Shangazi Akujibu

Kila wakati tukipatana lazima achovye asali, yaani ni kama sheria

April 18th, 2024 1 min read

Hujambo Shangazi,

Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye nampenda kwa dhati. Tatizo lake ni kuwa kila wakati tukikutana ni lazima adai asali. Hiyo ni sawa?

Huenda hali hiyo inatokana na maumbile yake au hisia nzito za kimapenzi ambazo watu huwa nazo uhusiano ukiwa mchanga. Jaribu kumpa muda uone kama joto lake litapungua aweze kutulia.

Meidi anampagawiza mume wangu nyumbani

Shangazi, nina mume na watoto wawili. Mwanamke mfanyakazi wetu wa nyumbani anatishia ndoa yangu. Mienendo yake hapo nyumbani imeteka hisia za mume wangu. Nifanyeje?

Ninaamini kwamba unamfahamu vyema mume wako. Kama umeona dalili za kutosha kuwa anaweza kunaswa kimpenzi na mfanyakazi wenu, itabidi uchukue hatua kuokoa ndoa yenu. Mwachishe kazi utafute mwingine.

Urafiki wa miezi miwili unatosha kuota penzi?

Nina miaka 30. Kuna mwanamume tumekuwa marafiki kwa miezi miwili sasa na ananiambia ananipenda. Mimi pia nampenda lakini simwamini.

Nahisi hofu yako ni kwa sababu hujamfahamu vyema mwanamume huyo kwa sababu mmejuana kwa muda mfupi tu. Unahitaji muda zaidi umfahamu vyema ndipo uweze kufanya uamuzi unaofaa.

Kuna fununu mpenzi ananicheza nikiwa mbali

Hujambo Shangazi. Ninafanya kazi mbali na mpenzi wangu. Marafiki wameniambia mpenzi wangu ameanza kunicheza na wanaume wengine na habari hizo zinanikosesha amani.

Usikubali mambo ya kuambiwa kumhusu mpenzi wako. Badala yake, kuchunguza wewe mwenyewe ujue ukweli wake. Inawezekana wanaokupa habari hizo wanaonea wivu mapenzi yenu.