Makala

KILIMO CHA MBOGA: Ethiopian kales ni rahisi kukuza, huchukua muda mfupi kuchumwa

November 21st, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MBOGA aina ya Ethiopian kales huwa na umbo sawa na la sukumawiki japo majani yake ni madogo.

Mboga hii inaenziwa sana Barani Afrika, Kenya ikiwamo, kwa sababu haina asidi.

Wenye shida ya asidi au vidonda vya tumbo wanahimizwa kula mboga za kienyeji kwa wingi.

Kimsingi, zina faida lukuki kiafya.

Mboga aina ya kansara hustawi maeneo yoyote nchini muradi tu udongo uwe wenye rotuba. Kulingana na wajuzi wa masuala ya kilimo, udongo usiwe unaotuamisha maji na uchachu (asidi) wake uafikie kigezo kinachohitajika kufanikisha ukuzaji wa mboga.

Kilimo cha kansara hakina kikwazo kwani mbegu zake hutolewa kwa mboga zilizokomaa, aghalabu zilizofikisha umri wa miezi mitatu. Pia huuzwa katika maduka ya nafaka, kilo ikiwa kati ya Sh300 – 400.

Samuel Kamau ni mkulima wa kansara Kasarani, Kaunti ya Nairobi, na anasema ekari moja inahitaji mbegu kilo mbili.

Mwanazaraa huyu ana uzoefu wa kilimo cha mboga za kienyeji kwa zaidi ya miaka 15.

Kulingana naye, kansara ni miongoni mwa mazao rahisi mno kuzalisha. “Hazina utaratibu wowote katika upanzi. Si kama sukumawiki au spinachi, ambazo zina mpangilio maalum wa mashimo,” asema Bw Kamau.

Anaiambia Akilimali kuwa shamba huandaliwa kwa kuinua udongo uunde mfano wa kitanda, kuufanya kuwa mwororo na kuutandaza. Mbegu humwagwa tambarare halafu maji yanamwagiliwa.

“Anachohitaji mkulima ni mbolea pekee, ya mifugo au kuku,” ahimiza mwanazaraa huyu.

Kwa kawaida, mbegu huchipuka ardhini baina ya siku tano hadi saba, baada ya upanzi.

Mkulima Kamau anasisitizia haja ya kunyunyizia maji, ingawa kwa kipimo.

Anaendelea kueleza kwamba mboga hizo zinaweza kunawirishwa kwa mbolea ya kisasa – fatalaiza, wataalamu wakihimiza iliyosheheni Nitrojini.

“Inapotiwa, zinyunyiziwe maji ili kustawisha matawi na majani,” ashauri mtaalamu Veronica Kirogo.

Kansara huwa tayari kwa mavuno baada ya siku 25 na 30, sawa na mwezi mmoja. Kulingana na Samuel Kamau, huvunwa kwa kung’oa, kilo moja ikiuzwa zaidi ya Sh25. Aidha, ekari moja iliyotunzwa vyema ina uwezo kuzalisha zaidi ya kilo 3, 000