Habari za Kitaifa

Muguka: Viongozi wa kidini walia ‘jaba baze’ zasambaratisha ndoa nyingi

May 31st, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

VIONGOZI wa dini ya Kiislamu wamewafokea wanaume watafunaji wa muguka na miraa kwa kile wanachodai ni kuwatesa wake zao.

Katika kikao na wanahabari kisiwani Lamu, viongozi hao, ikiwemo maimamu na maustadh waliwasuta waraibu wa muguka na miraa na kushikilia kuwa ni kupitia hizo hizo ‘jaba base’ ambapo ndoa nyingi zinaendelea kusambaratika ilhali zile zinazoendelea zikiwa ni za wanandoa kuvumiliana tu.

Imamu Mkuu wa Msikiti wa Jamia mjini Mokowe, Mohamed Bwanamkuu alifoka kuwa miaka ya sasa imeshuhudia waume wengi, hasa wale wanaokula muguka wakigeuzwa goigoi, ambapo ikifika jioni wao huchomoka nyumbani kwenda kuchana na wenzao hadi usiku wa manane.

Hilo limewaacha wanawake waliojipamba tayari kwa shughuli za chumbani usiku wakisalia pweke na kuungulika moyoni.

Bw Bwanamkuu alitaja muguka kuwa malevya yasiyokuwa na umuhimu wowote ila kuletea wanaume madhara.

Alieleza masikitiko yake kwamba wanaume wengi wa umri mdogo Lamu, Pwani na nchini kwa jumla wamegeuzwa kuwa ‘wanaume suti’ ambapo fikra zao nyingi zimejikita kwa muguka.

“Imekuwa hata mume kutenga muda wa chumbani na mkewe ni ngumu. Mke anajitahidi kujipamba na kujifukiza akijua fika kwamba jioni imeingia ya kuwa na muda mwema na mumewe, kumbe mume huyo ni wa kuchomoka chumbani kwenda kuchana miraa na muguka hadi usiku wa manane na kisha kurudi chumbani kujikoromea tu usingizini,” akasema Bw Bwanamkuu.

Aliiomba jamii ya Lamu na Pwani kwa ujumla kuungana na kupiga vita muguka na miraa ili isiendelee kuingizwa na kuuzwa maeneo hayo.

Alisisitiza kuwa ili kufaulu kukikomboa kizazi cha sasa na kijacho, lazima ushirikiano na msimamo dhabiti uwepo kupiga marufuku biashara ya muguka ambayo alisema imeathiri Lamu na maeneo mengine ya Pwani.

“Hatuwezi kuwa na kizazi ambacho wanaume wanasalia kuwa mabwege. Tumepokea malalamishi mengi kutoka kwa wanandoa, hasa wanawake, wanaodai kukosa kukidhiwa mahitaji yao ya chumbani na wanaume wao. Huwezi kumwacha mkeo akihesabu paa, milingoti au boriti chumbani ilhali wewe ukikesha kutafuna muguka. Hatutaki tena muguka Lamu,” akasema Bw Bwanamkuu.

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK), Kaunti ya Lamu, Ustadh Abubakar Shekuwe, alitaja muguka kuwa janga eneo hilo, hivyo wafaa kuondoshwa kabisa.

Ustadh Shekuwe alisema msimamo wa waumini, maimamu, viongozi na wazee wa Lamu ni kwamba serikali ya kaunti ya Lamu, ikiongozwa na Gavana, Issa Timamy, isimama kidete kupiga marufuku biashara ya muguka na miraa kote eneo hilo.

Alisema utumizi wa muguka umeathiri na hata kuharibu pakubwa mambo mengi Lamu, ikiwemo elimu, afya, uchumi na akili za vijana.

“Hatuoni faida ya muguka ila hasara tu. Na ndio sababu msimamo wetu ni kwamba hatutaki muguka Lamu. Furaha yetu ni kumuona gavana wetu, Issa Timamy akipiga marufuku na kuondosha kabisa uuzaji na usambazaji wa muguka eneo hili,” akasema Bw Shekuwe.

Mwakilishi wa vijana, Abdul Karim pia alieleza hofu yake kuhusiana na jinsi muguka na miraa ilivyoathiri masuala mengi ya kijamii.

Kulingana na Bw Karim, hata wazazi wamekuwa wakikwepa majukumu yao ya ulezi na kutenga muda wao mwingi katika kutafuna muguka.

Isitoshe, baadhi ya waraibu wa muguka na dawa nyingine za kulevya wameshindwa kabisa kukimu gharama ya kuendelea kuikata kiu yao ya muguka na malevya, hivyo kugeukia wizi vichochoroni na mitaani ilmradi wapate hela za kukimu hitaji hilo.

Bw Karim alisema afueni itapatikana tu wakati ambapo muguka utapigwa marufuku kabisa Lamu na Pwani.

“Unapata wazazi wanatelekeza malezi ya watoto wao. Wanashindwa kuwasomesha ilhali fedha na muda mwingi ukitumika kwenye uraibu wa muguka. Jamii inaendelea kuzorota na tunaelekea kubaya. Tunaamini kuwa ikiwa huwezi kumnufaisha mtu basi kumdhuru pia usimdhuru. Twahisi muguka hautunufaishi kwa lolote ila unatudhuru na kutuzorotesha,” akasema Bw Karim.