Makala

KILIMO NA BIASHARA: Mradi eneo kame umewapa wakazi riziki

May 9th, 2019 3 min read

Na SAMUEL BAYA

KATIKA maeneo kame, kuendeleza kilimo-biashara huwa ni changamoto kubwa.

Kuna sababu kadhaa ambazo huwa chanzo cha hayo, mojawapo ikiwa ni uhaba wa mvua na idadi ndogo ya vyanzo vya maji ambavyo vinaweza kuhimili ukame wa muda mrefu.

Katika eneo la Bamba, Kaunti ya Kilifi kuna mradi wa kilimo ambao unaendelezwa katika eneo kame la Chapungu, na umeonyesha ustawi mkubwa.

Mradi huo wa unyunyizaji maji mashamba unaopatikana katika kijiji cha Gwaseni unatarajiwa kubadilisha taaswira hiyo ya ukame.

Kuna mboga na mimea mbalimbali ambayo inapandwa katika shamba hilo la ukubwa wa ekari 18.

Bwawa dogo ambalo lilijengwa na mfadhili kusaidia wakazi kuhifadhi maji ya mvua ndilo ambalo linatumiwa na wakazi kunyunyizia mashamba maji.

Mwenyekiti wa mradi huo wa Gwaseni/Bumbi irrigation project Bw Robert Mkutano aliambia Akilimali kwamba wamekuwa wakipanda mboga mbalimbali ikiwemo sukuma wiki na biringani ambazo baadaye huuzwa katika soko la Bamba.

Mkulima Bw Robert Mkutano (kulia) kutoka kwenye mradi wa unyunyziaji maji mashamba wa Gwaseni/Bumbi akimuonyesha mwakilishi wa Wadi ya Bamba Bw Christopher Mwambire (kushoto) na mbunge wa Ganze Bw Teddy Mwambire (wa pili kushoto) wakati walipotembelea mradi huo wa kilimo unaopatikana katika barabara ya Mariakani-Bamba. Mradi huo umekuwa ukiwasiaida sana wakulima katika eneo hilo kame la kaunti ya Kilifi. Picha/ Samuel Baya

“Kwa muda wa miaka mitatu sasa, tumekuwa tukipanda mboga, migomba pamoja na miwa. Bidhaa hizi zote zina soko katika kituo cha kibiashara cha Bamba ambacho kinapatikana kilomita 10 kutoka hapa,” akasema Bw Mkutano.

Ekari 18, ambapo mradi huo unatekelezwa, zilitolewa na jamii ya eneo hilo baada ya kupata ari ya kuendeleza kilimo.

“Tunatekeleza mradi huu katika mto wa muda ambao unajulikana kama Gwaseni, ambao unapitia hapa na kuunganisha kijiji cha Nzovuni. Wazee wa hapa waliamua kutupatia shamba hili tulime na tunashukuru,” akasema.

Bw Mkutano alisema kuwa hata baada ya mfadhili kuchimba bwawa hilo, walikumbana na shida baada ya mto wakati mmoja kufurika na kuliharibu bwawa hilo.

“Bwawa hili liliharibika na kwa sasa, halina uwezo wa kuhifadhi maji mengi. Tunaomba wahisani wajitokeze ili kuliziba,” akasema Bw Mkutano.

Mradi huo unasimamiwa na vikundi vitatu vya wakulima vyenye jumla ya wanachama 250.

“Hapa tuna vikundi vitatu vya wakulima, mojawapo ikiwa ni kikundi cha Gwaseni Mazingira. Kikundi cha Gwaseni kinahusika na ukulima wa mboga na upanzi wa mimea hali kikundi cha FAO kikihusika na kilimo-biashara,” akasema Bw Mkutano.

Mmoja wa wakulima Bw James Kahindi alisema kuwa kwa sasa anauza mboga zake katika soko lililoko katika kituo cha biashara cha Bamba.

“Nimekuwa nikipanda ndizi na miwa na huwa ninauza katika soko la Bamba. Wakati nikiwa na siku nzuri, huwa ninauza mboga zenye kiasi cha Sh1, 000. Pesa hizi zinanisaidia kuimarisha maisha yangu pamoja na familia yangu,” akasema Bw Kahindi.

Kisha Bw Mkutano alisema kuwa bado wanapitia changamoto kadhaa ambazo ni ukosefu wa vifaa vya kisasa vya unyuynizaji mashamba maji pamoja na uhaba wa maafisa wa nyanjani ambao wanafaa kuwapatia ushauri kuhusu kilimo bora.

“Tunashukuru uwepo wa mradi huu lakini hatuna vifaa vya kutumia kuboresha shughuli zetu hapa kama wakulima,” akasema Bw Mkutano.

Mwakilishi wa Wadi ya Bamba Bw Christopher Mwambire alisema katika mahojiano kwamba mradi huo umeleta matumaini mengi kwa wakazi na wakulima wa sehemu hiyo.

Alisema kuwa kupitia kwa shirika la kilimo ulimwenguni (FAO) wamefaulu kuwahamasisha wakulima kuhusu umuhimu wa mradi huo.

“Mradi huu ni muhimu sana kwa kuwa unawaleta wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya wadi kuja na kulima hapa, kupanda mboga na mimea,” akasema.

Fedha za uimarishaji mradi

Alisema kuwa serikali ya kaunti kwa sasa imetenga kiasi cha Sh5 milioni kuimarisha mradi huo.

“Kupitia kwa mfuko wa hazina ya maendeleo ya wadi, tumetenga kiasi cha Sh5 milioni kuendeleza kilimo hiki,” akasema Bw Mwambire.

Katika bajeti ya mradi huu, Bw Mwambire asema kuwa wanapanga kuweka mashini za kupiga maji ambazo zinatumia mwangaza wa jua.

Vilevile anaongeza kwamba eneo la bwawa lililoharibika litafanyiwa marekebisho ili kuhakikisha kwamba maji yanabakia mengi na kusaidia wakulima.

Serikali ya kaunti katika ripoti yake maalumu ilisema kuwa imaenzisha miradi mingi ya kunyunyizia mashamba maji. Miradi hiyo imesaidia wakazi wengi wa Kilifi kukumbatia kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji kama njia mojawapo ya kukabiliana na baa la njaa.

Ripoti hiyo inajulikana kama ‘A Gem by the Indian Ocean‘.

“Kutoka mradi wa Uhai Marikano ambao una jumla ya ekari 75 na ambao unapatikana katika eneo la Jilore hadi mradi wa Mdachi katika eneo la Ganze, kuna jumla ya ekari 2,000 ambazo zimewekwa katika kilimo cha kunyunyizia mashamba maji,” ikasema sehemu ya ripoti hiyo.