Makala

Kilele cha ukatili polisi wakiendelea kulenga wanahabari

Na BENSON MATHEKA August 9th, 2024 2 min read

POLISI wa Kenya wanaendeleza ukatili dhidi ya wanahabari wakifuatilia maandamano, licha ya mashirika ya humu nchini na ya kimataifa kuwataka kuheshimu uhuru wa kukusanya na kusambaza habari.

Mnamo Alhamisi, wanahabari wa humu nchini na wa kimataifa waliokuwa wakifuatilia maandamano ya Nane Nane, walishambuliwa na maafisa wa polisi kwa kuwafyatulia vitoa machozi.

Hatua hii ilionekana kuwatisha wanahabari wasifichue ukatili wa maafisa wa polisi kwa waandamanaji waliodumisha amani.

Mwanahabari wa CNN Larry Madowo, alinusurika polisi walipomfyatulia mkebe wa kitoa machozi akitangaza moja kwa moja kutoka kati kati mwa jiji wakati wa maandamano ya Nane Nane.
Madowo, hakujeruhiwa katika kisa hicho ambacho afisa wa polisi aliyekuwa juu ya lori alipomrushia kitoa machozi kwenye makutano ya barabara za Wabera na Kenyatta.

“Ananilenga mimi, ananilenga moja kwa moja,” alisema Madowo ambaye alikuwa akitangaza mbashara kutoka eneo hilo huku mkebe wa gesi ya kutoa machozi ukipita karibu sana na kichwa chake.

Shambulizi hilo lilinaswa kwenye video iliyopeperushwa katika runinga ya kimataifa ya CNN ya Amerika.

Tukio hilo lilijiri saa chache baada ya Waziri Msaidizi wa Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Binadamu, Bi Uzra Zeya kuonya serikali ya Kenya kuhusu ukatili wa polisi dhidi ya wanahabari na ukiukaji wa jumla wa haki za waandamanaji wanaodumisha utulivu.

” Katika mazungumzo yangu na Rais Ruto na maafisa wakuu wa Kenya, nilishutumu ghasia zilizofanywa dhidi ya waandamanaji waliodumisha amani, watetezi wa haki za binadamu, na waandishi wa habari, na kuhimiza kulindwa kwa uhuru wa kimsingi wa kukusanyika kwa amani na kujieleza, kama ilivyo katika katiba ya Kenya,” alisema.

Mwanahabari mwingine Cecilia Ngunjiri, pia alijeruhiwa na polisi akifuatilia maandamano ya Nane Nane jijini Nairobi.

Siku hiyo pia, afisa wa polisi alinaswa kwenye picha akimpiga teke mwanabahari nje ya jumba la Nation Center, Nairobi.

“Vitendo vya polisi vilivyolenga kudhuru wanahabari katikati mwa jiji havikubaliki kabisa,” aliandika mwanahabari wa runinga ya Citizen Stephen Letoo.

Mwezi jana, wanahabari nchini waliandamana kulalamikia ukatili wa polisi dhidi yao na kutaka ukomeshwe baada ya mwanahabari Catherine Wanjeri Kariuki kupigwa risasi mguuni na afisa wa polisi mjini Nakuru akifuatilia maandamano ya Gen Z.

Shirika la kimataifa la Reporters Without Borders (RSF) ambalo limekuwa likifuatilia vitendo vya polisi kwa waandishi wa habari, linalaumu serikali kwa kuendelea kunyanyasa wanahabari.

Mkuu wa Uchunguzi wa Shirika hilo Arnaud Froger, amelaani ukatili unaotendewa wanahabari nchini Kenya akitaja matukio ya hivi punde kama kilele cha ukatili bila adhabu kwa wanaoutekeleza.

“Kukosa kwa maafisa wa serikali kutambua polisi wanaohusika licha ya baadhi ya visa kunaswa kwenye video ni aibu kubwa ya uepukaji wa adhabu,” Froger alisema.

Alisema kwamba RSF imewasiliana na polisi wa Kenya na kuwataka kufanya uchunguzi wa kina kuhusu visa sita vya ukatili dhidi ya wanahabari na kuweka wazi matokeo ya uchunguzi huo na kuchukulia hatua wanaotekeleza dhuluma hizo.