Habari Mseto

Kilio cha wagonjwa wa figo mashine zikikwama

May 25th, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

WAGONJWA wa figo katika kaunti ya Kilifi wanaendelea kuhangaika kufuatia kuharibika kwa mashine za kusafisha damu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti Kilifi.

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alizindua rasmi kitengo hicho cha kuwahudumia wagonjwa wa figo mnamo Agosti 2023 lakini kimekosa kuwafaa wagonjwa ambao wanahitaji huduma kwa dharura.

Baadhi ya wagonjwa waliokuwa wameratibiwa kutibiwa Alhamisi walikosa huduma hizo kwani mashine zote tatu zilikuwa zimeharibika.

Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi, Mzee Francis Konde kutoka Kakanjuni alisema alianza matibabu yake katika hospitali hiyo na wakati huo mashine zote tatu zilikuwa zinafanya kazi vizuri.

Ila alipokuwa akiendelea na matibabu mashine zilianza kuharibika moja baada ya nyingine.

“Sote hapa tumefika kupata matibabu lakini mashine zote tatu hazifanyi kazi,” akasema Bw Konde.

Mzee Konde alieleza ya kwamba juma lililopita alifanyiwa matibabu yake kama ilivyoratibiwa na wakati huo ni mashine mbili zilikuwa zinafanya kazi lakini kufikia Alhamisi asuhuhi hangeweza kuhudumiwa kwani mashine zote zilikuwa zimeharibika.

“Daktari alitueleza kuwa mashine zimeharibika na walikuwa wameita mafundi kurekebisha lakini kufikia wakati tunatoka hospitalini hakuna mtu yeyote alikuwa amefika,” akasema.

Alisema kuwa imekuwa changamoto kwa wagonjwa wachochole kutafuta huduma katika hospitali za kibinafsi kwa sababu ya ukosefu wa pesa.

“Inagharimu mgonjwa Sh10,000 kutibiwa mara moja katika hospitali ya kibinafsi na wengi wetu hatuwezi kwa sababu ya gharama kubwa ya matibabu. Tunahofia maisha yetu kwa sababu wakati tulikuja hospitalini hapa tulipewa ratiba ya kufanyiwa matibabu na iwapo mgonjwa atakosa, inaathiri afya pakubwa,” akasema.

Alisema kuwa madaktari walikuwa wanuia kubadilisha ratiba zao za matibabu jambo ambalo linawapa wasiwasi zaidi.

“Tunateseka sana na licha ya madaktari kutupa moyo kuwa mashine zitakuwa sawa, hatujui ni hadi lini,” akasema.

Askofu Cosmas Tuji wa Kanisa la Kimethodisti kutoka Ribe alisema kuwa ameugua matatizo ya figo kwa miaka mitatu sasa na kwa muda huu wote alikuwa anasafiri hadi katika hospitali ya Malindi.

Alisema licha ya kitengo cha kuwahudumia wagonjwa wa figo kuzinduliwa rasmi na gavana Mung’aro mwezi Agosti, kilianza kufanya kazi mnamo Oktoba 2023.

“Tulifurahi kitengo hicho kilipoanzishwa Kilifi kwani ilitupunguzia mwendo wa kwenda Malindi,” akasema Bw Tuji.

Alisema mashine ya kwanza iliharibika mnamo Desemba na wagonjwa wameteseka kwa muda huo wote.

Mashine za kusafisha figo. PICHA | MAKTABA

Mzee Hariri Kazungu kutoka kijiji cha Roka alisema kuwa familia yake hujawa na wasiwasi kila mara anapokosa kufanyiwa matibabu kwani hali yake ya afya inaendelea kudhoofika.

“Tunatoa wito kwa serikali kutengeneza mashine ili kutupunguzia mateso,” akasema.

Bw John Juma alieleza masikitiko yake kuwa wagonjwa wengi wanaendelea kuteseka na kufa nyumbani kwa sababu ya umaskini.

Alieleza kuwa baadhi ya wagonjwa ambao hufanyiwa matibabu wameaga dunia.

“Ukikosa kufanyiwa matibabu unachungulia kifo kwa sababu uchafu unajaa mwilini na wagonjwa wengi wamegadhabika na kuharibika kwa mashine yote,” akasema Bw Juma.

Alieleza kuwa licha ya ahadi ya ahadi ya gavana kuwa angeongeza mashine kumi na tatu zaidi kuwahudumia wagonjwa hakuna kilichotendeka kwa sasa.

“Tumeamua kuongea kwa sababu wengi wetu hawawezi kupaza sauti zao na tunaendelea kuteseka huku idadi ya wagonjwa ikongezeka,” akasema.

Alisema watoto na wazee wameathirika sana kwani kukosa matibabu huwafanya kupitia changamoto nyingi mwilini na maumivu.

Bw Hamisi Ali kutoka kijiji cha Kiwapa alisema inasikitisha kuwa serikali iimewanyima wagonjwa haki ya kupata huduma bora za afya.

“Tunafahamu ya kuwa mgonjwa wa figo atapona iwapo atapata matibabu kikamilifu bila kukatizwa. Lakini wagonjwa katika Hospitali ya Kilifi wakianza kukosa huduma muhimu, jamii inaingiwa na hofu,” akasema Bw Ali.

[email protected]