Habari

Kilikuwa kibarua kigumu kutafuta, kutoa gari

October 11th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO na CHARLES WASONGA

INGAWA ajali ilipotokea Wakenya walikasirika na kulaumu serikali kwa kujivuta kuopoa miili ya marehemu na gari walimokuwa lilipozama, haikuwa kazi rahisi.

Ilibidi serikali na familia kutafuta msaada kutoka Afrika Kusini ili kufanikisha operesheni hiyo.

Wa kwanza kutoa huduma zake alikuwa ni raia wa Uswidi Volter Bassen ambaye alitoa ahadi ya kupata gari hili baada ya muda mfupi lakini naye akalemewa kutokana kile alitaja kama mawimbi makali ya chini ya bahari.

Ingawa hivyo, kuna wanaosema alibainisha lilipokuwa gari hilo na wakajijazia pengine ‘alinyamazishwa’.

Alikuwa mmoja wa wapigambizi 16 walioanza juhudi za kuopoa gari hilo na maiti za Bi Mariam Kighenda na bintiye waliokufa maji katika kivuko cha Likoni mnamo Septemba 29.

“Niligundua kuwa ukadiriaji wangu kuhusu hali hapa haukuwa sahihi,” akasema Bassen ambaye aliongea na wanahabari Ijumaa wiki jana.

Mnamo Oktoba 7, 2019, kikosi cha wapigambizi kutoka Afrika Kusini kiliwasili kuungana na wenzao kutoka humu nchini kusaidia katika shughuli ya uopoaji wa miili ya Bi Mariam Kighenda na mwanawe waliotumbukia katika kivuko cha Likoni.

Kikosi hicho kilihusisha wapinga mbizi watano waliokodishwa na familia ya Bi Kighenda kupitia Gavana wa Mombasa Hassan Joho kutoka shirika la Subsea na watatu waliokodishwa na serikali ya Kenya.

Gavana huyo alikabidhi familia Sh2 milioni, ili kusaidia kukodi wataalamu wa uopoaji kutoka Afrika Kusini baada ya familia kuchukua hatua ya kukodi wapiga mbizi binafsi ili kuharakisha uopoaji.

Matumaini ya kupata miili ya wawili hao yaliongezeka baada ya serikali kununua vifaa maalum vyenye uwezo wa kuona chini ya bahari.

“Tuna matumaini kuwa shughuli hii itakamilika hivi karibuni kwani wataalamu wenye tajriba ya hali ya juu watafanya kazi na wenzao wa hapa nchini wakitumia kamera zenye uwezo mkuu wa kuona sakafu ya bahari,” alisema mwenyekiti wa shirika la huduma za feri Dan Mwazo.

Siku ya Jumatano baada ya kutambua sehemu lilipokuwa gari la marehemu, wataalamu hao walifunganya kurudi nchini mwao lakini ilidaiwa kuwa walirudishwa na Gavana Joho baada ya vikosi vya humu nchini kushindwa kutoa gari kufuatia kukosa vifaa vya kwenda katika sakafu ya baharini.

Ijumaa, Bw Joho alitetea jeshi la wanamaji akisema kazi hiyo haikuwa rahisi.

“Walihatarisha maisha yao kwenda chini ya bahari kufanikisha shughuli hii, haikuwa kazi ya mchezo na tunafaa kuheshimu vikosi vyetu vya usalama kwa ujasiri wao,” alisema Joho.

Aliwataka watu kutohusisha mkasa huo na ushirikina akisema ilikuwa ajali kama nyingine.

“Ajali ni ajali na hii ilikuwa ajali,” alisema.