Habari

Kilio cha wandani wa Ruto kicheko cha ODM, Wiper na Kanu

July 15th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa ODM, Wiper na Kanu na wale wa mrengo wa ‘Kieleweke’ katika chama cha Jubilee wanatarajiwa kutwaa nafasi za uongozi wa kamati za bunge katika chaguzi zinazoanza Alhamisi, Julai 16, 2020.

Hii ni baada ya orodha mpya ya wanachama wa kamati kuidhinishwa ambapo washirika wa Naibu Rais William Ruto wamepokonya nafasi katika kamati zenye ushawishi mkubwa.

Orodha hiyo imeidhinishwa Jumatano baada ya kiongozi wa wengi Amos Kimunya kukubaliana na wazo la kiongozi wa wachache John Mbadi kwamba wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wasipewe nafasi katika kamati tatu muhimu kufanikisha kupitishwa kwa ripoti ya BBI.

Hizo ni; Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC), Kamati kuhusu Sheria za Ziada na Kamati kuhusu Bajeti.

Kamati hizi pia zinachangia pakubwa kufanikishwa kwa mchakato wa mageuzi ya Katiba kupitia bunge na kura ya maamuzi.

Katika uchaguzi wa kesho Alhamisi Mbunge wa Kangema Muturi Kigano (Jubilee) na mwenzake wa Rarieda Otiende Amollo (ODM) wanatarajiwa kuchaguliwa kwa urahisi kuwa mwenyekiti na naibu mwenyekiti wa JLAC, mtawalia.

Awali, nafasi hizo zilikuwa zimeshikiliwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo na mwenzake wa Kandara Alice Wahome; ambao ni washirika wa Dkt Ruto.

Naye Mbunge wa Kieni Kanini Kega ambaye ni mkereketwa wa mrengo wa ‘Kieleweke’ anatarajiwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, nafasi ambayo zamani ilishikiliwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa.

Bw Ichungwa ambaye ni miongoni mwa wabunge 16 wandani wa Dkt Ruto ambao waling’olewa kutoka uongozi wa kamati za bunge kwa madai ya kumkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta, ameteuliwa kuwa mwanachama wa Kamati kuhusu Huduma za Wabunge.

Akikubali nafasi hiyo Bw Ichung’wa aliibua kicheko aliposema: “Nitatumia nafasi hii kuwahudumia wenzangu wazee kama vile Jimmy Angwenyi na Maina Kamanda wakati huu wa janga la Covid-19.”

Naye Mbunge wa Tiaty William Kamket (Kanu) kesho Alhamisi anatarajiwa kuchaguliwa, bila upinzani mkubwa, kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria za Ziada. Cheo hicho kilipokonywa Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Uasin Gishu Gladys Boss Shollei.

Naye Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Busia Florence Mutua (ODM) anatarajiwa kutunikiwa nafasi ya mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Kuhusu Elimu ambayo ilipokonywa Mbunge wa Tinderet Julius Melly.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga (ODM) sasa ndiye ataongoza Kamati ya Bunge kuhusu Fedha, baada ya Mbunge wa Kipkelion Mashariki Joseph Limo kupokonywa wadhifa huo.

Na Mbunge wa Mavoko Patrick Makau (Wiper) ndiye sasa atakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Michezo na Leba ambayo zamani ilishikiliwa na mwenzake wa Machakos Mjini Dkt Victor Munyaka.