Makala

KIKOLEZO: Wamechukua wameweka kisha, waah!

December 11th, 2020 1 min read

Na THOMAS MATIKO

TUMEFIKIA upeo ambao kwa wanaoulewa muziki, hawaufanyi kwa sababu ya mapenzi ya muziki kama ilivyokuwa zamani, ila wanaufanya muziki kama biashara.

Sasa basi kufanya muziki kwa mapenzi, na kufanya muziki biashara ni vitu viwili tofauti.

Kufanya muziki kwa mapenzi na ari ni kwa sababu unapenda tu kuimba. Hiyo huwa kazi rahisi. Ila kufanya muziki biashara hapa ndio kuna kizungumkuti. Hoja kubwa hapa huwa ni kujua namna ngoma hiyo itakavyoweza kuingiza pesa. Ngoma hiyo inaweza kuingiza pesa endapo tu itapata umaarufu hata maishairi yakiwa ovyo.

Angalia kwa mfano Waah!, yake Diamond Platnumz na Koffie Olomide. Ni mastaa wawili waliokurupuka studio na kurekodi ngoma haraka haraka. Hawakuchukua muda kama ilivyo kawaida yao.

Ukiwa msikilizaji makini utangundua kwamba ngoma ni kawaida sana ila imetembea na kupata umaarufu mkubwa. Siri ya ngoma hii kuwa kubwa ni nini haswa? Hapo sasa ndio yale maujanja ya muziki biashara yanapoingia na kufanya kazi. Kwa mfano Diamond alihakikisha anawekeza sana kwenye video ya ngoma hiyo.

Makala ya leo yanalenga kuangazia maujanja waliyotumia wasanii walioorodheshwa na Google katika nafasi sita za kwanza mwaka 2020, wenye kazi zilizotazamwa mara nyingi zaidi nchini. Kumbuka hii ni tofauti kabisa na ngoma kupata ‘views’ nyingi, ila ngoma iliyotokea kutazamwa mara kwa mara. Yaani kwa marudio na mashabiki ‘most watched’. Wengi wa wasanii wameshatambua maujanja ya kuhakikisha kazi zao zinatazamwa mara kwa mara kwa namna wanavyozisukuma.