Habari Mseto

Kilimo cha pamba kuimarisha maisha ya wakulima Machakos

February 27th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wa zao la pamba eneo la Ndalani, Yatta, Kaunti ya Machakos, watanufaika na msaada wa dawa za kunyunyizia zao hilo kutoka kwa kampuni ya Thika Cloth Mills (TCM).

Zaidi ya wakulima 300 wanaokuza mipamba ili kuvuna pamba kutoka maeneo ya Kivingoni, Ndalani, Kisuki, na Kwandoto, watapata afueni msimu huu kwa sababu wanatarajia kuvuna pamba kwa wingi kabla ya Aprili 2020.

Jambo linalo wapa matumaini ni kutokana na kampuni ya Thika Cloth Mills kuwasaidia na dawa ya kunyunyiza katika zao hilo la pamba.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bi Tejal Dodhia, alisema wakulima wengi watapata faida kubwa kwa sababu kampuni hiyo itanunua pamba kutoka kwao kwa bei ya Sh52 kwa kilo moja kutoka kwa Sh25 ya hapo awali.

“Sisi tunataka kuinua wakulima hao ili wapate mapato mema ya kujitosheleza kwa kuwahimiza wapalilie na kupanda pamba kwa wingi ili nasi tuweze kununua zao hilo kwa kiwango kikubwa,” alisema Bi Dodhia alipozuru eneo hilo mnamo Jumanne.

Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakinunua pamba kwa wingi kutoka Tanzania na Uganda, kwa bei ya juu lakini kwa sasa watapata afueni kununua zao hilo kwa wingi kutoka kwa wakulima wa hapa nchini.

Bi Dodhia alisema tayari serikali imewapa kandarasi ya kuunda mavazi ya wan jeshi huku akisema imewapa nguvu kama kampuni kupiga hatua zaidi kibiashara.

Alisema mwezi Novemba 2019, walizuru kaunti za Homa Bay na Siaya ambapo waliwahimiza wakazi wa huko kuingilia kilimo cha pamba ili baada ya miezi kadha watapata mavuno kwa wingi na kampuni ya Thika Cloth Mills itakuwa tayari kununua zao hilo kutoka kwao kwa bei nzuri.

Alitaka Kaunti ya Machakos kuwahimiza wakazi wa huko waingilie upanzi wa pamba ili waweze kunufaika siku zijazo baada ya mavuno.

Bw Francis Kilango kutoka eneo la Kivingoni, amepanda mipamba katika ekari sita za kipande cha ardhi na anatarajia kupata mavuno mazuri kwa miezi michache ijayo.

“Tunatarajia wakulima wachache waliozamia kupanda zao hilo watapiga teke umaskini kwa sababu kampuni hiyo iko tayari kununua zao lote linalotoka shambani,” alisema Bw Kilango.

Alisema wazazi wake walipanda pamba miaka za hapo awali lakini kutokana na malipo duni kwenye soko, walilazimika kuachana na ukuzaji wake.

Bi Pauline Muasya na John Ndolo wakazi wa Ndalani wameipongeza serikali kwa kuhimiza wananchi kuingilia upanzi wa pamba kwa sababu inalipa faida ya kuridhisha.

“Tunataka kaunti ya machakos kuingilia kati na kusaidia wakulima na vifaa muhimu vitakavyowapa mwelekeo mwafaka wa kujiende;leza,” alisema bw John Ndolo.