Makala

Kilio cha mwanamke mgonjwa aliyekwama Saudi Arabia

April 17th, 2024 3 min read

NA OSCAR KAKAI

MWISHONI mwa mwaka wa 2021, Emily Cherop Kaptuwai mwenye umri wa miaka 27, alipanga virago vyake na kutoka kwenye kijiji chake akiwa mwenye furaha na matumaini makubwa.

Akiwa na lengo la kujitafutia riziki, Bi Kaptuwai ambaye anatoka kijiji cha Murkwijit, Pokot Magharibi alisafiri kwenda kazi Saudi Arabia, ambapo alipata kazi kama yaya nyumbani.

Hata hivyo, ndoto zake zimefifia na kuharibika. Mama huyo wa watoto watatu sasa ni mgonjwa na amekwama Uarabuni.

Imebainika kuwa, Emily ambaye amelazwa hospitalini aliondoka kwenye boma la mwajiri wake akiwa mgonjwa katika mazingira yasiyoeleweka.

Kutokana na video ambayo inazungushwa kwenye mitandao, Emily anasikika akiomba msaada ili aokolewe na kuondoka kutoka taifa hilo la kigeni.

Akisimulia masaibu yake bila kutaja hasa yale ambayo yalijiri na ni nani aliyemkosea, Emily anasema kuwa alipokonywa kila kitu ikiwemo begi na hela zake zote.

“Ni stori ndefu; Ninahitaji tu usaidizi nirejee nyumbani. Niko hospitalini na niliokolewa na Msamaria Mwema. Sina njia yeyote ya kurejea nyumbani. Stakabadhi zangu zote zikiwemo pasipoti na kitambulisho muda wake umeisha,”anasema Bi Kaptuwai.

Uchunguzi unaonyesha kuwa Bi Kaptuwai sasa yuko katika hospitali ya King Salman, chumba nambari 212A katika mji wa Riyadhi akipokea matibabu.

Nyumbani Kenya, familia yake haina furaha kuwa msichana wao huenda akafariki akiwa huko Saudia.

Familia hiyo sasa inaiomba serikali kuingilia kati na kusaidia kurejesha mwana wao nyumbani Kenya.

Vilevile, imewaomba Wakenya kuchangisha fedha ambazo zitasaidia kumrejsha mwana wao nyumbani.

Mumewe Emily, John Wekesa Wamukota ambaye anaishi na wanawe watatu katika kijiji cha Downtown Ekegoro, wadi ya Sinyerere, Kaunti ya Trans-Nzoia anaomba usaidizi wa kumrejesha mkewe nyumbani ambaye amekwama ugenini.

Anasema kuwa walikuwa wakiwasiliana kila mara hadi juzi ambapo hakuwa anapatikana.

Kulingana na yeye, Emily amekwama kwenye nchi hiyo tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Habari kumhusu bado ni finyu

John Wekesa Wamukota mumewe Emily Kaptuwai ambaye anasimulia jinsi hali ya umaskini imemzuia kupata pesa za kumsafirisha mkewe nyumbani kwa matibabu. Picha|Oscar Kakai

“Hatujaelewa hasa kile ambacho kilimfanyikia. Kama familia hatujapata ukweli kuhusu hali yake,” anasema.

Mume huyo mwenye huzuni anasema kuwa habari kumhusu mkewe bado ni finyu.

“Tunaumia kimawazo ninataka tu arejee nyumbani. Hatuna chochote lakini hapa ni salama. Anafaa kurejea nyumbani kuishi na kile tuko nacho,” anasema Bw Wekesa.

Bw Wekesa anasema kuwa mkewe alikuwa na kandarasi ya kazi ya miaka miwili nchi ya Saudia ambayo iliisha mwaka jana na amekuwa akilalamikia kazi ngumu ya kufanya muda mrefu, kuwa mgonjwa hasa kuumwa na kichwa.

“Maisha yalikuwa magumu hapa Kenya. Hatukuwa na fedha na tuko na watoto shuleni. Tulielewana yeye aende Saudia na mimi nibaki  nilee watoto. Tulifaa kupanga maisha yetu ya siku za usoni,” anasema Bw Wekesa.

Anasema kuwa mara ya kwanza, Emily alikuwa ameenda Saudia mwaka wa 2013 kwa kandarasi ya kazi ya miaka miwili kisha akarejea.

“Mara ya kwanza, hakukuwa na shida. Mwaka wa 2013 alienda ambapo muda wa pasipoti yake uliisha na walikuwa kwenye mchakato wa kutafuta nyingine ndiposa arejee nyumbani. Imekuwa miaka 11 tangu apate pasipoti yake. Tajiri wake alikuwa ameahidi kumsaidia apate nyingine lakini ikachelewa. Stakabadhi zake zote ziliwekwa na mdosi  wake. Alifaa kurejea Disemba mwaka jana,” anaeleza.

Bw Wekesa anasema kuwa maisha yake yamekuwa salama hadi wiki jana.

“Ijumaa Aprili 5, 2024 aliniambia kuwa mawimbi ya mawasilianao yake yatakatwa na hatapatikana. Simu yangu ilipata shida na kila kitu kikapotea. Aliniambia kuwa niulize ndugu yake Tito anipe nambari ya ajenti wake. Jumapili alinitumia ujumbe wa kutaka nimpigie simu nikajua yuko salama na anataka mawasiliano nami. Nilimrejeshea ujumbe sawia na huo kuonyesha kuwa imeona ombi lake. Nilimpigia Tito anipe nambari ya ajenti lakini nilipomgia alikataa kuwa yeye sio ajenti. Baabaye rafiki ya Emily kwa jina Kala anilipigia Aprili 10, 2024, na kuniuliza ikiwa nimeongea na Emily. Nilimwambi tuliongaea Ijumaa,” anaeleza Bw Wekesa.

Anasema kuwa msichana mwingine kutoka Saudia alimtumia picha ya mkewe akiwa amelazwa kwenye hospitali.

 

“Mimi sina kazi, sina pesa za kumrejesha nyumbani,” anasema.

Dadake Emily, Silvia Kaptuwai anasema kuwa wanataka mwana wao kutibiwa akiwa hapa Kenya na wala sio nchi ya kigeni.

“Nilizungumza na Emily wiki moja iliopita. Alikuwa anaulizia hali ya mwanawe. Ana watoto wadogo. Mimi nilipata habari hizi kwenye mtandao. Nasikia simu yake ilichukuliwa. Tunamtegemea sana,” anasema Silvia.

Silvia anaelezea masaibu na hali ya uchochole iliyowakumba kisha Emily akalazimika kuenda kutafuta riziki nje ya nchi kuliko kuishi bila shughuli.

 

Taifa Leo ilifanikiwa kuwasiliana na Emily Jumamosi usiku kupitia mtandao wa WhatsApp akasema anaendelea kupata matiabu lakini anavuja damu kutoka ndani ya tumbo.

Anasema kuwa anataka tu kuondolewa Saudia.