Makala

KILIMO CHA KISASA: Pata faida za unyunyiziaji kwa njia ya matone (drip irrigation)

August 29th, 2019 2 min read

Na GRACE KARANJA

KILIMO cha unyunyiziaji kwa njia ya matone (drip irrigation) ni njia au mfumo unaotumika katika uzalishaji wa mazao mbalimbali kama vile mboga, matunda na mimea mingine katika maeneo ambayo huwa na uhaba wa maji ama kwa lengo la kuleta ufanisi wa matumizi bora ya maji katika uzalishaji wa mazao.

Kupitia unyunyiziaji kwa njia ya matone, mkulima hunufaika kwa kupunguza gharama za shambani au bustani yake pamoja na kuokoa muda, hivyo basi hupata muda mwingi wa kushiriki shughuli zingine.

Pia kupitia njia hii, mkulima kuwa na uhakika wa kupata mavuno yake maana maji huweza kutumika kwa ajili ya mmea husika tu.

Mfumo wa unyunyiziaji maji kwa njia ya matone una uwezo wa kuokoa kiwango cha maji yanayotumika shambani na kuruhusu maji pamoja na virutubisho kupenyeza polepole hadi katika mizizi ya mimea.

Lengo kuu la kutumia mfumo huu ni kuhakikisha kwamba maji yananyunyiziwa moja kwa moja kwenye mizizi na kupunguza kutowekea kwa unyevu hewani.

Mfumo huu hutumika katika mashamba yaliyo wazi na pia katika vivungulio.

Kwa kutegemea njia ambazo mkulima atatumia kuunganisha, kuendeleza matumizi ya vifaa hivyo pamoja na kuvidumisha, mfumo huu unaweza kuwa wa ufanisi mkubwa ikilinganishwa na mifumo mingine ya unyunyiziaji maji shambani huku wataalamu wakisema kuwa mkulima anaweza kuutumia hadi kipindi cha hadi miaka 10 iwapo atatunza kikamilifu.

“Jambo la muhimu ni kudumisha mifereji kwa kuangalia isiingie uchafu unaoweza kuzuia maji kama vile nyasi na mchanga, ambazo zinaweza kufunga mashimo ya matone. Iwapo mkulima atazingatia kanuni za kitaalamu zinazohitajika katika kutunza mfumo huu, huenda akautumia hadi muda wa miaka 10,” anasema Julius.

Hii ndiyo njia rahisi ya kuendeleza kilimo ambapo mara kwa mara wakulima wamekuwa wakishauriwa kutumia mfumo wa njia ya matone katika kunyunyizia mimea shambani lakini wengi wao hawajaweza kukumbatia mfumo huo kwa sababu ya kutofahamu gharama yake.

Kulingana na Julius Nduati mtaalam wa kilimo kutoka Kampuni ya African Soil and Crop Care Ltd, anashauri wakulima kutoanza na kipande kikubwa cha ardhi kwani itakuwa ni gharama kubwa hasa kwa wakulima ambao hawana uwezo mkubwa.

“Ninamshauri mkulima yeyote ambaye ana ari ya kuanza kilimo kwa kutumia mfumo huu aanze kwa kulima kipande kidogo cha ardhi. Kwa mfano, ni vyema kuanza na robo ekari. Hii ni kwa sababu gharama itakuwa ya chini huku mkulima akiendelea kujifunza mengi yatakayomsaidia kupanua kilimo chake katika siku za usoni,” anashauri mtaalamu huyu.

Mtaalamu huyu anasema mfumo huu hupunguza ukuaji wa magugu shambani kwa kiwango cha juu, hupunguza magonjwa ya fangasi (kuvu) pamoja na kuondoa unyevu katika matandazo miongoni mwa manufaa mengine.

Pia hupunguza mmomonyoko wa udongo kwa sababu maji hutoka kwa mfereji ambao una matone.

Hata hivyo, kuna vifaa ambavyo mkulima atahitaji kununua ambavyo hutumika ili kufanikisha kilimo hiki.

Mshauri huyu wa kilimo anatupa mwongozo wa kununua vifaa hivi vya ardhi ya nusu ekari.

Mwanzo kabisa, ni kufahamu chanzo cha maji na kuyaweka katika pipa ambalo mkulima ataunganisha na mifereji ambayo hutoa maji kutoka kwa chanzo kikuu na mkulima anashauriwa kuifukia chini ili kuzuia uharibifu wa mara kwa mara.