KIKOLEZO: Waliambiwa ‘mtaachana tu’!

KIKOLEZO: Waliambiwa ‘mtaachana tu’!

Na THOMAS MATIKO

NI kama laana au mkosi vile.

Tumeshuhudia ndoa nyingi za mastaa zikivunjika baada ya muda mfupi hasa pale wahusika hawa wanapoamua kuringisha ndoa zao mitandaoni.

Sasa imekuwa kama mtindo kwamba ndoa nyingi za maceleb zinazoringishwa mitandaoni haziishi kudumu na mtindo huu haonekani kupoa.

ANERLISA NA BEN POL

Baada ya kusumbua sana mitandao na penzi lao lililoota maua 2018, kapo hii ya binti Mkenya tajiri na mwanamuziki staa kutoka Bongo iliamua kufunga ndoa.

Harusi ya kimya kimya ilifanyika Mei 2020 kule Dar es Salaam katika kanisa la Katoliki la St. Gaspar na kuhudhuriwa na wageni wachache waalikwa wengi wakiwa ni wanafamalia na marafiki wa karibu sana.

Hata hivyo mwaka ukiwa hata bado haujamalizika, taarifa za utendeti kutoka Bongo zinaarifu kuwa Ben Pol tayari kawasilisha faili mahakamani kuomba talaka dhidi ya mke wake Anerlisa.

Bado sababu za talaka hii hazijabainika ila matukio ya hivi karibuni yamekuwa yakiashiria kitumbua kuingia mchanga.

Taarifa hizi zilizofichuliwa na bloga maarufu na mtangazaji radio Millard Ayo, zinajiri siku chache tu baada ya Anerlisa kulidondosha jina la Ben Pol (Bernard) Mnyang’anga kutoka kwa majina yake. Aidha mishemishe za kuposti picha na video zao za malavidavi zimepungua tofauti na pale penzi hilo lilipoanza.

WILLIS RABURU NA MARY PRUDE

Mapenzi yao yalianza vizuri tu na kuwa gumzo sana kutokana na jinsi wapenzi hawa wa zamani walivyokuwa wakijianika hasa mitandaoni.

Mtangazaji wa Citizen TV hakuchoka kumsifia mke wake mara kwa mara. Yalikuwa mapenzi matamu kiasi cha wao kuanzisha chaneli yao ya pamoja ya Youtube. Chaneli hiyo ilihusu masuala ya lishe bora na afya.

Posti zao za mapozi ya kilavidavi ungekutana nazo kila leo. Yalikuwa ni mapenzi yaliyokuwa yameshamiri kwa miaka miwili lakini majanga yalianza walipoamua kuingia kwenye ndoa.

Nyufa kwenye ukute wa ndoa ya hawa zilianza kujitokeza Januari 2020 Raburu alipoomba likizo ya dharura ili kuwa karibu na mke wake baada ya kupoteza ujauzito.

Tetesi wakati huo zilidai kwamba chanzo cha Mary kupoteza ujauzito wake na hata kuugua sonona, ilisababishwa na mume wake kumchepukia kipindi akiwa na mimba hiyo.

Hakuna kati yao aliyezungumzia madai hayo. Miezi mitano baadaye ikaripotiwa kwamba wanandoa hao wametemana na kila mmoja kashika hamsini zake.

Zile picha za pamoja walizokuwa na mazoea ya kuposti zikasita. Mary naye akabadilisha majina yake kwenye Instagram kwa kudondosha jina la mume wake. Mpaka leo wote wamegoma kuzungumzia tatizo lililoizonga ndoa yao. Hata hivyo mapaparazi wanadai ni michepuko kwa upande wa Raburu ndio uliosambaratisha ndoa hiyo.

BETTY KYALO NA DENNIS OKARI

Mahusiano ya watangazaji hawa wa runinga yaligonga vichwa vya habari sana. Walianza mahusiano yao walipokuwa wakifanya kazi katika stesheni ya KTN ambapo Betty alifichua kuwa ndiye aliyemtongoza Okari.

Mapenzi yao yalikuwa ya kweli na hawakuchoka kuposti mitandaoni jambo ambalo liliwaongezea umaarufu.

Walipoamua kufunga ndoa Oktoba 2015, walipokea udhamini mkubwa kutoka kwa wadhamini mbalimbali waliotaka kuhusishwa na kapo kubwa na maarufu nchini wakati huo. Ndoa yao ya kifahari ilifanyika katika uwanja wa Marula Manor katika mtaa wa kifahari wa Karen. Ilikuwa ni harusi iliyogharimu mamilioni ya pesa.

Hata hivyo baada ya miezi sita pekee, ndoa hiyo iliingia mdudu na kuvunjika huku kukiwa na tetesi kuwa familia zao zilihusika kwenye kusambaratisha ndoa hiyo.

Tangu wakati huo Okari aliamua kuwa msiri sana na maisha yake mitandaoni kwani hata ndoa yake nyingine ya 2019 aliifanya kimya kimya. Kwa mwenzake Betty, amekuwa makini kuficha sana mahusiano yake mitandaoni.

JB MASANDUKU NA TINA KAGGIA

Ni mahusiano mengine yaliyoanikwa sana mitandaoni na hata baada yao kufunga ndoa bado hawakuchoka kuposti maisha yao.

Hata hivyo matatizo yalianza pale mchekeshaji Masanduku aligeua na kuwa mlevi wa kupindukia na mara nyingi hakuwa akifika nyumbani.

Baada ya kuvumilia kwa miezi kadhaa mtangazaji wa redioni Tina aliamua kumtaliki na kuomba mahakama imzuie Masanduku kuzungumzia mahusiano yao.

SHARON MUNDIA NA LONINA LETEIPAN

Ilipokuwa kapo, kila mmoja aliitamani sana. Hakuna anayeweza kusahau jinsdi Leteipan alivyokodisha chopa na kwenda kumposa vloga Sharon kwenye eneo fulani la mlima hivi. Penzi lao lilikuwa habari ya mjini na hata ndoa yao ilifuatiliwa sana na wengi. Mahusiano yao yalikuwa yamedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja lakini walipoamua kufunga ndoa, haikudumu kwa zaidi ya miezi sita. Inadaiwa kuwa Sharon ndiye aliyeivuruga ndoa hiyo baada ya kuchepuka. Toka wakati huo, Sharon hajawahi kuwa muwazi tena na mahusiano yake mitandaoni.

You can share this post!

Dawa za kutibu akili taahira zinapogeuzwa ulevi wa mauti

KASHESHE: Sioni tena nikiwahi kuwa mke wa mtu!