Makala

KILIMO BIASHARA: Wakulima wa nyanya wanavyoendelea kuumia mikononi mwa mawakala

July 18th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

SEKTA ya kilimo inatoa mchango wake katika uchumi na mapato nchini Kenya.

Serikali huvuna ushuru usiomithilika kupitia sekta ya kilimo, kando na kuwa kapu la lishe.

Licha ya kuwa na sifa kuntu, wakulima wa nyanya wasio na wateja wa moja kwa moja sokoni wanaendelea kunyanyaswa na mawakala.

Mfanyabiashara huyu ambaye ni ‘daraja’ kati ya mzalishaji wa bidhaa na muuzaji kwa watumizi, anaaminika kuwa mwamuzi wa bei na ina maana kuwa ameishika mateka zinakozalishwa na sokoni.

Aidha, mawakala wanaaminika kuwa kufahamu ziliko bidhaa au mazao na wana ushawishi mkuu katika bei.

“Sisi tulio sokoni tunawategemea, kwani hutuondolea gharama ya kusafiri kutafuta mazao shambani, kuyasafirisha na kizungumkuti cha kuyapata,” mfanyabiashara wa nyanya na maparachichi eneo la Githurai akaambia Taifa Leo, akiomba jina lake lisichapishwe.

Alisema mbali na kuwaondolea gharama, mawakala huwafikishia mazao waliko, hilo wakilichukulia kama faida kwao.

Kwa baadhi ya wakulima wa nyanya, wasio na soko la moja kwa moja, tabasamu hiyo ni mahangaiko chungu nzima.

Mbali na kukandamizwa bei, upakiaji wa zao hili ni ule wa kumuacha mkulima akiuguza majeraha ya hasara.

Nyanya katika shamba la mkulima. Picha/ Sammy Waweru

Bw Muriuki Kamau, mkulima wa nyanya Kirinyaga analalamikia mawakala akidai wanapakia nyanya kupita kiasi.

Mkulima huyu akitumia mfano wa miaka ya tisini na sasa, anasema kuna tofauti kubwa sana katika suala la upakiaji.

Kwa kijumla, nyanya huuzwa kwa kreti na anasema miaka ya tisini kreti ilikuwa ya uzani wa kilo 60 na haikuborongwa.

“Kwa sasa mawakala wamezindua kreti ya kilo 130 ambayo inakarabatiwa kupakia hadi kilo 180,” anaeleza Bw Kamau.

Kulingana na mkulima huyu, licha ya bei ya nyanya kutotabirika, kreti ya kilo 130 na inayoborongwa wakati soko ni duni huuzwa hata chini ya Sh3, 000.

“Bei hiyo kwa mkulima ni hasara, ikizingatiwa gharama anayotumia kuzalisha nyanya ni ghali,” alalamika.

Hukuza nyanya kwenye shamba la ukubwa wa ekari saba na nusu, na anasema gharama ya matumizi kuzalisha ekari moja ni karibu Sh350,000.

Baadhi ya matumizi ni kuandaa shamba, pembejeo kama mbolea, mbegu, dawa dhidi ya magonjwa na wadudu, na leba-wafanyakazi. “Bei ya dawa ni ghali mno na inaendelea kuongezeka kila uchao,” anasema Bw Kamau.

Kulingana na Kamau ni kwamba kreti ya kilo 130 na ambayo imeborongwa kusitiri kilo 180 ikiuzwa chini ya Sh3, 000 ni hasara chungu nzima. “Ya kilo 60 tulipokuwa tukiiuza hata chini Sh2,000, hatukuona ikiwa hasara kwani bado ilikuwa inatuletea faida tukilinganisha na gharama ya kuizalishia.

“Kreti ya kilo 130 kuuzwa Sh3,000 ni hasara tupu. Hii ni changamoto kuu kwa wakulima wa nyanya, wanaendelea kuumia mikononi mwa mawakala,” ateta.

Hata hivyo, anadokeza kwamba wakati nyanya zimeadimika kipimo hicho huuzwa hadi Sh13,000 kwani mawakala hawana budi kuitikia. Huo ni wakati ambapo nyanya moja mijini huuzwa zaidi ya Sh15.

Bw Derrick Mutugi mkulima wa nyanya Kiambu anasema ili kukwepa kero la mawakala hujipeleka sokoni kutafuta wafanyabiashara wateja wa moja kwa moja.

“Wakati ninaendelea kutunza nyanya shambani, huanza kutafuta soko. Soko langu kuu ni Makongeni, Thika,” anaeleza Bw Mutugi.

Kutafuta wateja

Pia, mkulima huyu hutumia mitandao ya kijamii kama Facebook na WhatsApp kutafuta wateja.

Hata hivyo, Muriuki Kamau anasema kizungumkuti cha kujipelekea mazao sokoni huwa mawakala kushika mateka wafanyabiashara.

Pandashuka nyingine ni utozaji wa ada ya juu na halmashauri ya jiji, kanjo, wakati wa kupakua mizigo.

“Wawili hao wakiungana mkulima hana budi ila kukubali matakwa ya mawakala, la sivyo mazao yake yataozea hapo,” anasema Kamau.

Soko kuu la mkulima huyu ni Githurai, Kangemi na Marikiti, masoko yote yakiwa kaunti ya Nairobi na Kiambu.

Wataalamu wa kilimo kwa upande wao wanahimiza wakulima kujiunga na vyama vya ushirika ili kupata soko lenye bei bora.

“Iwapo wangekubali kujiunga na vyama vya ushirika, ingekuwa rahisi mazao yao kununuliwa kwa bei bora na kuwaepusha na masaibu yanayoletwa na mawakala,” anashauri mtaalamu Daniel Mwenda.

Mdau huyu pia anasisitiza umuhimu wa kukumbatia teknolojia ya kisasa, kutumia mitandao kama Facebook na Whats App katika kutafuta soko.