Kilimo: Wanafunzi 20 wa UoN wanufaika na mpango wa mafunzo yanayosimamiwa na Elgon Kenya

Kilimo: Wanafunzi 20 wa UoN wanufaika na mpango wa mafunzo yanayosimamiwa na Elgon Kenya

NA SAMMY WAWERU

WANAFUNZI 20 wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) waliofuzu kwa taaluma mbalimbali za kilimo wamepata fursa katika kampuni ya Elgon Kenya kuongeza tajiriba.

Kulingana na kampuni hiyo ya pembejeo, jukwaa hilo litawasaidia kuboresha ujuzi na maarifa ya kozi walizosomea.

Hatua hiyo, baada ya mafunzo itawaweka katika nafasi bora kupata ajira katika sekta ya serikali na kibinafsi.

Akisifia ushirikiano wa karibu kati ya Elgon Kenya na UoN, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Dkt Bimal Kantaria amesema mpango huo utasaidia kuimarisha huduma za utoaji ushauri nasaha katika shughuli za kilimo, ikizingatiwa kuwa wanafunzi hao wametumwa katika kaunti wanazotoka.

Mafunzo hayo ya miezi sita yalianza Aprili 2022.

Kila mwanafunzi atapata mshahara wa Sh25,000 kwa mwezi, Dkt Kantaria akidokeza baada ya kunolewa bongo watapokezwa vyeti vya kuhitimu.

“Mpango wote unafadhiliwa na Elgon Kenya, ukigharimu Sh400,000 kila mwezi,” afisa huyo akasema.

“Tutawaandaa kitajiriba ili tuwahami na ujuzi na maarifa ambayo yatawafaa siku za usoni,” akaongeza.

Dkt Kantaria aidha alisema Elgon Kenya inalenga kuziba gapu ambapo waajiri huweka vikwazo, kuajiri wenye uzoefu wa muda mrefu.

Dkt Bimal Kantaria, Mkurugenzi Mkuu Elgon Kenya akizungumzia wanafunzi wa UoN waliopata fursa kunoa makali tajiriba yao katika kampuni hiyo. PICHA | SAMMY WAWERU

Wengi wakiwa vijana waliofuzu vyuoni, inakuwa vigumu kuafikia mahitaji yanayowekwa hivyo basi kuwafungia nje kupata kazi.

“Kama taasisi ya kibinafsi katika sekta ya kilimo na inayochangia mtandao wa uzalishaji chakula nchini, tunapaswa kushirikiana na ile ya serikali,” Dkt Kantaria akahimiza, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo UoN, jijini Nairobi.

Alisema mpango huo utakuwa endelevu, kila baada ya miezi sita.

UoN iliteua wanafunzi hao kwa mujibu wa taaluma walizosomea na kufuzu.

Akielezea kusikitishwa kwake na kero ya uhaba wa chakula nchini hasa ukame unapotokea, Naibu Chansela UoN, Prof Stephen Kiama, alisema gapu hiyo itazibwa endapo wadauhusika na sekta za kilimo watashirikiana.

Prof Kiama alitilia mkazo haja ya wakulima kukumbatia mifumo ya kisasa kuendeleza shughuli za kilimo.

“Ni kupitia ushirikiano tutaweza kunusuru taifa hili, liwe na chakula cha kutosha,” akasema.

Kenya ni miongoni mwa nchi taifa Upembe wa Afrika, inayohangaishwa na janga la ukame.

Nchi nyingine ni Ethiopia na Somalia, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) likionya zaidi ya watu 20 wanakumbwa na baa la njaa.

Prof John Kimenju, mwenyekiti kamati ya Kilimo, Teknolojia na Uvumbuzi UoN, alifichua wanafunzi walioteuliwa kupata mafunzo Elgon Kenya waliteuliwa kutoka kwa kozi nane zinazohusiana na masuala ya kilimo.

Bernice Wangechi ni kati ya wanafunzi waliopata jukwaa hilo la mafunzo, aliyetumwa Kaunti ya Nyeri.

“Ninaridhia na kushukuru fursa niliyopata kupanua mawazo zaidi kitajiriba,” Wangechi akaambia Taifa Leo.

Naye Beverlyne Akwale wa Kiambu, alisema fursa aliyopata itamsaidia kukua kitajiriba kupitia kutangamana na wakulima, akiangazia changamoto zinazowakumba kuendeleza kilimo bora.

  • Tags

You can share this post!

Serikali ya Lamu lawamani kwa kulipa wafanyakazi hewa...

Uhuru awataka wawaniaji wakubali matokeo ya uchaguzi wa...

T L