Kilio beste akiponyoka na bebi wake

Kilio beste akiponyoka na bebi wake

Na JOHN MUTUKU

KAYOLE, Nairobi

POLO mmoja mtaani hapa hajiwezi hajifai kwa machozi baada ya rafiki yake wa dhati kumpokonya mpenzi.

Jamaa hakuamini kuwa rafiki waliyefaana kwa jua na mvua alikuwa akichovyachovya buyu lake la asali.

Polo alikuwa na totoshoo waliyependana kwa dhati, mahaba moto yakifungua ukurasa mpya wa maisha yao.

Walikuwa katika harakati za kukamilisha mipango ya arusi iliyotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh2 milioni. Wawili hao walikuwa wameapa kutoachana huku demu akimhakikishia jamaa kwamba alikuwa akimpenda kwa dhati.

“Nakupenda switi. Nitakuoa tuishi kwa majaaliwa maisha ya raha mustarehe,” polo alimhakikishia demu.

“Nakupenda sana nyota wangu bila kung’aa kwako, maisha kwangu ni giza zito,” demu alimuapia.

Lakini hayo yalifikia kikomo polo alipobisha majuzi kwa rafiki yake na akamfumania akiwa na totoshoo wake. Jamaa hakuamini kupata demu aliyetarajiwa kuoa akiwa kifuani mwa rafiki yake wakinong’onezana matamu waliyoyajua wao wenyewe.

“Switi, yaani umefikia kiwango hiki cha kunisaliti? Nilikutendea nini unisaliti hivi?” polo aliuliza akitokwa machozi.

Demu alimwangalia jamaa na kusonya.

“Mpenzi, hebu mjibu huyu mshenzi maana sina maneno ya kumwambia,” demu alimuomba rafiki wa jamaa.

“Buda, kanyaga nje. Umesikia kutoka kinywani mwake ameshakushiba,” mwenye nyumba alisema na kuufunga mlango.

Huku akitokwa na machozi, jamaa aliondoka na kurudi kwake akijuta kumwamini rafiki yake bila kujua alikuwa fisi.

“Mie siwezi kuolewa na jamaa asiyejua kupenda. Hela anazo lakini penzi hana,” demu alisikika akisema.

Bado polo hajaachilia picha ya demu kumuondoka akilini na moyoni. Huzuni haimwachi japo wenzake washamwambia amtafute mwengine mwenye penzi la kweli.

You can share this post!

Kiambu yaendelea kujiimarisha katika ufugaji wa samaki

FUNGUKA: ‘Sauti nyororo huniyeyusha mzima’