Makala

KILIMO CHA KISASA: Ukuzaji wa nyanya ala mpya ya kufukuza ufukara katika kaunti

August 29th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

UCHUMI wa Kenya hutegemea kilimo kwa takribani asilimia 80.

Mbali na kulisha nchi na kutoa ajira isiyo rasmi kwa vijana wengi, kilimo pia hutoa malighafi ambayo hutumika sana katika viwanda kutengeneza bidhaa na kuongeza thamani kwa mazao mengine.

Nyanya ni mmea ulio na thamani kubwa sana na wakulima wanaojitosa katika ukuzaji wake wana kila sababu ya kujivunia.

Katika Kaunti ya Kirinyaga kwa mfano, kuna wakulima wengi kiasi cha haja wanaojishughulisha na kilimo hiki kama kitega-uchumi.

Mbali na kuwepo kwa mimea mingine inayofanya vizuri kama vile mpunga, kahawa, majani-chai na maharagwe, nyanya pia hunawiri sana.

Katika eneo la Nyangati, Kaunti Ndogo ya Mwea, Akilimali ilikutana na Bw David Gitari Githinji ambaye amekuwa mkulima wa nyanya tangu mwaka wa 2013.

Anasema kwamba kilimo ndiyo kazi yake ya kila siku inayompa ajira.

Kutoka wakati huo, amekuwa akikuza nyanya katika thuluthi moja ya shamba lake la ekari moja.

Japo nyanya zimempa mafanikio mengi, anasisitiza kuwa ni lazima mkulima awe hodari katika kilimo chenyewe.

Yeye hununua miche ya nyanya zake kutoka kwa kampuni ya Greenlife iliyoko Athi River, Kaunti ya Machakos. Hununua miche ya umri wa wiki mbili baada ya kuota na kuchipuka ardhini.

Kwa kawaida, huwa ananunua jumla ya miche kama 2,000 kwa Sh14 kwa kila mmoja.

Halafu anatayarisha ardhi yake siku chache kabla ya kupanda na baada ya upanzi, yeye hunyunyizia maji kila mara hadi kila mche uwe thabiti udongoni.

Baada ya siku tatu hivi, Bw Gitari hutia mimea yake mbolea ili kuiwezesha kupata madini muhimu na kukua kwa haraka. Ili kupigana na wadudu ambao wanaweza kuharibu mmea huu, yeye hutumia dawa ili kuwazuia na kuwaangamiza viwavi wachache wanaoweza kupatikana. Jambo hili huwa analifanya kila baada ya juma moja.

Maji ya kunyunyizia mimea yake hutoka kwenye Mto Murubara ambako huwa anayaelekeza kutumia mifereji na kuyahifadhi katika matangi makubwa yaliyoko shambani mwake.

Ndani ya kivungulio (Greenhouse), Bw Gitari huwa anatumia vijiti na nyuzi ili kuzipa nyanya mahali pa kuegemea na kukua zikiwa imara bila ya kuanguka. Pia huwa akipania kunyunyizia maji mara mbili kwa siku.

“Kivungulio kina umuhimu zaidi kwa vile maji unayohitaji kunyunyizia si mengi kwa kuwa kivuli kinazuia jua kali. Pia mazingira ya kivungulio huzuia mvua nyingi ambayo inaweza kuharibu mmea huu,” Gitari anasimulia.

Kulingana naye, kupogoa au kukata majani yaliyokauka na mengine yaliyo makubwa mno kwenye nyanya kunasaidia kuupa mmea nafasi nzuri ya kupata madini ya kutosha. Hili huwezesha mmea kukua kwa haraka ukiwa na afya njema.

Baada ya kipindi cha miezi miwili, Gitari anasema nyanya zake huwa tayari kuanza kuvunwa. Anapoanza, huwa inamchukua miezi minne ya kuvuna ndipo mazao yote yakamilike shambani.

Katika miezi hii, huwa anachuma nyanya mara moja au mbili kwa wiki maanake nyanya hukua, kukomaa na kuiva kwa mfululizo.

Anasimulia kwamba katika msimu wote wa kuvuna, kila mmea una uwezo wa kutoa kati ya nyanya 130 – 200.

Bei

Wakati hakuna nyanya nyingi sokoni, yeye huuza nyanya zake kwa zaidi ya Sh5,000 kwa sanduku la kilo 150.

Hili ni pato zuri hasa ikizingatiwa kwamba shamba lake humtolea zaidi ya masanduku 200 ya kilo 150 kwa msimu mmoja. Bw Gitari anasimulia kwamba baadhi ya changamoto ambazo huwa anakumbana nazo ni uvamizi wa wadudu, magonjwa na bei ya chini kwa mazao yake kila anapofikisha bidhaa sokoni misimu mingine.

Bei hushuka pakubwa pale ambapo nyanya zimeingia sokoni kwa wingi kutoka kwa wakulima wengi wa mbali na wa karibu. Hili wakati mwingine humweka katika ulazima wa kuuza nyanya zote kwa wakati ambako huwa zinaharibika baada ya muda.

Kwa kawaida, kila anapovuna, yeye huwa anakodisha gari la kusafirisha nyanya zake sokoni. Soko haswa ambalo yeye huwa anapeleka bidhaa hii ni Kawangware jijini Nairobi japo masoko mengine katika maeneo mbalimbali ya Narok, Naivasha, Gilgil na Ol Kalou.

Anasema kuwa kuwekeza katika kutengeneza hema kunahitaji hela nyingi.

Hata hivyo, hajutii kilimo hiki cha hema maanake kinamwezesha kupata mavuno mengi na bora na kwa hivyo, kusimamia gharama aliyotumia katika ujenzi wake na kumpa faida pia.

Hema lake ni la kampuni ya Amiran ambayo inahusika na kilimo cha mimea mbalimbali kupitia mahema. Anasema kilimo kinalipa na watu zaidi wanapaswa kujihusisha nacho maanake chakula kinahitajika kwa wingi kadri idadi ya watu inavyoongezeka nchini.