Makala

Kilio mji wa Makutano ukigeuka makao makuu ya taka

June 1st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MJI wa Makutano ulioko katika mipaka ya kaunti za Kirinyaga, Murang’a na Machakos, wenyewe ukiwa ndani ya Kaunti ya Embu, umejipa sifa ya kuwa mchafu ajabu, wakazi wamelalamika.

Wanalia kwamba magonjwa yanayoambatana na uchafu kama kipindupindu yameongezeka huku mbu kuzaana katika mitaro hiyo ya maji machafu ikiwa ni hali ya kawaida.

Hatari nyingine ambayo wakazi wameteta kuhusu mji huo ni uchafu huo kuwavutia mbwa walio na kichaa na ambao huwafanya wahofie kuumwa.

Nao wenyeji wamechukua fursa ya uchafu huo kuzidisha hali ya hatari kupitia kutumia vichochoro kama vyoo vya umma kwa haja kubwa na ndogo.

Mitaro iliyojaa uchafu wa vyoo ukitiririka na kukwama, huupa mji huu uvundo.

Wapangaji hulazimika kuweka vidaraja vidogo vya kuvuka uchafu huo hadi kwa milango ya kuingia kwa nyumba zao.

Aidha, vichochoro vya mji huo ulio na sifa za kuwa na masoko ya mifugo, bidhaa za kilimo cha mboga na matunda na pia soko la mapenzi, huwa vimejaa kila aina ya taka ikiwemo mipira ya kondomu na sodo.

Pia, mji huu wa Makutano hufahamika vyema kwa kuwa ngome ya genge la kukamua mafuta kutoka kwa malori.

“Huu ni mji ambao serikali ya Kaunti ya Embu imeupuuza kiasi kwamba tunaonekana tu kama taka yenyewe. Tukipeleka malalamishi kwa vitengo husika huwa tunaambiwa tusubiri bajeti iandaliwe. Hadi sasa nikiwa nimeishi hapa takriban miaka 13, sijajua siku hata moja ya usafi hapa,” akasema Bw James Muema.

Naye Bw Stephen Mutiso ambaye ni mmiliki wa nyumba za upangaji, aliambia Taifa Leo kwamba mji huo umetelekezwa na serikali ya kaunti kwa kuwa matingatinga hayatumwi kukata mitaro ya majitaka.

“Tangu serikali za ugatuzi zizinduliwe, mimi sijawahi kuona wafanyakazi wa kudumisha usafi mtaani wala tingatinga la kufungua baadhi ya barabara za vichochoroni,” akasema Bw Mutiso.

Aliyekuwa Gavana wa Embu Bw Nyaga Wambora aliambia Taifa Leo kwamba mji huo wa Makutano huwa na changamoto kadha kwa kuwa kile kinachousumbua zaidi ni ukosefu wa miundombinu ya utupaji taka.

Alisema kwamba mji huo wa Makutano huwa na changamoto ya kukua kwa kasi kutokana na wengi kuuhamia.

“Hali hiyo inaufanya mji huo kuzidiwa na taka ya vioo na pia aina nyingine za taka na hatimaye kuufanya uwe mchafu. Shida ni kwamba ujenzi wa miundombinu ya utupaji taka ni jukumu la serikali kuu,” akasema Bw Wambora.

Naibu Gavana wa Embu Bw Kinyua Mugo alisema kwamba iwapo mji huo utapata hadhi ya kuwa manispaa, utabahatika na ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) wa kurekebisha miundombinu.

“Tutafanya juu chini kurekebisha hali ya usafi Makutano. Ni ukweli tuko na shida hapo ikiwemo ya mabomba ya kusafirisha majitaka kupasuka. Tunajua pia kuna wamiliki wa nyumba ambao matangi yao ya vioo yakijaa huwa wanayafungua na uchafu huo kutapakaa mitaani,” akasema Bw Mugo.

Bw Mugo alisema kuna mpango ambao unasukwa wa kuupa mji huo sura mpya.

“Kuna barabara mbili ambazo zitawekwa lami ndani ya mji huo. Tutaweka mikakati ya kupiga msasa vichochoro hivyo na kuhakikisha uzoaji taka unakumbatiwa,” akasema.