Habari Mseto

Kilio cha msichana aliyepita KCPE 2023 kukosa kujiunga na shule ya upili   

February 26th, 2024 1 min read

NA SAMMY KIMATU

MSICHANA mwenye umri wa miaka 13 eneo la Njiru, kaunti ya Nairobi ameendelea kusalia nyumbani kwa kukosa karo kujiunga na kidato cha kwanza licha ya wanafunzi wenza kuendelea kukata kiu cha masomo.

Msichana huyo alifanya mtihani wa Kitaifa Darasa la Nane (KCPE) mwaka jana, na zaidi ya mwezi mmoja baada ya wenzake kujiunga na kidato cha kwanza ndoto zake kuingia shule ya upili zinazidi kufifia.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali, Msaidizi wa Kamishna wa Kaunti katika eneo la Njiru, Bi Florence Syokau alisema msichana Stacy Ochieng alizoa alama 366 katika KCPE 2023, japo hajaweza kujiunga na shule ya upili kwa sababu ya ukosefu wa karo.

Stacy alikuwa akisomea katika shule ya Msingi ya Brisbane Cincinnati katika kaunti ndogo ya Njiru na alipata barua ya kujiunga na St Francis Rangala Girls.

Stacy Ochieng, mwanafunzi aliyekosa karo kujiunga na kidato cha kwanza akiwa na Msaidizi wa Kamishna wa Kaunti katika eneo la Njiru, Bi Florence Syokau. PICHA|SAMMY KIMATU

Bi Syokau alisema kutokana na umaskini wa kupindukia ambao familia yake inapitia, wazazi wake hawawezi kumudu kupata karo ya binti yao.

Bi Syokau alisema msichana huyo alipatikana akilia kwa kukosa kuwa shuleni, akikumbuka wenzake waliofanikiwa kuingia shule za upili wanakuja nyumbani wiki ijayo kwa likizo fupi ya muhula wa kwanza.

“Msichana huyo analia bila kujizuia akiwazia wenzake waliobahatika kupata nafasi katika kidato cha kwanza jinsi watarejea nyumbani wiki ijayo kwa mapumziko ya katikati ya muhula,” Bi Syokau akasema.

Bi Syokau aliongeza kwamba msichana huyo anatamani elimu na akaomba wahisani na wasamaria wema kujitokeza kumsaidia.

KCPE 2023, ilifunga jamvi la mfumo wa 8-4-4 ambao nafasi yake imetwaliwa na mtaala mpya wa CBC.

[email protected]