Habari za Kitaifa

Kilio cha wakulima wa miwa ikielekea kuozea shambani

April 16th, 2024 2 min read

NA VICTOR RABALLA

WAKULIMA wa miwa sasa wanaitaka Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) kuamuru viwanda vya kutengeneza sukari kurejelea shughuli za kawaida kuzuia uharibifu wa miwa iliyokomaa.

Wanalalamika kwamba hatua ya kampuni hizo kusaga kiwango kisichokamilifu cha miwa inaibua wasiwasi miongoni mwa wakulima kwamba huenda miwa yao ikavunwa ikiwa imechelewa na hivyo kupata hasara.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Miwa Nchini (KSGA) Richard Ogendo, Jumatatu, Aprili 15, 2024 alisema kuna wakulima ambao miwa yao haijavunwa miezi sita baada ya kukomaa.

“Kuna miwa ya kutosha na hivyo AFA inafaa kuruhusu viwanda kuendesha shughuli kwa ukamilifu kulingana na uwezo wavyo,” akasema Bw Ogendo.

Alisema endapo uvunaji wa miwa utacheleweshwa zaidi, wakulima watapata hasara kwani miwa yao itapoteza madini ya “sucrose” na uzani.

“Sawa na biashara nyingine, wakulima wanahitaji kuvuna faida kutoka kwa uwekezaji wao. Uvunaji wa miwa ukicheleweshwa wakulima watakosa pesa za kuwawezesha kuwalipia karo watoto wao baada ya shule kufunguliwa mwezi ujao,” Bw Ogendo akaeleza.

Desemba 2023, AFA iliviruhusu viwanda vya sukari katika maeneo ya Magharibi na Nyanza kurejelea shughuli baada ya marufuku ya miaka mitano.

Marufuku hiyo iliwekwa Julai 2023 ili kutoa nafasi kwa miwa kukomaa mashambani.

Hii ni baada ya AFA kupata habari kuhusu visa vya uvunaji miwa ambayo haijakomaa huku baadhi ya viwanda vikosa miwa.

“Baadhi ya viwanda vilikuwa vikiendesha shughuli kwa kiwango cha chini ya asilimia ya uwezo wavyo,” akasema kaimu mkurugenzi wa AFA Jude Chesire.

Baada ya kuondolewa kwa marufuku hiyo, AFA ilisema kuwa viwanda vya kutengeneza sukari vinaweza kuhudumu kwa siku 15 kwa mwezi huku vikisaga hadi tani 600 ya miwa kila siku.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Kitaifa la Wakulima wa Miwa (KNFSF) tawi la Transmara, tephen Ole Narup kwa upande wake alisema kuwa miwa imekomaa kwa wingi wakati ambapo serikali imetangaza kupungua kwa bei ya miwa.

Ndani wa muda wa miezi miwili iliyopita, alisema, bei ya miwa imeshuka kutoka Sh6,8000 hadi Sh5,100 kwa tani moja.