‘Kilimo cha miwa Mlima Kenya kina uwezo wa kuvuna Sh20 bilioni kwa mwaka’

‘Kilimo cha miwa Mlima Kenya kina uwezo wa kuvuna Sh20 bilioni kwa mwaka’

Na MWANGI MUIRURI

WAKULIMA wa miwa katika ukanda wa Mlima Kenya sasa wanaitaka serikali iwajumuishe katika sera maalum za kitaifa kuhusu sekta ya sukari wakisema kwamba kwa sasa wanavuna Sh3.5 bilioni kwa mwaka.

Wanasema ikiwa serikali itaweka wakulima wa miwa katika ukanda huo katika sera ya kuwapa mbolea, mikopo na mbegu za kisasa wako na uwezo wa kuzidisha pato hilo hadi Sh7 bilioni kwa mwaka na kuwaajiri wengi wa vijana wa eneo hilo.

“Hasa ikiwa serikali itatuunga mkono kwa kutupa uwezo wa kuzindua viwanda vidogovidogo vya uongezaji ubora zao la miwa, basi pato letu litazidi hadi Sh20 bilioni kwa mwaka,” akasema Katibu mkuu wa wakuzaji miwa ukanda huo Bw David Mwangi.

Bw Mwangi aliambia Taifa Leo kuwa takwimu zake ni za kati ya mwaka wa 2017 na 2020 ambapo muungano wake ulikuwa na wakulima 8,850 wa zao la miwa usajili ukiwa katika Kaunti za Kirinyaga, Murang’a, Nyeri, Kiambu na Embu na ambapo hata kando na kuwa na wakulima wa kibinafsi, kunao ambao wanatekeleza uzalishaji huo wakiwa katika makundi ya vijana na kina mama.

Bw Mwangi alisema kuwa katika soko kila mua wa Sh20 uko na uwezo wa kumpa mchuuzi Sh40 hivyo basi kuwa na faida ya kuvutia wengi kusaka riziki ndani ya kilimo hiki.

“Ile dhana kwamba miwa hukuzwa tu katika maeneo ya Magharibi mwa nchi haijawezesha wengi kung’amua kwamba hapa Mlima Kenya tuko na uwezo wa kuvuna vinono vya sekta hii,” akasema.

Maeneo hasa yaliyoorodheshwa nchini kama ngome za uzalishaji miwa ni Muhoroni, Homa Bay, Chemelil, Miwani na SoNy, Mumias, Nzoia, Tana River na Busia. Mua hukomaa katika kipindi cha kati ya miezi sita na 24 kulingana na ubora wa miche; ujio wa Sayansi ya uzalishaji ukipunguza muda wa ukomavu hata hadi kwa miezi mitatu pekee.

Hekari moja ikiwa chini ya upanzi wa miwa iliyotunzwa vyema inaweza kutoa mavuno ya kati ya tani 45 na 53.

Bw Mwangi anasema kuwa kuafikia ndoto yao ya kuzidisha pato kutahitaji serikali iwape uwezo wa kuzindua viwanda vya kutumia miwa kama malighafi ya kutengeneza bidhaa kama juisi, mvinyo na sukari ya matumizi nyumbani.

Anasema serikali za Kaunti kwa ushirikiano na idara ya ustawishaji viwanda katika serikali kuu ndizo ziko na wajibu wa kuwafaa kwa hili.

“Kiwanda kimoja kitahitaji bajeti ya Sh10 milioni lakini kikishaanza kutekelezewa kazi ya uongezaji ubora, kila kiwanda kinaweza kikaunda faida ya Sh3 milioni kwa mwaka huku kikiajiri vijana 50 na kuwapa wakulima wa miwa soko la moja kwa moja hivyo basi kuwavutia wengi kujiingiza katika riziki ya kuongeza utajiri mashinani.

Bw Joseph Mwaura amekuwa katika biashara ya kuuza miwa katika mji wa Maragua Kaunti ya Murang’a kwa miaka 23 sasa na anasema ni biashara ambayo imemwezesha kusomesha watoto wake na kuwapa lishe ya kila siku.

“Kwa siku moja ya kawaida sasa ninaweza nikajipa faida ya Sh1, 200 kumaanisha kwa mwezi niko na uwezo wa kuunda Sh36, 000 kwa mwezi. Katika miaka ya 1990’s, faida kwa siku ilikuwa ya Sh300 kwa siku ikijumulisha Sh9, 000 kwa mwezi na kwa kuwa gharama ya maisha haikuwa imepanda kwa viwango vya sasa, ni pesa ambazo zilinifaa pakubwa kiasi hata cha kununua shamba ekari tatu,” asema.

Ambrose Kisinga ambaye huuza miwa katika steji ya Ruiru Kimbo na ambaye wateja wake wa dhati ni wanafunzi wa taasisi ya kozi za biashara na Kiufundi ya Nairobi (NIBS-TC) anasema kuwa katika miaka ya 1990’s alikuwa akinunuwa miwa kutoka masoko ya Jiji la Nairobi “lakini kwa sasa nimegundua kuwa ninaweza nikapata bidhaa hii kutoka Kaunti kadha za Mlima Kenya.”

Anasema kuwa uzuri wa uteja wake Mlima Kenya ni kuwa “miwa hukuzwa katika mashamba na maji ya mvua au ya unyunyiziaji kinyume na hali zingine za Jiji la Nairobi na mingineyo ambapo miwa hukuzwa kwa kutumia maji taka na kuishia kuwa na kemikali hatari kwa binadamu na pia kuwa na ladha ya chumvi.”

Anasema kuwa akishanunua kutoka kwa wakulima shambani huwa hapati shida ya uchukuzi “kwa kuwa eneo hilo liko na magari mengi ya huduma za uchukuzi wa bidhaa kwa bei nafuu.”

Kwa mujibu wa mtaalamu wa tiba kwa kutumia mimea asili Bw Vincent Ole Yiapan kutoka Mji wa Narok, miwa hujipa soko lake kwa urahisi kwa kuwa huhusishwa na uwezo wa kimatibabu.

“Kwa mfano, juisi ya au mvinyo wa miwa huwa na uwezo wa kuongeza nguvu za kiume na pia nguvu za kijumla kwa mwili wa binadamu. Pia, huwa na uwezo wa kukabiliana na maradhi ya njia ya mkojo na pia husafisha figo,” akaambia Taifa Leo.

Utafunaji miwa pia ni njia mbadala ya kuosha mdomo na kuuondolea harufu mbovu, huhusishwa na kusaidia maini ya binadamu kuhepa maradhi kadhaa yanayotokana na bakteria, husaidia macho kuhepa ugonjwa wa Jaundice na hutambulika na kuwa na madini ya protini ambayo husaidia uponyaji wa vidonda.

Uwezo mwingine wa miwa ni kusaidia ngozi kunyooka, mifupa kubakia imara na katika uongezaji ubora ili kuunda bidhaa za kimatibau hidadisiwa kuwa pato kwa juisi ya lita moja hupanda kwa zaidi ya asilimia 300.

“Hii ina maana kuwa ule muwa wa kuuzwa Sh20 unaweza kuafikia bei ya Sh60 katika uongezaji ubora. Ina maana kuwa muwa mmoja ukiongezwa ubora unaweza ukaajiri vijana wengine wawili na kwa ujumla yale mavuno yetu ya miwa 19775 yako na uwezo wa kuajiri vijana 59, 325,” asema Bw Mwangi.

Mzee Joseph Mwangi akibandua maganda kutoka kwa mua katika mji wa Maragua. Picha/ Mwangi Muiruri

Mtaalamu wa kilimo cha kisasa katika Kaunti ya Murang’a Bw James Thuo anasema kuwa utunzaji wa mimea ya miwa huhitaji njia asili za kupambana na magonjwa na wadudu “na ni katika zile hali za kipekee ambapo utumizi wa kemikali unaweza ukazingatiwa.”

Jivu ni mojawapo ya ‘dawa’ ya kupambana na maradhi na wadudu katika kilimo cha miwa.

Anaorodhesha wadudu ambao huvamia miwa kama Early shoot, na Internode borer, mchwa na nzi weupe ambao huvamia ili kufyonza sukari huku magonjwa katika kiilimo hiki yakiwa ni Red rot, Smut na Ratoon stunting ambayo kikemikali hukabiliwa kwa kutumia dawa ambayo sio ya gharama kubwa.

You can share this post!

Mikakati ya kupanua ushiriki wa gozi la UEFA kutoka timu 32...

Madereva wa tuktuk Githurai waonyesha umoja kuboresha kazi...