Makala

KILIMO: Ukuzaji wa spinachi kitaalamu zaidi

July 3rd, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

MBOGA aina ya spinachi imesheheni Vitamin K, A, B2, B6, E na C, pamoja madini ainati kama vile Manganese, Folate, Copper na Calcium.

Aidha, mboga hii hukaangwa na kuliwa kama kitoweo kinachoandamana na vyakula vingine.

Pia, hutumika kutengeneza saladi.

Ni aina ya mboga ambayo ni nyepesi na mwororo na isiyo na asidi, hivyo basi wenye shida ya asidi wanapendekezwa kuila.

Kulingana na wataalamu wa kilimo pamoja na wakulima wenye uzoefu wa kuikuza wanasema ni miongoni mwa mboga rahisi kupanda.

Spinachi hustawi katika udongo tifutifu (loam soil) na usiotuamisha maji. “Udongo wenyewe unapaswa kuwa na kiwango cha asidi, pH, 6.4-7,” anasema Bi Caroline Njeri, mtaalamu wa kilimo Safari Seeds.

Kampuni hiyo ni tajika nchini katika utafiti na uzalishaji wa mbegu za mboga aina tofauti, spinachi ikiwamo.

Kulingana na mtaalamu Njeri ni kwamba ufanisi katika kilimo cha mboga unategemea pembejeo; mbegu, fatalaiza na dawa dhidi ya magonjwa na wadudu.

Anatahadharisha kwamba kuna mbegu nyingi duni sokoni, na ambazo zimefisha ari ya wakulima.

“Suala muhimu na la kwanza kuzingatia ni ubora wa mbegu za mboga. Ukulima wa spinachi unafinikishwa na mbegu bora zilizoafikia ubora wa bidhaa,” anashauri.

Mbegu hupandwa katika kitalu ili kupata miche, shughuli inayochukua kati ya wiki 4 hadi 5.

“Vigezo vya kutunza miche kitaluni vitiliwe maanani, ikiwemo mbolea na maji ya kutosha,” anasema mdau huyu, kauli inayotiliwa mkazo na Josphine Nyaboke, mkulima wa spinachi Kasarani, Nairobi.

Kitaluni, Bi Nyaboke anasema baada ya kukiandaa na kupanda mbegu, hukiwekelea nyasi za boji zilizokauka na kumwagalia maji kila asubuhi na jioni.

“Miche huchipuka kati ya siku 5-7. Maji ni kiungo muhimu kwa mimea hiyo michanga, yanapaswa kumwagiliwa kwa utaratibu na umakinifu wa hali ya juu,” anaelezea Bi Nyaboke.

Wakati miche ikiendelea kukua, mkulima anashauriwa kuandaa eneo la kuipanda wiki 2 hadi 3 kabla ya shughuli za upanzi kuanza.

Lima shamba karibu sentimita 20 kuenda chini, litandaze (harrowing) kisha liinue kwa makundi (beds), sentimita 15 kuenda juu ili kuepushia mimea uharibifu wa maji yanapozidi.

“Udongo uchanganywe sawasawa na mbole, kisha maji yamwigiliwe juu iwapo si msimu wa mvua,” anashauri Bi Caroline Njeri.

Kifuatacho, ni uandaaji wa mitaro au mashimo ya upanzi ambapo kutoka laini moja hadi nyingine inafaa kuwa na umbali wa sentimita 30.

Miche inapaswa kung’olewa majira ya jioni au mawingu yatandapo, kwa kuwa miale kali ya jua ni hatari kwa mimea hiyo michanga.

Bi Josphine Nyaboke anahimiza kitalu kimwagiliwe maji kabla ya kuing’oa.

Aghalibu, miche iliyo tayari kwa upanzi huwa na majani kati ya matatu hadi manne.

Upanzi, mche mmoja hadi mwingine kwenye laini uwe na nafasi ya sentimita 15.

Kwenye mashina yake, weka nyasi za boji (mulching) ili kuzuia mnyauko wa maji jua linapoangaza miale kale.

Hata hivyo, unashauriwa kutumia nyasi zilizokauka kwani zile mbichi husambaza wadudu na magonjwa.

Palizi ni shughuli muhimu katika kilimo cha spinachi ili kudhibiti makwekwe yanayoleta ushindani mkali wa lishe; mbolea na maji.

Ni muhimu kukushauri wewe mkulima kuwa mimea inahitaji jua ili kunawiri, na kuwepo kwa makwekwe huzua miale kufikia majani na matawi.

Mbolea ya kisasa hutiwa wiki kadhaa baada ya upanzi kwa minajili ya kunawirisha mispinachi. Usisite kunyunyizia maji.

Muda mrefu

Mwezi mmoja baadaye, spinachi huwa tayari kwa mavuno na kuna baadhi ya zinazovunwa kwa muda mrefu.

Zingatia mzunguko wa mimea (crop rotation), ambapo eneo linalokuzwa spinachi linaweza kupandwa maharagwe, nyanya, giligilani (dania) au viazi.

Mboga hii inapokuzwa eneo moja kwa muda mrefu, magonjwa na wadudu wanaoiathiri hukatalia udongoni.

Wadudu tata kwa spinachi ni; viwavi na vidukari. Magonjwa yanayoathiri mboga hii ni kama vile ukungu na ule wa majani kukauka.

Unahimizwa kutafuta ushauri wa dawa bora kukabiliana na changamoto za magonjwa na wadudu, haswa kutoka kwa wataalamu au maduka ya kuuza bidhaa za kilimo.

Ni muhimu kukumbusha kuwa unapopulizia mimea dawa, ipe muda wa siku 14 sawa na wiki mbili, ukiendelea kuinyunyizia maji kabla ya kuvuna.