Kilimo champa ajira na kumlipia karo ya chuoni

Kilimo champa ajira na kumlipia karo ya chuoni

Na WINNIE ONYANDO

Akiwa katika ziara yake ya kila siku ya kukagua shamba lake la robo ekari, Rueben Onyang’o, 22, anaonekana akitabasamu kutokana na mazao kubwa ya sukuma wiki, nyanya na matikitimaji shambani mwake, kijiji cha Uyawi, Kaunti ya Siaya.

Alipotembelewa na Akilimali, mkulima huyo mashuhuri katika eneo hilo ana sifa si haba kutokana na ujuzi wake wa kutumia njia za kisasa katika ukulima.Onyang’o ambaye yuko katika mwaka wake wa pili katika Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga anakosomea kozi ya Linux katika uhandisi wa kompyuta, anaeleza kuwa alipenda ukulima tangu akiwa mdogo.

Baada ya kumaliza Kidato cha Nne, Onyang’o anaeleza kuwa alikosa msaada wa karo ya kujiunga na Chuo Kikuu, hali iliyomsukuma kuanza ukulima.Maarifa katika ukulima aliyopata kutoka kwa hayati baba yake miaka mingi iliyopita yalimpa ujasiri wa kuanza ukulima katika shamba lao lililo kwenye ufuko wa Ziwa Victoria.

“Nilitafuta njia ya kupata aghalau karo ya kujiunga na Chuo Kikuu. Baada ya kukosa msaada kutoka kwa marafiki, niliamua kujitosa kabisa katika ukulima. Tayari nilikuwa na ujuzi katika sekta hiyo na hivyo nikaanza kazi mara moja,” asimulia Onyang’o.

Katika shamba hilo, kijana huyo amepanda sukumawiki, mboga za kienyeji, matikitimaji na nyanya.Anasema kuwa bidii yake na kutobagua kazi imemwezesha kuendelea na masomo yake.Katika eneo hilo lililozingirwa na Ziwa Victoria, wakazi wana mazoea ya kula samaki kama chakula chao kikuu ila kijana huyo anahakikisha kuwa wanapata mboga misimu yote.

Anaeleza kuwa baadhi ya wakulima hawatumii dawa za kisasa kulinda mimea yao shambani jambo linalowafanya kuchukia ukulima hasa baada ya kupata hasara kutokana na mazao mabovu.Anahusisha mapato duni na ukosefu wa maarifa na kutotumia dawa za kisasa kama vile mbolea aina ya Haifa MPK, Calcium Amonium Nitrate (CAN) na dawa ya kuboresha ukuaji kama vile Vegimax, matumizi ya Topaz na Co-power.

Akielezea umuhimu wa mbolea ya Haifa MPK, Onyang’o anasema kuwa tangu agundue mbolea hiyo, hajawahi kujuta wala kupata mazao madogo.Mbolea hiyo ina uwezo wa kuyeyuka kabisa kwenye maji, tofauti na aina nyingine za mbolea zinazotumika na baadhi ya wakulima.

Kadhalika, Haifa MPK ina asilimia 100 ya virutubisho vinavyohitajika na mimea ili kukua haraka na kuwa thabiti.Kwa upande mwingine, Vegimax imejaa nitrogeni kati ya asilimia 65 na 75, Fosforasi ya Kikaboni kati ya asilimia 20 na 25 na Potasiamu ya Kikaboni ya kati ya asilimia 3 na 5, madini, vitamini na asidi ya amino zinazohitajika na mimea.

Hii inaifanya kuwa bora kimatumizi hasa baada ya kuchanganywa na maji. Inaweza kunyunyizwa moja kwa moja kwenye mimea inayokua na miche.“Nafahamu kuwa tegemeo langu ni mapato kutoka shambani.

Kwa hivyo lazima niwekeze pesa na bidii yangu shambani ndipo niweze kupata mazao bora,” akasema Onyang’o.Katika shamba lake, Onyang’o anatumia takriban Sh50,000 katika maandalizi ya shamba, kabla ya kuanza kupanda.

Kila mwaka, Onyang’o anavuna mara tatu kutoka shambani mwake.Hata hivyo, anaweza kuvuna sukumawiki zaidi ya miezi saba kutokana na matunzo yake.Sukumawiki humpa Sh10,000 kwa wiki, nyanya humpa faida ya Sh100,000 huku tikiti maji kumpa Sh40,000 katika kila kipindi cha mavuno.

Soko lake ni Nang’o, ufuko wa Ziwa Victoria inayojumuisha eneo la Oyamo, Ndeda na Uyawi.ChangamotoKinachomtia wasiwasi sana mkulima huyo ni ukosefu wa usalama. Anaeleza kuwa baadhi ya wakazi wanalivamia shamba lake usiku wa manane na kuiba mazao yake.

Shamba lake linapatikana katika ufuko wa Ziwa Victoria hivyo basi wanyama kama vile viboko hulivamia shamba lake na kula mimea yake.“Kwa kuwa siwezi kushindana na viboko, mimi huwawekea mitego ili kuwanasa,” akasema Onyang’o.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa soko la nje. Onyang’o anaeleza kuwa anategemea soko la mitaa kuuza mazao yake.Hata hivyo, mkulima huyo anawahimiza wakulima wenzake kuwekeza pesa zaidi katika utunzaji wa mimea ndipo waweze kuchuma hela.

You can share this post!

KINYUA BIN KINGORI: Rais ni kiongozi wa Wakenya wote si...

Ananyoa kwa shoka na wateja wamejaa kibao

T L