kadhaa kama Mad Max Fury Road 2015, The Italian Job, The Fate of The Furious, kati ya nyinginezo.

Kipato chake cha mwaka jana kilichangiwa na mshahara mzuri aliolipwa kutokana na uhusika wake kwenye filamu ya Fast & Furious 9. Pia mwaka huu alihusika kwenye filamu ya Long Shot iliyotoka Mei akiwa mhusika mkuu.

 

Ellen Pompeo

Kipato: Dola 22 Milioni

Ndiye anayekamilisha listi hii. Pompeo ni miongoni mwa waigizaji wa bei ghali. Hii ni kwa sababu kando na kuigiza pia ni mwelekezi na produsa. Sifa hizo mbili ndizo zinazopandisha thamani yake.

Katika miaka ya hivi karibuni, amekuwa akijihusisha zaidi na uprodusa.