Michezo

Kikosi cha Barcelona katika hatari ya kutangazwa muflisi

November 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

BARCELONA iko katika hatari ya kutangazwa muflisi iwapo wanasoka wake hawatakubali kupinguziwa posha zaidi kwa mara nyingine.

Baadhi ya masupastaa wa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania wamekubali kupunguziwa mshahara kwa hadi asilimia 70 tangu ujio wa janga la corona.

Ingawa hivyo, hali ya fedha kambini mwa Barcelona bado hairidhishi huku kikosi hicho kikikadiria hasara ya Sh12 bilioni kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa hesabu kufikia mwisho wa Oktoba 2020.

Kufikia sasa, madeni ya Barcelona yamekadiriwa kufikia Sh62 bilioni huku mapato yao kutokana na msimu wa 2019-20 yakiwa Sh17 bilioni pekee.

Hali tete ya kifedha kambini mwa Barcelona imewafanya vinara wa kikosi hicho kuanzisha mchakato wa kushiriki mjadala mpya na wachezaji wake ili kuwashawishi kukubali kupunguziwa ujira.

Kwa mujibu wa kituo cha Redio cha RAC1 jijini Catalonia, Barcelona wana hadi Novemba 5, 2020, kufikia muafaka.

Iwapo Barcelona watashindwa kupunguza matumizi yao kwa hadi Sh23.9 bilioni na kuwaanikia vinara wa La Liga kuhusu jinsi wanavyopanga kuafikia hayo, basi mabingwa hao mara tano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) watakuwa katika hatari ya kutangazwa wafilisi.

Barcelona wamekuwa na misukosuko mingi katika miezi ya hivi karibuni kiasi kwamba nyota wao Lionel Messi aliwahi kuwasilisha ombi la kutaka kuondoka uwanjani Camp Nou mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Hata hivyo, vita vya kukabiliana na Barcelona mahakamani kuhusiana na kifungu cha kuruhusu Messi kuagana na waajiri wake kulimchochea nahodha huyo kupiga abautani na kusitisha mipango ya kutua Manchester City alikokuwa aungane na kocha wake wa zamani, Pep Guardiola.

Mwezi mmoja umepita tangu Barcelona warefushe kandarasi za wachezaji Gerard Pique, Frenkie de Jong, Clement Lenglet na Marc-Andre ter Stegen.

Pique alikubali kupunguziwa mshahara wake kwa hadi asilimia 50 alipotia saini kandarasi mpya huku wenzake watatu wakikubali kukatwa ujira kwa hadi asilimia 30.

Baada ya kujiuzulu kwa Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu, Bodi mpya itasimamiwa na Carles Tusquets hadi uchaguzi wa viongozi wapya utakapofanyika mwaka ujao.

Mnamo Aprili 2020, wanachama sita wa Bodi ya Usimamizi kambini mwa Barcelona walijiuzulu. Mbali na Emili Rousaud na Enrique Tombas waliowahi kushikilia wadhifa wa urais wa Barcelona, wanachama wengine wa Bodi waliong’atuka ni wakurugenzi wanne wakiwemo Silvio Elias, Josep Pont, Jordi Calsamiglia na Maria Teixidor.

Katika barua yao ya kujiuzulu, sita hao waliangazia pia jinsi Barcelona inavyokosa mpango madhubuti wa kukabiliana na athari za kifedha zitakazotokana na virusi vya homa kali ya corona.