Habari Mseto

Kilabu cha densi za uchi chafungwa

January 9th, 2020 1 min read

Na Stephen Munyiri

NAIBU Kamishina wa Mathira Mashariki, Bw Patrick Messo amethibitisha kwamba kilabu kimoja kinachodaiwa kuruhusu usakataji densi watu wakiwa uchi kimefungwa baada ya malalamishi ya wakazi.

Klabu hicho kwa jinakinachopatikana katikati mwa mjini Nyeri kilifunguliwa mwezi moja uliopita na kumekuwa na malalamishi kwamba kinaendeleza tabia zisizokuwa za kimaadili.

“Sisi tunawafanyia wananchi kazi na baada ya kupokea malalamishi yao, tulifanya uchunguzi wetu na tukagundua kwamba baadhi ya mambo yanayovuruga maadili yalikuwa yakiendelezwa kwenye klabu hicho,” akasema Bw Messo.

Kilipofunguliwa, vijana kwa wazee walikuwa wakimiminika klabuni humo kwa kishindo kutazama mabinti ambao walikuwa wakicheza aidha wakiwa nusu uchi au uchi.

Taifa Leo ilipotembelea klabu hicho, ilikuta kwamba kufuli kubwa imetiwa kwenye mlango wake bila notisi kwa wateja kwamba kilikuwa kimefungwa.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wameonyesha kukerwa kwao na hatua hiyo ya serikali wakisema inawanyima starehe zao wala hawajawahi kushuhudia densi za uchi klabuni humo.