Makala

KILIMO: Maharagwe aina ya 'minji'

August 13th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

WATAALAMU wa lishe huhimiza watu kula vyakula vya kiasili kama viazi vikuu, mihogo na viazi vitamu.

Pia wataalamu wanashauri haja ya wakulima kuzingatia mfumo wa kilimohai, mazao yaliyozalishwa bila kemikali ya dawa dhidi ya magonjwa na wadudu na hata kutotumia fatalaiza.

Mfumo huo unatilia mkazo ukuzaji wa mimea kwa kutumia mbolea mifugo na kuku.

Kulingana na madaktari na wataalamu wa masuala ya afya, watu wakiitikia kula chakula asilia au kienyeji na ambacho mazao yake yamekuzwa kupitia kilimohai, visa vya magonjwa hatari kama vile Saratani vitadhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Juliet Mwanga, mtaalamu, anasema aina ya lishe ni mojawapo ya vigezo muhimu kuzingatia katika orodha ya chakula. “Mazao yaliyokuzwa kwa kemikali ni wazi si salama kwa binadamu.

“Huenda magonjwa ibuka yakakosa kuonekana punde tu baada ya kula chakula cha mazao hayo, lakini muda mrefu baadaye yatachipuka,” Juliet aeleza.

Mbali na viazi asilia, mboga za kienyeji kama vile mnavu, mchicha, kunde, mito, saga na murenda, ni miongoni mwa chakula unachohimizwa kukijumuisha katika ratiba yako ya lishe.

Si wakulima wengi wanaokuza maharagwe aina ya minji, kwa Kiingereza ‘garden peas’. Aidha, maharagwe haya yanaorodheshwa miongoni mazao asili.

Kulingana na David Kariuki, afisa na mtaalamu wa kilimo katika kaunti ya Kirinyaga, minji ni zao rahisi mno kukuza.

Isitoshe, mdau huyu anasema si lazima mkulima awe na mamia au maelfu ya ekari kuyazalisha. “Ukuzaji wa minji hauna mwalimu, manufaa yake kwenye udongo na afya ni tele,” asema Bw Kariuki.

Katika shamba la Timothy Mburu, lenye ukubwa wa ekari nne, mkulima huyu hakosi kuwa na mazao kila baada ya miezi miwili.

Tunampata Bw Mburu akiwa kwenye kipande chenye kipimo cha thumni ekari (1/8), akikagua yanavyoendelea maharagwe haya.

Mwanazaraa huyu anasema sehemu hiyo inahitaji kilo mbili za mbegu, ambapo kilo moja inagharimu Sh100. Upanzi wake ni kwa njia ya mitaro au mashimo.

“Upanzi wake ni sentimita 25 kwa 25 mraba, yaani; nafasi kutoka mmea mmoja hadi mwingine iwe sentimita 25 na nafasi kati ya mstari wa laini ya mashimo au mitaro iwe na kipimo sawa na hicho,” anafafanua Bw Mburu.

La kutia moyo ni kuwa mbegu zake hupandwa moja kwa moja, sawa na yapandavyo maharagwe na hayahitaji mbolea yoyote ile.

“Yasitiwe mbolea kwa sababu unachoyapa tayari yanayo kwa wingi,” anasisitiza.

Minji inaorodheshwa katika mimea ya Legumi (legumes), na imesheheni Nitrojini; madini muhimu katika mbolea na kilimo.

“Maharagwe haya huongeza rutuba na Nitrojini kwenye udongo. Hayahitaji mbolea yoyote ile kuyapanda, kwa sababu unachotaka kuyapa yanacho,” asema Bw Mburu ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kilimo.

Mbegu huchipuka baada ya siku nne au tano. Wiki ya tatu, hupuliziwa dawa dhidi ya wadudu, hususan wanaposhambuliwa. Wadudu wanaoshuhudiwa ni vidukari na viwavi. Ni nadra minji kuathiriwa na magonjwa.

 

Mkulima Timothy Mburu akiwa katika shamba la garden peas; maharagwe ambayo wengi nchini Kenya huyaita ‘minji’. Picha/ Sammy Waweru

Mburu anaeleza mkulima anapaswa kupalilia kuondoa makwekwe mara moja pekee. Shamba likiwa safi haimlazimu mkulima kupalilia.

“Makwekwe kiasi husaidia minji kusimama kwa kuwa ni mimea inayotambaa ikielekea juu,” anasema, akiongeza kuwa mkulima anaweza kuisimamisha kwa vijiti vyenye urefu karibu mita tano.

Maji ni kiungo muhimu katika kilimo cha minji, na Bw Mburu huinyunyizia kwa mifereji.

“Maharagwe haya yana mapato ya haraka. Miezi miwili baada ya upanzi, huanza kuvunwa,” aeleza. Thumni ekari ina uwezo kuzalisha zaidi ya kilo 600. Kilo moja ya minji inagharimu Sh100.

Mkulima huyu hukuza viazimbatata na kabichi kwa wingi. Pia, huzalisha vitunguu saumu. Mkulima huyu wa kipekee ameweza kufanikisha shughuli za kilimo kwa ajili ya kuwa na bwawa, linaloteka maji hasa msimu wa mvua.

Viazi na kabichi ni mazao yanayohitaji udongo wenye rutuba na Nitrojini ya kutosha.

Kulingana na mtaalamu David Kariuki, wakulima wengi huchosha udongo kwa kuutia fatalaiza ilhali ukuzaji wa minji ni mbinu murwa kudumisha rutuba.

“Wakumbatie kupanda minji eneo wanalovuna mazao kama viazi, nyanya, vitunguu, mboga na matunda, ili kuongeza rutuba kwenye udongo. Nitrojini ni miongoni mwa madini yanayoongeza rutuba udongoni, na maharagwe haya yamesheheni madini haya,” anafafanua Bw Kariuki.

Pia anahimiza umuhimu wa kuzingatia mfumo wa kilimohai; uzalishaji wa mimea kwa kutumia mbolea ya mifugo.

Mbali na maharagwe haya asilia, maharagwe mengine hasa yanayotumika kuandaa kande (githeri) pia huongeza Nitrojini na kudumisha rutuba ya udongo.

Njia nyingine ni kuruhusu makwekwe yamee shambani.