Kilio wageni wakiwadhulumu watoto kingono Pwani bila kujali

Kilio wageni wakiwadhulumu watoto kingono Pwani bila kujali

Na MWANDISHI WETU

VISA vya Wazungu kuwadhulumu wasichana wadogo kimapenzi vinaendelea kufanyika katika sehemu kadhaa za eneo la Pwani.

Eneo la Pwani limekuwa katika vichwa vya habari kama sehemu ambayo ni maarufu kwa utalii wa ngono inayohusisha wasichana wa umri mdogo.

Umasikini umelaumiwa kuwa chanzo cha wasichana wadogo kujitosa kwenye tabia hiyo ya kufanya ngono ili wapate pesa za haraka za kujikimu maisha yao.

Hivi majuzi, Waisraeli wawili walitiwa mbaroni baada ya kupatikana na wasichana wawili katika jumba moja lililoko eneo la mtaa wa Bamburi mjini Mombasa.

Wawili hao, Bw Ashush David na Bw Koren Avraham sasa wanakabiliwa na kesi ya ulanguzi ya watoto na kuendeleza biashara ya umalaya wa watoto.

Korti imeambiwa kwamba Bw Avraham na Bw David waliwashawishi wasichana hao wenye umri wa miaka 14 na 15 na Sh14,000 na simu mbili za bei ghali kabla ya kuwafungia katika nyumba moja huko Bamburi.

Stakabadhi zilizowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji zinaonyesha kuwa watu hao waliwaonea watoto hao na kuwadhulumu kimapenzi.

Bw Avraham anakabiliwa na shtaka tofauti ambapo serikali imemtuhumu kwa ukahaba wa watoto, ambapo inasemekana alimpa mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 15 simu ya rununu na Sh7,000 akiwa na nia ya kumdhulumu.

Bw David pia anasemekana kumpa mtoto wa umri wa miaka 14 simu ya rununu na Sh7,000 akiwa na nia ya kumnyanyasa.

Mama wa mmoja wa watoto hao (jina twalibana) pia ameshtakiwa kwa kushindwa kumlinda mtoto wake na kufaidika kwa kipato kilichotokana na kitendo hicho.

Hata hivyo, imegunduliwa kuwa Waisraeli hao wawili waliorudi kwao baada ya kupewa dhamana bado hawajarudi kuendelea na kesi hiyo ya jinai.

Miaka miwili iliyopita, raia wa Ukraine na Ujerumani walikamatwa na kufunguliwa mashataka baada ya kumdhulumu msichana kingono.

Bw Zerbin Sascha Marius Waldermar (Mjerumani) na Wectabe Shestavetskyi (raia wa Ukraine) walishtakiwa kwa kumtoa nguo kwa nguvu Bi YMN na kumpiga picha na video akiwa uchi bila ya idhini yake huko Mtwapa, Kaunti ya Kilifi.

Msichana huyo alikuwa amekutana na Bw Waldermar kupitia kwa mtandao wa kijamii.

Wazungu hao wanadaiwa kutaka kufanya mapenzi na mwanamke huyo kwa nguvu.

Katika kisa kingine, Mturuki, Bw Osman Elsek anakabiliwa na mashtaka ya kuwadhulumu kimapenzi wasichana watatu.

Hata hivyo, Mahakama ya Juu imeamuru kesi hiyo kuanza upya baada ya kupata kwamba kulikuwa na makosa jinsi kesi hiyo ilivyofanyika katika Mahakama ya Hakimu.

You can share this post!

Mishi Mboko ajiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana

PSG yapepeta Lyon kwenye mechi ya kwanza ya Messi katika...