NA SINDA MATIKO
MALUMBANO kati ya shirika la Music Copyright Society Of Kenya (MCSK) na Bodi ya Hakimiliki nchini – Kenya Copyright Board (KECOB0) – yamechacha.
Kwa miaka na mikaka sasa MCSK ambayo imetwikwa jukumu la ukusanyaji wa mirabaha kwa niaba ya wanamuziki wanachama wake, imekuwa ikijikuta kwenye vuta nikuvute na KECOBO chombo ambacho hutoa leseni kwa makampuni ya ukusanyaji mirabaha nchini.
MCSK hukusanya zaidi ya Sh100 milioni kama mirabaha kila mwaka kwa niaba ya wanamuziki 16,000 wanachama wake.
Kwenye vita vya sasa, mambo yameonekana kubadilika na vita vimeonekana kuwahusu watu wawili; Afisa Mkuu Mtendaji wa MCSK Dkt Ezekiel Mutua dhidi ya Mkurugenzi Mkuu wa KECOBO Edward Sigei.
Malumbano ya vyombo hivi viwili yalianza mwaka jana KECOBO ilipoamrisha kufanyike ukaguzi wa vitabu vya kifedha vya MCSK.
Kulizuka vuta nikuvute zilizoishia mahakamani.
Upepo sasa umeonekana kubaadilika na kuwa kimbunga kikali kati ya vyombo hivi.
MCSK YAMLIPUA SIGEI
Ngoma ilianza Oktoba 25, 2022 MCSK ilipoandikia barua KECOBO ikiomba kupewa leseni ya 2023.
Miezi minne baadaye, KECOBO haikuwa imerudisha majibu yoyote kwa MCSK kuhusu maombi hayo.
Januari 11, 2023, MCSK kupitia Afisa Mkuu Mtendaji wake Dkt Mutua iliandika barua kwenda kwa afisi ya Ombudsman ikiomba kuondolewa kwa Sigei kama Mkurugenzi wa KECOBO.
Ombudsman ni afisi kwenye kitengo cha Mahakama chenye mamlaka ya kuvichunguza vyombo vya serikali na kuvipiga msasa.
Kwenye barua hiyo iliyoandikiwa Katibu mkuu wa Ombudsman, Mercy Kalondu Wambua, ilimshutumu Sigei kwa kuwa na tabia za udikteta kwenye utendaji wake.
“MCSK inawasilisha ombi kwa niaba ya wanachama wake zaidi ya 15,000 ikitaka Bw Sigei, Mkurugenzi Mkuu wa KECOBO atimuliwe. MCSK tumekuwa tukijitahidi kutekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa malekezo ya KECOBO ila muhusika Sigei ameonyesha tabia za kitapeli, unyanyasaji na ukandamizaji. Amekuwa na tabia za kutupokonya leseni kwa visingizio vya makosa ya kubuni kinyume na sheria. Aidha, amekuwa na tabia za kuitisha hongo wanachama wa bodi ya MCSK,” sehemu ya barua hiyo ilieleza.
KECOBO YAIKAUSHIA MCSK LESENI
Siku moja baadaye Janauri 12, 2023 ikiwa ni miezi minne toka MCSK itume ombi la leseni ya kufanya kazi mwaka huu, KECOBO ikajibu.
Kwenye barua iliyotiwa saini na Sigei, KECOBO ilitoa maelezo kadhaa ikitaja kuwa sababu za kushindwa kuipa leseni MCSK.
KECOBO ilieleza kuwa MCSK haikuwasilisha ukakuguzi wa vitabu vyake vya kifedha kufikia Juni 2022, majina kamili ya wanachama wake kufikia 2022 pamoja na listi ya wanachama wote waliolipwa mirabaha 2022.Kwa sababu hizo, KECOBO ikadinda kutoa leseni na kuiamrisha MCSK kukoma kuendelea kukusanya mirabaha mara moja.
MCSK YAJIBU MAPIGO
Siku iyo hiyo, MCSK ilikaijibu KECOBO na kuifahamisha kuwa itaendelea kukusanya mirabaha hata bila ya leseni hiyo.
Aidha kwenye barua hiyo iliyotiwa saini na Dkt Mutua, ilimchana Sigei ikimshtumu.
“Fahamu kuwa MCSK itaendelea kukusanya mirabaha kwa misingi ya amri ya mahakama ya rufaa kesi namba E395 2022 iliyotoa ruhusa kwetu kuendelea kukusanya mirahaba hadi pale itakapofanya kikao Februari 2023 kutoa maamuzi kamili.”
Mbali na hilo, barua hiyo ndefu ilimchana Sigei kwa madai ya kujaribu kuisambaratisha MCSK.
“Tunajua mpango wako ni kuja na mchakato mpya wa ukusanyaji mirabaha utakaokufaidi wewe. Unachojaribu kufanya ni kama lile tukio la 2017 ulipoipokonya MCSK leseni na kuipa MPAKE iliyokuwa ikisimamiwa na kibaraka wako. Kwa muda wote MPAKE ilikuwepo ilikusanya zaidi ya Sh100 milioni na wala haikugawa senti hata moja kwa wanamuziki. Taarifa tulizonazo ni kuwa wewe bwana Sigei ulifaidi sehemu kubwa ya fedha hizo ulizotumia kujenga boma ya kifahari na hoteli.”
SIGEI AJIBU MADAI
Tulipowasiliana na Sigei, Mkurugenzi huyo alimtupia kijembe Dkt Mutua akimtaja kuwa mwoga na mwenye machungu baada ya kunyimwa leseni.
“Kama kweli anasema ana ushahidi ni kwa nini hajautoa au kuukabidhi kwa vyombo husika ili sheria ifuate mkondo? Hao anaosema nilioamba hongo, ni vyema akiwataja majina, tarehe nilizowaomba hongo, maeneo tuliyokuwepo na akaunti zilikoishia fedha hizo. Hiki ni kitendo cha uwoga cha kunichafulia jina ninachowazia kukichukulia hatua. Kuna njia nyingi za kulalamika kunyimwa leseni ila sio hivi,” Sigei alijibu.
Kwa sasa ni kusubiri kuona ni wapi jipu litapasukia.