Makala

KIKOLEZO: VIP haileti shangwe!

September 13th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

JUZI niliketi kwenye kikao na mabosi wangu wa kitengo hiki cha burudani na masuala ya Showbiz.

Vikao hivi vya kuitathmini gemu na kupanga nini cha kuangazia, huwa ni kitu cha kawaida katika maisha yetu ya kila siku tukiwa miongoni mwa wadau wa Showbiz.

Mjadala uliponoga, iliibuka ishu moja nzito ambayo wengi au baadhi mtakuwa mumewahi kushuhudia.

Hivi katika tamasha zote za kiburudani uliyowahi kuhudhuria hapa nchini na ukalipia tiketi ya VVIP au VIP, uliridhishwa?

Je, ulipata huduma inayokwendana na staha na hadhi ya VVIP au VIP au ulichezwa?Jibu tayari najua unalo. Itakuwa ni, hapana.

Hakika hapa nchini ununuzi wa tiketi za VVIP au VIP huwa ni wizi wa mchana kweupe tena wa kimabavu sema mwathiriwa haachwi na majeraha. Katika tamasha kibao zilizoandaliwa hapa nchini ambazo huwa na tiketi za VVIP au VIP (kwa kawaida huwa ghali mno kuanzia Sh7,000), mwisho wa siku huwa sio matumizi mazuri ya fedha.

Kati ya nilizofanikiwa kuhudhuria hapa nchini na nikalipia VVIP au VIP, ninaweza kukukatia kauli kwamba sikupata huduma ya kiwango cha tiketi hiyo.

Hivi lakini huduma ya VVIP au VIP kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa ambavyo waandalizi wa Showbiz nchini hukwepa kwa makusudi ili kutuibia, huwa nini haswa?

ENEO LA VIP AU ‘VIP LOUNGE’

Hili huwa ni eneo spesheli lililoandaliwa kwa kupambwa na kurembwa kwa ajili ya kuwapokea wateja wa VIP.

Makochi ya kisasa huwa sehemu hii, tofauti kabisa na eneo la kawaida (Regular) ambalo wateja hubanana tena huwa wamesimama mara nyingi

Kama ni tamasha ya muziki au uigizaji, au Stand Up Comedy, eneo hili huwa karibu sana na jukwaa. Pia ulinzi wa eneo hili huwa wa hali ya juu kuliko sehemu nyingine ile.

Nitakuwa mwongo kusema kuwa tamasha hapa nchini huwa hazitimizi haya. Suala la utengenezaji wa ‘VIP Lounge’ hapa Kenya ndicho kitu ambacho mapromota wengi hutilia mkazo na baada ya hapo wanasahau mengine.

Wakishapanga makochi ya kisasa na kuyaremba, basi wanajisahaulisha kabisa mahitaji mengine ya huduma ya ki-VIP.

Mahitaji haya mengine ni kama vile kuwa na mhudumu spesheli aliyetengewa kazi ya kuwahudumia wana-VIP.

Hapa Kenya hata ukiwa VIP bado utakwenda kujitafutia msosi au kinywaji. Ndivyo ilivyokuwa kwenye Jah Cure Concert uwanjani Uhuru Gardens Julai mwaka huu kwa mfano tu.

MAZINGIRA YENYE STAHA NA HADHI

Ndio sababu msingi ya kuwepo na eneo la VIP. Tamasha inapoandaliwa, bei za tiketi hutengenezwa kugharimia mahitaji ya kila mteja.

Wote wale kusudi lao huwa ni kufika na kupata burudani kutoka kwa mtumbuizaji yule yule.

Sasa tofauti itakuwa pale kwenye VIP. Lazima kuwepo na la ziada kwa mteja wa VIP, yaani ile ‘experience’. Anapaswa kuhisi anapata zaidi ya aliyelipia Regular. Haya ndiyo yale mazingira ya staha na hadhi.

Kumtengea VIP mhudumu wake, ni sifa moja. Yule staa anayetumbuiza pia anapaswa aagizwe kuwa asisahau kujichanganya na wana -VIP wakati wa tamasha na hata apige nao picha ama selfie.

Kwa mfano kama ilivyokuwa kwenye tamasha ya Chris Brown mjini Mombasa 2016. Nyota huyo alitangamana na mashabiki wa VIP na baadhi waliobahatika kupiga picha naye, wameishi kuisifia tamasha hiyo mpaka leo. Kwenye Wasafi Festival, kitengo cha VVIP, Diamond na wapambe wake walijitahidi na kutangamana na kupiga picha na baadhi ya mashabiki japo kwa vijisekunde tu.

USALAMA THABITI

Kwa waliohudhuria tamashaya Konshens Jumamosi iliyopita, wana-VIP na wenzao wa Regular walitoka kapa au sare licha yao kulipia tiketi zao Sh7,000 na wenzao Sh2,000.

Waandalizi wa Hype Fest walishindwa kabisa kutengeneza ua thabiti na salama kwa ajili ya wateja wa VIP.

Walishindwa kupanga ulinzi wa mabaunsa wa kutosha au maafisa usalama ili kuwalinda wana-VIP. Kilichofuatia, kijiji cha mashabiki kiliwazidi nguvu walinzi wale na kuvunja ua kwenye eneo la VIP na kuingia ndani. Utahisi vipi kujichanganya na mtu aliyelipa Sh2,000 na wewe Sh7,000?

Kwa levo za kimataifa, suala la usalama kwenye eneo la VIP huwa kitu kikubwa sana, Kenya tunapenda kupuuza.

Kando na kuhakikisha kuna ua au vizuizi thabiti na mabaunsa au maafisa wa usalama wa wanaozingira eneo hilo, pia kunapaswa kuwe na maeneo tofauti ya kiingilio. Yaani anakoingilia VIP na anakotokea inapaswa kuwa sehemu tofauti kabisa na Regular. Kwa kifupi watu hawa hawapaswi kukutana kabisa kutokana namna vizuizi vilivyopangwa. Hype Fest walilazimika kuomba msamaha sababu wana-VIP wengi kwenye tamasha ya Konshens walipoteza simu zao za bei.

ZAWADI ZA BURE

Hili waandalizi wengi hapa nchini katu hawawezi wakakubaliana nalo, lakini ni mojawapo ya vigezo vya kumtengenezea mazingira ya kujihisi spesheli mteja wa VIP.

Nchini Kenya utanunua tiketi ya VIP ya zaidi ya Sh15,000 kama kwenye Wasafi Festival na bado vinywaji utajinunulia mle ndani tena kwa bei ya juu.

Kimataifa kwenye VIP, mteja atapata kifurushi ambacho kitampa kinywaji cha bure; inaweza ikawa glasi moja au mbili za mvinyo, au mzinga au mizinga miwili kisha mingine akajinunulia mwenyewe.

Au wakati mwingine mteja wa VIP anapewa bonasi nyingine ya kinywaji kwa kila anachonunua. VIP za Kenya hili sahau. Huduma zao huwa ovyo na kawaida sana.

Ndio maana mara nyingi VIP na Regular za hapa nchini ni sawa na mtu aliyevalia tisheti ya ‘camera’ na wewe ukawa na tisheti kama hiyo ila umenunua dukani tena kwa bei mbaya!