Makala

KILIMO: Upanzi wa mchicha

August 14th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BW Peter Wahome amekuwa mkuzaji wa mchicha kwa zaidi ya miaka miwili.

Alianza shughuli za kilimo mwaka 2016 ambapo pia hukuza mboga za kienyeji kama mnavu, spinachi, pamoja na sukumawiki eneo la Kasarani.

Wahome, ambaye pia ni mpishi katika mkahawa mmoja jijini Nairobi anasema alikata kauli kukuza mboga za kienyeji kwa sababu ya urahisi wake kupanda na hata kutunza.

Akitumia mfano wa mchicha, anasema ni mojawapo ya mboga za kienyeji ambazo ni rahisi mno kukuza.

“Kwa jumla, ni kilimo ambacho utaweza kuendesha hata ukiwa na gange nyingine,” Wahome anaeleza.

Kulingana naye, mbegu za mchicha hupandwa kwenye kitalu ili kupata miche, shughuli inayochukua karibu mwezi mmoja.

Wakati miche ikisubiriwa kuwa tayari, mkulima anashauriwa kuandaa eneo la upanzi.

“Kitaalamu shamba linapaswa kuandaliwa wiki kadhaa kabla ya upanzi. Hili litawezesha makwekwe yakauke na udongo kupumua, iwapo lilikiwa limepandwa mimea mingine,” asema Caroline Njeri, mtaalamu.

Mdau huyu wa masuala ya kilimo anasema muda huo husaidia wadudu kuondoka. “Mimea iliyokuwepo awali na hata makwekwe yanapokauka, uwezekano wa magonjwa kusambazwa huwa umedhibitiwa,” afafanua Njeri.

Bw Wahome anasema mitaro yenye urefu wa karibu inchi tatu kuenda chini inaandaliwa, katika upanzi wa mchicha. Aidha, mashimo pia yanaweza kutumika. “Nafasi ya mtaro mmoja hadi mwingine iwe kati ya inchi 6-8,” ashauri mkulima huyu.

Kwa kuwa mchicha ni mboga asilia, mkulima anahimizwa kutumia mbolea ya mifugo au kuku. Pia, inaweza kuimarishwa kwa kuichanganya na majani na matawi, kuunda mbolea mboji au vunde. “Mbolea vunde hupewa muda wa miezi kadhaa kuiva, ambapo huwa imefunikwa kwa karatasi kubwa ya nailoni hasa nyeusi,” aeleza Timothy Mburu, mkulima na mtaalamu.

Hewa au maji, hayapaswi kuruhusiwa kuingia. Kisayansi, karatasi nyeusi ya nailoni inajulikana katika kuvuta na kuongeza kiwango cha joto jua linapoangaza, na kwa mujibu wa maelezo ya Bw Mburu ni kwamba joto hilo kwa mbolea mboji huua wadudu waliomo na hata kuondoa uwezekano wa magonjwa ibuka.

Upanzi wa mchicha, mitaro iwekwe mbolea kisha miche ipandwe na kuongezwa udongo kiasi na kunyunyiziwa maji.

Kwa kuwa miche ni mimea michanga, mkulima anashauriwa kumwagilia kitalu maji kabla ya kuing’oa.

Pia, inapaswa kubebwa kwa umakinifu wa hali ya juu, majira ya asubuhi au jioni, yakiwa bora zaidi kufanya shughuli za uhamishaji na upanzi.

“Ufanisi katika kilimo cha mboga unategemea kuwepo kwa maji. Michicha ukiitunza kwa maji, nayo itakutuza,” anasema Bw Wahome.

Ili kunawirisha mazao, mashina ya mboga yanaweza kutiwa mbolea yenye madini ya Calcium, Ammonia na Nitrogen, hususan fatalaiza. Potassium pia ni madini muhimu.

Mchicha huanza kuvunwa mwezi mmoja baada ya upanzi. Mavuno huendelea kwa muda wa miezi mitatu mfululizo.

“Cha muhimu ni kutunza michicha kwa maji na mbolea,” anaeleza Bw Wahome.

Magonjwa na wadudu wanaoshuhudiwa kwa mchicha ni sawa na ya mboga zingine. Mkulima anahimizwa kupata ushauri wa dawa bora kukabili changamoto hizo. Akizingatia mfumo wa kilimohai, matatizo ya aina hiyo huweza kudhibitiwa upesi.

Michicha inapoachwa kukomaa huzalisha mbegu, ambazo wataalamu wa afya wanasema zimesheheni Protini.

“Mbegu zake zinaweza kusagwa, unga huo utumike katika mapishi ya uji,” amasema mtaalamu Anne Njeri.

Mboga za mchicha, zinaweza kupikwa zikiwa pekee au kuchanganywa na zingine kama mnavu, au saga.

Pia, kuna wanaozichanganya na spinachi au sukumawiki.

Majani ya mchicha yana ukwasi wa madini ya Calcium, Iron, Vitamini A, B na C.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema mchicha husaidia usagaji wa chakula tumboni kwa sababu ya kusheheni Fibre.

Hali kadhalika, ni tiba bora kwa ugonjwa wa kuendes