Makala

KIKOLEZO: Walichepuka ila haikuwa ishu!

November 22nd, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

KULE Bongo wana msemo wao kuhusiana na michepuko ‘Michepuko sio dili’.

Hakika kuchepuka mwisho wake huwa ni madhara makubwa katika mahusiano. Lakini ukweli mchungu ni kuwa, michepuko imekuwa jambo la kawaida na hasa kwa mastaa wasanii.

Wapo wengi ambao wameumizana wakaishia kuachana lakini wapo pia waliokiri kuchepuka na wakasamehewa na kurejesha mapenzi yao kwenye mstari. Hii hapa ni listi ya mastaa wachepukaji waliopata afueni ya kusamehewa baada ya kukiri kucheza mechi za nje.

DIAMOND PLATNUMZ (Zari Hassan)

Staa huyu kabla hajatemwa na Zari alikiri kumchepukia na soshiolaiti Hamisa Mobetto ijapokuwa awali aliishi kupinga.

Baada ya Diamond kukiri redioni na hata kuahidi kutambaa kwa magoti hadi Afrika Kusini kumwomba msamaha Zari, soshiolaiti huyo wa Uganda alimkubali na kuamua wayazike.

Hata hivyo miezi michache baadaye, Februari 14, 2018 kwenye siku ya wapendano, Zari alifanya maamuzi ya kumdampu kabisa Diamond.

Kwenye mojawepo ya mahojiano Zari alisema kuwa hata baada ya kukubali kumsamehe, Diamond aliendelea kumwonyesha dharau kwa kuendelea kujichanganya na mademu wengine akiwemo huyo Hamisa.

ERIC WAINAINA (Sheba Hirst)

Imepita miaka 10 toka mwanamuziki maarufu wa Afro Pop nchini Eric Wainaina alipomchepukia mkewe Sheba na mwanamuziki Valerie Kimani.

Valerie alikuwa akishiriki shindano la uimbaji Tusker Project Fame ambapo Wainaina alihusika kama produsa na kocha. Kwenye harakati hizo aliishia kupiga mechi ya ugenini na kumtundika ujauzito Valerie.

Mkewe Wainaina, Sheba alipogundua, aliamua kuomba talaka. Hata hivyo, msanii huyo hakuwa tayari kumpoteza mke wake na hivyo alitumia muda mwingi kumwomba msamaha akiahidi kutorudia tena.

Akifunguka hivi majuzi kuhusu majuto katika maisha yake, Wainaina alisema ikiwa kuna kitu kimoja anachojutia maishani ni huko kumchepukia Sheba jambo ambalo lilimuumiza sana. Anasema angelikuwa na uwezo wa kurejesha saa nyuma, basi ndicho kitu cha pekee ambacho angefuta.

Ndoa yake na Sheba sasa imegonga miaka 10 lakini wamekuwa wapenzi kwa kipindi cha miaka 21.

TERRENCE CREATIVE (Milly Chebet)

Oktoba 2019 mvunja mbavu Terrence anayefahamika kwa vichekesho vyake vya Kamami, alikiri kumchepukia mke wake Milly kipindi akiwa mjamzito.

Terrence alichepuka na binti mdogo kwa jina Anita Soina kipindi mke wake akiwa mjamizito. Terrence alijaribu kufunika stori hiyo isitoke lakini baada ya kuvuja, alikiri wazi wazi huku akimlaumu shetani kwa kumpoteza na kuahidi hatarudia tena.

Aidha alipuuzilia mbali tetesi kuwa Milly aliitisha talaka baada ya skendo hiyo, akishikilia kuwa hawatatalikiana ila watajitahidi kumaliza utata huo. Bado wapo pamoja.

KEVIN HART (Eniko Parrish)

Mwigizaji na mvunja mbavu huyu alikiri kumchepukia mke wake 2017 Parrish kipindi akiwa na ujauzito wa mtoto wao wa kwanza.

Taarifa zilidai kuwa rafiki yake mmoja ndiye aliyemseti na kumtishia kuachia video aliyomrekodi akichepuka ikiwa hatamlipa kiasi fulani cha pesa. Kwa kuhofia mabaya hata zaidi, Hart alitumia Instagram kumwomba msamaha mke wake. Kisha alipofanya mahojiano na kipindi cha The Breakfast Club alisema atakwenda amweleze ukweli wote mke wake akiwa na matumaini kwamba atamsamehe sababu hatawahi kurudia tena.

Hakika alisamehewa kwani mpaka sasa kapo hiyo ipo pamoja.

JAY Z (Beyonce)

Rapa wa kwanza bilionea duniani Jay Z naye alijikuta akimchepukia mke wake wa zaidi ya miaka sita Beyonce na kichuna ambaye hakuwahi kufahamika. Kipindi hiki kilikuwa kigumu sana na Beyonce aliishia kuachia albamu Lemonade iliyouza kweli kweli. Kwenye albamu hiyo iliyobeba ngoma Lemonade Beyonce husikika akimponda laivu Jay Z kwa kumchepukia na kichuna aliyeitwa Becky. Kwa kuhofia ndoa yake itavunjika, Jay Z alimwomba msamaha Bey na kuahidi kuwa mwaminifu huku akimtaka ampe fursa ya mwisho ya kuotesha penzi lao. Hakika Beyonce alimsikiza na ndoa yao imerudi kwenye mstari.