Habari Mseto

Kikosi chatumwa Nyeri kuzima magenge

July 3rd, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

KIKOSI maalum cha kukabiliana na magenge ya uhalifu, kimetumwa katika Kaunti ya Nyeri kufuatia ripoti kuwa wabunge wawili wanaunda makundi ya vijana kwa ajili ya kuyatumia kisiasa.

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa afisa wa ngazi ya juu ametumwa eneo hilo kutoka Nairobi kuongoza operesheni ya kuvunja makundi hayo.

Ripoti za kijasusi zinaeleza kuwa wabunge wanaohusika wanaegemea makundi pinzani yanayovutana katika Jubilee ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’ na wanaunda makundi hayo kutumika kutisha wapinzani na kuvuruga mikutano ya wapinzani.

Mmoja wa wabunge hao ni mfuasi sugu wa ‘Tangatanga’ huku mwenzake akifahamika kwa kuwa mtetezi wa ‘Kieleweke’.

Hatua ya kufanywa kwa operesheni hiyo ilichukuliwa na makao makuu ya polisi kufuatia kisa cha wikendi iliyopita ambapo hafla ya maendeleo ya Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri ilitatizwa na kundi la vijana wa moja ya makundi hayo.

Duru zilieleza kuwa wabunge wanaohusika wanafufua makundi ya Mungiki, kila mmoja katika eneo bunge lake, na ni moja ya makundi hayo ambalo liliongoza kuvuruga mkutano wa Bw Kiunjuri pamoja na kwenda nyumbani kwa diwani wa wadi ya Muruguru, Simon Muturi ambapo wanadaiwa walitishia kumuua.

Vitisho hivyo vimemlazimu diwani huyo kuhama nyumbani kwa kuhofia maisha yake na sasa anaishi hotelini.

Mnamo Jumanne, Spika wa Bunge la Kaunti ya Nyeri, John Kaguchia aliagiza diwani huyo kuongezewa usalama.

Diwani huyo aliambia bunge hilo kuwa kundi la watu wapatao 20 walifika nyumbani kwake wakiendesha bodaboda na kuacha ujumbe kuwa wanataka kichwa chake.

Alisema hata baada ya kuandikisha taarifa kwa polisi hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

Lakini kulingana na duru za polisi, diwani huyo yuko salama kwani kuna kikosi maalum cha maafisa sita wasiotambulika ambao wamepewa maagizo ya kuhakikisha hakuna chochote kinachomtendekea, na pia kukabilina na yeyote atakayethubutu kuhatarisha maisha yake.