Kilifi Ladies FC yaomba kushiriki ligi ya Pwani

Kilifi Ladies FC yaomba kushiriki ligi ya Pwani

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

KILIFI Ladies FC inatarajia kushiriki katika ligi ya jimbo la Pwani ambayo haijaanza msimu huu.

Hayo ni kulingana na Mfadhili Mkuu wa Kilifi Ladies FC, Bendera Wilson Charo aliyesema wanafanya mazungumzo na tawi la Kilifi la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kutaka kushiriki katika ligi hiyo.

“Tunaendelea na majadiliano na maofisa wa FKF tawi la Kilifi juu ya ombi letu la kutaka kushiriki katika ligi hiyo ya jimbo huku tukiitayarisha timu yetu kwa kucheza mechi kadhaa za kirafiki za kujipima nguvu katika sehemu mbalimbali za jimbo hili,” akasema Bendera.

Bendera anasema wanafanya matayarisho ya kuunda kikosi imara kitakachoshiriki kwenye ligi hiyo na akaeleza matumaini yake kuwa watakubaliwa kuwekwa katika ligi hiyo na FKF. Kikosi hicho kilianza maandalizi tangu mwaka uliopita ambapo imecheza mechi kadhaa za kirafiki.

Miongoni mwa maandalizi ya timu hiyo ilicheza mechi kadhaa za kirafiki katika kaunti za Lamu, Mombasa, Ukunda na Tana River na mwishoni mwa wiki hii, inatarajia kufanya ziara ya kutembelea mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta kwa mechi mbili.

Kilifi Ladies inatarajia kushiriki mechi za kirafiki zitakazochezwa Jumamosi dhidi ya Murang’a Queens kutoka Kaunti ya Murang’a, jimbo la Kati na Crown Ladies ya hapo Voi ambayo itakuwa mwenyeji. Mechi nyingine itakuwa baina ya Crown Ladies na Murang’a Queens.

“Tumefanya matayarisho ya kutosha ya timu yetu ambapo wachezaji wanafanya bidii ya mazoezi ili tuweze kufanya vizuri katika mechi zetu zilizobakia za kujipima nguvu na hata tutakapoanza kucheza ligi,” akasema Bendera.

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi wawili wa MKU wapata ufadhili kwa ubunifu wao...

WhatsApp kuanza kutekeleza masharti mapya Jumamosi