Makala

KIKOLEZO: Watazengua 2020?

January 17th, 2020 3 min read

Na THOMAS MATIKO

TUSHAANZA kuuzoea mwaka mpya, tayari tunakaribia kumaliza wiki ya tatu.

Na ukiwa ni mwaka mbichi, tayari matukio kwenye tasnia ya burudani yameshaanza kutokea.

Kuna bifu kati ya Avril na Naiboi iliyofufuliwa hivi majuzi kwa kisanga kilichotokea 2018, kisha rapa Khaligraph Jones yupo vitani na marapa wa Nigeria na vitu kama hivyo. Matukio kama haya ndio hunogesha showbiz ya +254, bila ya kusahau kiki.

Mpaka sasa hatujashuhudia kiki yoyote ile. Lakini si ndio mwaka unaanza? Naamini tutashuhudia visa kibao vya kiki mwaka huu kama tu ilivyotokea 2019 na wahusika kwa mtazamo wangu watakuwa ni wale wale. Listi hii hapa ya walevi wa kiki tunaopaswa kutarajia vituko zaidi kutoka kwao mwaka huu.

OTILE BROWN

Kama kuna mtu mmoja ambaye kiki zake ziliishia kuwa kawaida, basi ni Otile. Alifanya tabia ya kuachia ngoma mpya na inapoanza kutrendi, anaifungia kisha kulaumu watu fulani fulani kwa mkosi huo. Ishu inapozua hoja kwa kutrendi Otile anarejesha wimbo na unaishia kupata ‘views’ za kutosha. Alifanya hivi kiasi cha kuwakera mashabiki walioanza kumshurutisha ajitahidi kuwa mbunifu sasa sababu walikuwa wameshazoea kiki zake.

Otile pia alitumia mahusiano yake na mademu kutengeneza kiki za kusukuma kazi zake. Vera Sidika ni mfano, pia mpenzi wake Nabayet mliona. Alipoachana naye akatoa wimbo, waliporudiana tena akatoa wimbo. Ni kitu alichokifanya pia na Vera. Sasa naskia juzi kadai hakumtongoza Vera ila ni yeye ndiye aliyemwingiza box. Itakuwa jamaa anajianda kuachia ngoma mpya? Acha tusubiri.

RINGTONE

Mpaka leo sijamwelewa Ringtone. Mwaka 2019 wote kama sikosei aliachia ngoma moja pekee. Mwaka 2019 dhamira ya Ringtone haikuwa kuachia ngoma, ilikuwa ni kuhakikisha anasalia kuwa gumzo kwenye showbiz.

Ndio sababu alighushi barua akidai kufurushwa kutoka mtaa wa kifahari wa Karen kwa sababu ya kufuga ng’ombe kwenye mtaa wa kitajiri.

Mr Seed alipotibuana na Bahati, Ringtone alijigeuza msemaji wake. Aliponda sana Willy Paul na kina Bahati. Nakumbuka akibeba bango ‘I need a Wife’ lenye maandishi kwamba anasaka mke. Ndio ujue hakuwa anatania, Ringtone alienda na bango hilo hadi kanisani. Alianza drama hizi baada ya kiki zake za kumtaka Zari kimapenzi kugonga ukuta. Pia alitumia sana skendo za Rose Muhando kuwaponda watu wengi hasa wasanii wenyeji wake, mwisho wa siku wakaishia kutoa ngoma. Kwa mwaka huu, sijui tutegemee nini ila Ringtone kwa hulka zake, lazima ahakikishe anafanya jambo la kuzungumziwa.

ERICK OMONDI

Utakubaliana na mimi kwamba ni mbunifu sana kwenye kiki zake. Huwezi kujua utarajie nini kutoka kwa Ericko. Anaweza kufanya lolote ilimuradi tu ahakikishe jina lake lipo sio tu midomoni mwenu bali pia machoni mwa kampuni kadhaa ambazo zimekuwa zikimpa kazi kama mhamasishaji (Influencer) wa bidhaa zao.

Alituzengua kaachana na Mwitaliano wake Shantel, tukamzungumzia sana na miezi michache baadaye wakaonekana pamoja. Ericko alibisha sana kuwa kwenye mahusiano na Jackie Maribe ila mwaka jana waliweka wazi kwamba wana mtoto. Kisha wakaanza kula bata pamoja na kutengeneza picha eti wamerudiana. Wiki chache baadaye tukamwona Shantel. Na katika kufunga mwaka, alihakikisha bado mnamzungumzia kwa kuwakutanisha wanawake hao wawili Shantel na Maribe. Mafisi walibaki kumsifia kwa kuongeza ‘gangster points’. Huu mwaka acha tusubiri.

WILLY PAUL

Mzee masifa huwezi kumfungia nje ya listi hii. Anapenda sana skendo zake ambazo huja kama kiki na alizitumia sana kusukuma ngoma zake.

Staili ya Pozee ni tofauti, anaweza kuzua skendo leo akasubiri ipoe kisha ndio aachie wimbo. Unakumbuka akitrendi kwa kumzaba demu makofi hadharani?

Kisha baadaye alidai alikuwa akimrekebisha mdogo wake aliyemkimbia mume wake? Hivi pia unakumbuka akitishia kumpiga mtu risasi baada ya kuzozania eneo la kuegesha magari? Kiki zake na Nandy nani kasahau? Bifu aliyoilazimisha na Rayvanny nani hakuioana? Mwenyewe alikiri baadhi ya vitu anavyofanya ni kwa ajili ya biashara.

TIMMY T’DAT

Sio mzungumzaji ila ni mkali wa vitendo. Kiki za Timmy hukuacha kinywa wazi na kwa kawaida huhusiana na kazi zake.

Mwaka jana alitrendi kwa vituko aina aina, hasa alipoanza kuwa karibu na rapa wa kike kutoka Bongo, Rosa Ree. Kuna video ya wimbo walitoa iliyowaonyesha wakiwa uchi wa mnyama kwenye maji huku akiwa amemshika Rose Ree matiti. Bado wanakana kuwa kwenye mahusiano na kusisitiza ni washikaji tu. Kiki za Timmy lazima mwanamke ahusike, na ni kama vile yeye huwatumia kusukuma brandi yake, kisha anasepa au ndio sijui inakuwaje. Mwaka jana ilikuwa zamu ya Rosa Ree, mwaka uliotangulia 2018 ilikuwa ni Dela, huu mwaka sijui atakuwa nani.