Makala

KILIO CHA HAKI: Sababu za ubakaji kukithiri katika mitaa ya mabanda

May 17th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA
IDADI ya kesi za unajisi wa watoto inaendelea kuongezeka katika Mahakama ya Kibera hasa kutoka mitaa ya mabanda jijini Nairobi. 

Takwimu katika mahakama hiyo zinaonyesha hali ya kusikitisha huku kesi zaidi ya 10 zikifunguliwa kila wiki. Katika mwezi mmoja uliopita, kesi zaidi ya 40 zilisajiliwa katika mahakama hiyo na washtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.

Ingawa sio wote wanaopata dhamana, kuachiliwa kwa washukiwa kunawatia hofu waendeshaji wa mashtaka kwamba huenda wakawatisha waathiriwa na mashahidi.

Waendeshaji wa mashtaka wanasema japo ni haki ya mshukiwa kuachiliwa kwa dhamana, hofu kwamba wanaweza kuwatisha mashahidi haiwezi kuepukika.

Baadhi ya kesi za ubakaji huondolewa na washukiwa kuachiliwa huru baada ya mashahidi kukosa kufika kortini na juhudi za polisi kuwasaka kukosa kufua dafu.

Miongoni mwa kesi za ubakaji  zilizosajiliwa majuzi ni ya Keith Mbugua na Edwin Aluda kutoka kituo cha polisi cha Muthangari kinachohudumia mtaa wa Kawangware miongoni mwa mingine, Kelvin Orenge, Alfred Simbiri, Godffrey Osiemo na Romano Mbaya kutoka kituo  cha polisi cha Kabete na ya Salim Makhanu na Julius Mwangi kutoka kituo cha polisi cha Langata.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa walidaiwa kuwanajisi watoto baadhi yao wenye umri wa miaka mitatu. Rekodi hizo zinaonyesha kwamba washukiwa waliachiliwa kwa dhamana ya kati ya Sh200,000 na Sh300,000.

Hali ni mbaya hivi kwamba Jaji Mkuu David Maraga  anawataka wazee kuingilia kati na kuwashauri vijana kuepuka kujihusisha na visa hivi. Akizungumza alipozuru mahakama zilizoko Magharibi mwa Kenya mapema mwaka huu, Jaji Maraga alitaja kesi hizi kama janga linalofaa kukabiliwa na kila mmoja.

Rekodi katika mahakama hiyo zinaonyesha kwamba visa vingi hutokea mitaa ya mabanda ya Kawangware, Riruta, Kangemi, Kabete na Kibera ambayo inaishi watu wengi wa mapato ya chini.

Viongozi wa mashirika ya kijamii na ya kutetea watoto wanasema maisha ya wasichana katika mitaa ya mabanda yamo hatarini.

“Maisha ya wasichana yamo hatarini kwa sababu ya tisho la wanajisi. Tunashughulikia visa vya unajisi kila wakati na vinazidi kuongezeka,” alisema mtoaji ushauri nasaha kwa watoto Jane Atieno wa shirika la Just a Kid Foundation.

Alisema mbali na visa vinavyoripotiwa, wanahofia kwamba  kuna visa vingi ambavyo haviripotiwi kwa sababu ya mila na vitisho kutoka kwa washukiwa.

Takwimu za polisi zinaonyesha wanaohusika na ukatili dhidi ya wasichana na wanawake ni vijana walio na umri wa kati ya miaka 18 na 36 japo kuna watu wa umri mkubwa wanaoshtakiwa.