Makala

KIKOLEZO: Ujuha wa mapenzi kwenye showbiz

September 27th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

KUNA msemo niliowahi kuusikia zamani kidogo; sikumbuki wapi ila yale maneno yaliniganda kichwani kwamba ‘ukitaka kumfichia jambo Mwafrika, basi liweke kwenye vitabu na ukitaka kumfichia jambo Mzungu, basi liweke kwenye ndoa’.

Kauli hii kimsingi ina maana kwamba asilimia kubwa ya Waafrika sio wasomi wazuri au hawapendi kusoma hivyo kama kuna jambo ambalo utakusudia kumfichia itakuwa vyema ukiliweka kwenye madaftari na itamchukua muda kuling’amua au kulielewa.

Kwa upande ule mwingine kwa mzungu, ukitaka kumbania jambo, basi lisuke kwenye ndoa.

Kwa mujibu wa msemo huo ni kwamba wazungu hawana ufahamu mzuri wa maisha ya ndoa, hawana subra kwenye ndoa au pengine masuala ya ndoa huwa magumu sana kwao na ndio sababu asilimia kubwa ya ndoa zao huwa hazidumu. Hoja hii pia ipo kwa mastaa wa kimataifa na ili kupata picha kamili, makala haya yanaangazia ndoa fupi zaidi za mastaa kadhaa ulimwenguni na hasa majuu.

BRITNEY SPEARS NA JASON ALEXANDER

MUDA: Saa 55

Unaweza kusema ndoa hii ilidumu kwa siku mbili na nusu hivi. Ilitokea siku moja 2004 baada ya nyota huyo wa muziki wa Pop kwenda kujivinjari na rafiki yake wa tangu utotoni Alexander, mjini Las Vegas.

Mapenzi yaliwanogea na kuwapelekea kufikia uamuzi wa kuoana. Hata hivyo baada ya muda wa saa 55 wakagutuka kwamba walifanya kukurupuka na kuivunja ndoa hiyo.

NICOLAS CAGE NA ERIKA KOIKE

Muda: Siku 4

Ndoa ya nne ya mwigizaji huyu asiyeishiwa na utata ilidumu kwa siku nne pekee. Wawili hao walikuwa wamedumu kwenye mapenzi kwa miezi mitatu kabla ya kuamua kuoana mapema mwaka 2019.

Hata hivyo siku nne baadaye Nicolas aliitisha talaka akisema kuamkia siku ya harusi alikuwa mlevi chakari hivyo maamuzi yake hayakuwa sahihi.

EDDIE MURPHY NA TRACEY EDMONDS

MUDA: Siku 14

Baba huyu wa watoto tisa alimwoa Tracey Januari Mosi 2008, kipindi wakiwa wamekwenda kujivinjari katika visiwa vya Bora Bora vinavyopatikana kule Tahiti. Matatizo ghafla yakaanza wakiwa kwenye likizo hiyo na ndoa yao ikavunjikia huko huko na ndio sababu haitambuliki Amerika. Hadi wanaachana, ndoa hiyo ilikuwa imemaliza wiki mbili pekee.

PAMELA ANDERSON NA RICK SALOMON

MUDA: Siku 60

Mwigizaji na mwanamitindo mkongwe Pamela alifunga ndoa ya kukurupuka na mume wake wa zamani Salomon, Oktoba 2007. Huyu Salomon ni mpenzi wa zamani Paris Hilton na alishiriki kwenye mkanda wa ngono na nyota huyo mwanamitindo uliovuja miaka hiyo. Salomon na Pamela walilishana yamini kule Las Vegas kwenye ndoa ya faraghani. Miezi miwili baadaye Pamela aliitisha talaka kutokana na sababu zisizoepukika.

KIM KARDADHIAN NA KRIS HUMPHRIES

MUDA: Siku 72

Ndoa hii haikuwa fupi tu, bali inatajwa kuwa ndoa fupi na ghali zaidi. Soshiolaiti Kim alifunga ndoa na mwanavikapu huyo kwenye harusi moja ya kufana iliyoripotiwa kugharimu dola 10 milioni 2011.

Baada ya siku 72, Kim alitoa taarifa akisema wameamua kuivunja baada ya kugundua kwamba haukuwa uamuzi mzuri. Wengi walidai kuwa ilikuwa ni kiki ya kumpa umaarufu Kim na hakika hapo ndipo umaarufu wake ulianzia huku Kris akififia. Kwa sasa Kim yupo kwenye ndoa na rapa Kanye West wakiwa wamedumu kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

NICOLAS VAGE NA LISA MARIE PRESLEY

Muda: Miezi 3

Mwigizaji staa Nicolas mpaka sasa kaoa mara nne. Ndoa zimekuwa zikimla chenga. Ndoa yake ya pili ilikuwa ni kwa binti wa pekee wa marehemu mwanamuziki na mwigizaji Elvis Presley iliyofanyika 2002. Hata hivyo miezi mitatu baadaye walitemana kimyakimya. Talaka yao iliidhinishwa 2004. Wakifunguka kuhusu chanzo cha kuvunjika kwa ndoa hiyo, Nicholas alidinda kukizungumzia huku Marie akisema hawakupaswa kuoana toka mwanzo na kwamba walikosea sana kwa kuchukua uamuzi huo.

BRADLEY COOPER NA JENNIFER ESPOSITO

MUDA: Miezi sita

Mwigizaji Bradley Cooper alikutana na mke wake wa zamani Jenny kwenye uandalizi wa sinema ya Blue Bloods. Wakapendana na kuoana Disemba ya 2006 ila Siku 122 baadaye, Bradley akaitisha talaka huku akisema uamuzi wa kuvunja ndoa hiyo ulikuwa wa pande zote mbili baada ya kugundua kuwa walifanya kuparamia tu.

MILEY CYRUS NA LIAM HEMSWORTH

MUDA: Miezi 8

Baada ya kuwa wapenzi kwa mwongo mmoja, nyota mwanamuziki Miley na mpenziwe mwigizaji Liam waliamua kuhalalisha uhusiano wao kwa kuoana. Kwanza walichumbiana rasmi Juni 2012 baada ya kuwa kwenye mahusiano ya kutemana wakirudiana. Septemba 2013 wakavunja uchumba wao na kuacha kuishi pamoja kwenye mjengo waliokuwa wakimiliki mjini Los Angeles. Januari 2016 walirudiana tena na kuchumbiana kwa mara nyingine Oktoba 2016. Desemba 2018 waliamua kuoana kwenye ndoa ya kimyakimya kule Tennesse, Amerika. Agosti 10, 2019, Miley alitangaza kuwa wameachana. Siku 11 baadaye Liam akaitisha talaka huku akisema ilisababishwa na matatizo magumu baina yao yasiyoweza kutatulika.

JENNIFER LOPEZ NA CHRIS JUDD

MUDA: Miezi 10

Majuzi J.Lo alimwaga mamilioni ya pesa kusherehekea kutimiza miaka 50 katika maisha yake. Maisha ya J.Lo yamekuwa ya vimbwanga sana hasa kwenye upande wa mapenzi akipendelea sana kutoka na vibenten enzi za ujana wake. Mmoja wa vibenten ni Judd. Ilikuwa ni katika miaka ya 2000 alipomwajiri kuwa dansa wake kwenye video ya Love Don’t Cost a Thing. Ghafla mapenzi yakawalemea na wakaona ni freshi wavishane pete. Hilo likafanyika Septemba 2001 lakini kufikia Juni 2002 kila mmoja akaamua kushika hamsini zake.