Michezo

Kikosi kizima cha Bandari kuvinjari Afrika Kusini

June 20th, 2019 1 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

WACHEZAJI wote 30 wa kikosi cha Bandari FC watakuwa kwenye msafara wa timu hiyo kwenda Afrika Kusini ambapo wanatarajia kupiga kambi ya mazoezi na kucheza mechi kadhaa za kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2019-20.

Akizungumza Jumatano asubuhi na Taifa Leo mjini Mombasa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Bandari FC, Edward Oduor alisema kwa kuwa ni wakati wa kujitayarisha kwa msimu mpya, wachezaji wote watakuwa kwenye msafara wa kwenda Afrika Kusini.

“Hatuwezi kumuacha mchezaji yeyote kwani ni kipindi cha kumpa fursa kocha Bernard Mwalala kujionea hali ya uchezaji wa kila mchezaji kabla ya kuchagua wanasoka watakaowakilisha timu yetu msimu ujao,” akasema Oduor.

Alisema kati ya wachezaji watakaokuwa kwenye msafara huo ni sajili wao wawili wapya, kiungo Danson Chetambe kutoka Zoo Kericho na winga Wycliffe Kasuti kutoka Sofapaka ambao walitarajiwa kukamilisha usajili wao ama Jumatano jioni au leo Alhamisi asubuhi.

Oduor hakuweza kuthibitisha ni lini timu hiyo itakapoondoka nchini lakini alisema kuwa itakuwa wakati wowote wiki ijayo.

“Tuko kwenye mipango ya safari ya kwenda huko Afrika Kusini kwani tutaondoka wiki ijayo,” akasema.

Onyo

Kuhusu mjadala unaoendelea kuhusu golikipa Farouk Shikhalo, Oduor ametoa onyo lingine kwa klabu ya Young Africans (Yanga) kukoma kutangaza kipa huyo kuwa ni wao ama wameshamsajili kuwa watachukua hatua za kisheria.

“Ninavyofahamu ni kwamba Shikhalo ana timu ya taifa ya Harambee Stars nchini Misri na ni mchezaji wetu halali na kamwe hatutanyamaza kimya ikiwa Yanga itamsajili kupitia mlango wa nyuma.

“Kuna mkataba kati ya Shikhalo na Bandari FC na mkataba huo lazima uheshimiwe. Timu yoyote inayotaka kumsajili ni sharti ifuate kanuni zinazohitajika. Atakayekwenda kinyume na mkataba huo, tutachukua hatua za kisheria kwa kwenda kinyume na sharia za FIFA,” akasema.