Habari

Kilimo cha pamba chaendelea kusambaratika Lamu

January 27th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya wakulima 10,000 wa pamba, Kaunti ya Lamu wanahofia kusambaratika kwa kilimo hicho ambacho kimekuwa kikididimia kila kuchao katika siku za hivi karibuni.

Tangu jadi, kilimo cha pamba kaunti ya Lamu kimekuwa kikiendelezwa kwa wingi kwenye maeneo ya Baharini, Tewe, Uziwa, Hongwe, Nairobi Area, Mpeketoni na kwenye maeneo ya Witu, Hindi na Faza.

Katika mazungumzo na wanahabari wakati wa kongamano la kujadili muelekeo wa kilimo cha pamba Lamu, msemaji wa wakulima wa pamba eneo hilo, Joseph Migwi alisema kilimo cha pamba kwa sasa kimedidimia kwa hadi asilimia 30.

Alisema kati ya wakulima zaidi ya 10,000 ambao wamekuwa wakiendeleza kilimo hicho Lamu, ni wakulima takriban 6000 pekee ambao bado wameshikilia kilimo cha pamba.

Alisema wengi wao wamekuwa wakitekeleza kilimo cha kadri ambacho hakiwezi kukimu kiwango cha kibiashara.

Alitaja wadudu ambao wamekuwa wakihangaisha wakulima kwa kuharibu mmea huo mashambani na ukosefu wa kiwanda cha pamba eneo la Lamu kuwa sababu kuu zinazochangia kufifia kwa kilimo hicho.

Aliitaka serikali na wadau kujitokeza kusaidia kuboresha miundomsingi ya kilimo cha pamba ili sekta hiyo iweze kupanuliwa siku za usoni.

“Tuna hofu kubwa kwamba hali ikiendelea hivi, huenda kilimo cha pamba kikawa ndoto na tayari wengi tayari wamekufa moyo na kujitoa kwenye kilimo hicho. Kati ya wakulima 10,000 tuko na wakulima 6000 pekee ambao bado wanang’ang’ana kuendeleza ukuzaji pamba japo kwa kiwango kidogo. Ipo haja ya kiwanda cha pamba kubuniwa eneo hili ili kusaidia wakulima wetu hapa,” akasema Bw Migwi.

Bw Johnson Kamau ambaye tangu zamani ametambulika kwa kilimo cha pamba eneo la Mpeketoni, alisema ameshindwa kuendeleleza kilimo hicho na badala yake kuibukia kilimmo cha tikitimaji na mahindi.

Alisema ukosefu wa soko maalum la kuuza pamba na pia miundomsingi duni katika usimamizi wa kilimo cha pamba Lamu ni miongoni mwa sababu zilizomsukuma kupiga teke kilimo cha pamba.

“Nilinga’ng’ana lakini mwishowe nilishindwa kabisa kuendeleza kilimo cha pamba. Kila msimu unakadiria hasara. Niliona ni vyema nibadilishe kilimo cha mimea mingine ya kibiashara, ikiwemo tikitimaji na mahindi ambayo soko lao kidogo liko wazi. Serikali itafutie wakulima wa pamba soko maalum ili wawe na uhakika wa kununuliwa pamba yao kwa bei nzuri kila wanapokuza,” akasema Bw Kamau.

Bw Kimani Wanyoike pia aliitaka kaunti na wadau kutafuta mbegu ya kisasa ya pamba itakayoweza kustahimili hali ya anga na changamoto za wadudu Lamu.