Makala

KILIMO: Mboleahai inayoimarisha mazao na rutuba udongoni

October 8th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

KATIKA kijiji cha Karanga kilichoko Kinangop Kusini, Kaunti ya Nyandarua, Bw Nicholas Ngata hufanya shughuli mbalimbali za kilimo.

Kaunti ya Nyandarua ni tajika katika uzalishaji wa viazi, na anajishughulisha na ukuzaji wa viazimbatata na maharagwe asilia aina ya minji lakini kitaalamu zaidi yanafahamika kwa jina garden peas.

Isitoshe, mkulima huyu ni mtafiti wa pembejeo; hasa mbolea na ameibuka na mboleahai isiyo na kemikali. Ni ya majimaji na mwenyewe anapenda kuiita Agriculo Organic Food.

Huitengeneza kutokana na malighafi yatokayo shambani na mifugo.

Katika simulizi yake ipatayo miaka sita iliyopita, alifanya uchunguzi katika maeneo mbalimbali nchini, hususan yanayofanya kilimo ili kujua mbolea wanayotumia kuzalisha mazao na matokeo yake kwa walaji.

Dhamira ilikuwa kubaini ikiwa mimea, kuanzia nafaka, mboga na matunda inaweza kukuzwa bila kutumia fatalaiza na dawa zenye kemikali.

Aidha, shinikizo hilo hasa lilitokana na kujaribu kutafuta suluhu ya ongezeko la visa vya ugonjwa hatari wa Saratani.

Alirejea darasani, ambapo alijiunga na mpango wa masomo ya Sayansi ya udongo na kuimarisha rutuba. Bw Ngata anasema alifanya utafiti wa matumizi ya zaidi ya aina 50 ya mimea, miti na mizizi.

Shabaha ikawa iwapo anaweza kuibuka na mboleahai; isiyo na kemikali, lakini inayoweza pia ikatrumika kama dawa dhidi ya wadudu wanaoshambulia mimea na magonjwa mbalimbali ya mimea.

“Nilichanganya mimea, mizizi ya miti na malighafi hai yatokayo kwa wanyama. Mchanganyiko huo nikaufanyia jaribio katika udongo wa mashamba ya wakulima kadhaa na mimea yao, bila kutoza ada yoyote,” aeleza Ngata.

Hata ingawa safari ya utafiti huo haikuwa rahisi kwa sababu ya ukosefu wa fedha za kutosha kuufanikisha, aliibuka na mboleahai mpya ya maji aliyoipa jina la kipekee “Agriculo Organic Food”. Agri ina maana ya kilimo na Culo ni jina lenye asili ya Kiitaliano lenye maana ya mmea.

Malighafi anayotumia kuitengeneza ni mimea, mizizi ya miti, mkojo wa sungura, na mengineyo. Anasema kuwa Agriculo inasaidia katika uongezaji wa mazao na rutuba udongoni.

Hali kadhalika, husaidia kuzuia mimea na mazao kushambuliwa na wadudu. Pia anasema hustawisha afya ya mimea na kuifanya kuwa imara dhidi ya magonjwa ibuka.

Anasema mbolea hiyo ya maji ni sahibu ya udongo na inayoutunza. Kulingana na mkulima, udongo uchanganywe sawasawa na mbolea ya mifugo kabla ya upanzi. Kwenye mimea, anashauri kunyunyizia Agriculo kila wiki ili kupata mazao bora na ya kuridhisha.

Ekari moja inahitaji lita 30 za mbolea hiyo.

“Bei ninayouza ni nafuu ikilinganishwa na mbolea zingine aina ya mboleahai na hata fatalaiza. Lita moja inagharimu Sh500. Kipimo kiwe mililita 400 kwa mtungi wa lita 20 za maji,” Bw Ngata afafanua.

Anasema utafiti aliofanya umebaini aina hiyo yake ya mbolea inafanya vyema kuliko zingine, bila madhara yoyote yale kwa mkulima na mlaji wa mazao.

Mkulima na mtafiti Nicholas Ngata aonyesha viazi vilivyokuzwa na kisha mboleahai ya majimaji aliyovumbua; Agriculo Organic Food ikatumika. Picha/ Sammy Waweru

Aidha, utafiti huo uliegemea miti na mizizi iliyosheheni Vitamini, asidihai na madini kama Nitrogen, Potassium, Zinc, Iron, Manganese na Copper.

“Nilidhamiria kujua manufaa ya madini hayo kwenye udongo na mimea na ndiyo Agriculo imesheheni,” asema.

Wakati wa mahojiano alisema awali nusu ekari ilimzalishia chini ya magunia 20 ya viazi lakini baada ya kuvumbua Agriculo kwa sasa anapata hata zaidi ya magunia 60.

David Kamau, mkulima wa mahindi anasema baada ya kuanza kutumia mbolea hiyo ameshuhudia mabadiliko makubwa katika mazao.

“Kitambo ekari moja ilinizalishia chini ya magunia 15 ya mahindi, lakini baada ya kutumia Agriculo ninavuna karibu 50,” asema Bw Kamau.

Matumizi ya fatalaiza na dawa zenye kemikali yananyooshewa kidole cha lawama kwa kukithiri kwa maradhi kama vile Saratani.

Mbali na kuwa hatari kwa walaji wa mazao, ni kero ambalo huacha udongo ukiwa katika hali mahututi, kudhoofisha rutuba.

Afisa na mtaalamu wa kilimo David Kariuki anaonya kuwa wakulima wasiporejelea mfumo asilia kuzalisha mazao, uafikiaji wa kilimohai utakuwa ni kama ndoto ya mchana isiyotimia ng’o!.

“Fatalaiza zenye kemikali zinadhoofisha rutuba na kuongeza asidi ambayo ni hatari kwa mimea na wanyama muhimu udongoni. Athari hiyo inaambatana na matumizi ya dawa zenye kemikali,” atahadharisha afisa huyo.

Mbali na mimea, uvumbuzi wa Nicholas Ngata pia umejumuisha mifugo na ndege hususan wanaofugwa nyumbani. Anasema ameibuka na Agriculo Organic Food inayotumika kukabili vimelea kama vile minyoo, kupe, viroboto, nzi na maradhi mbalimbali ya mifugo na ndege. Anaeleza kwamba inasaidia kuongeza mazao ya nyama, mayai na hata maziwa,” asema.

Amewasilisha chembechembe za mbolea na dawa anazounda kwa taasisi ya Utafiti wa Ubora wa Mimea, Kephis, ili zitathminiwe na kupewa kibali.

Hakuna safari isiyokosa milima na mabonde, jitihada zake zinakwamishwa na ukosefu wa fedha na ushirikiano wa mashirika ya kilimo na ufugaji, akidokeza kwamba amepata oda tele kutoka mataifa ya kigeni.