Dondoo

Kimada atumia kafyu kuadhibu polo

December 16th, 2020 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KAYOLE, NAIROBI

JAMAA mmoja mtaani humu alilazimika kulala nje ya mlango wa nyumba ya mpango wake wa kando kidosho alipomtimua kwa kukosa kutimiza masharti aliyokuwa amemwekea.

Kulingana na mdokezi, kila mwisho wa mwezi, polo alistahili kumpeleka demu kujivinjari katika eneo la burudani. Pia polo alifaa kumnunulia mizinga miwili ya pombe.

Inadaiwa mwezi ulipoanza, polo hakuonekana kwa nyumba ya kidosho. Hata simu za kidosho hakuwa akizipokea naye mwanadada akaapa kumuadhibu.

Habari zilizotufikia zinasema baada ya wiki moja polo alifika kwa kidosho kama ilivyokuwa desturi yake,

“Sasa beib, siku nyingi hatujaonana,” polo alimueleza kidosho.

Inadaiwa kidosho alijitia hamnazo. Aliendelea na shughuli zake za kuandaa chajio.

“Leo utajua hujui. Unafikiria mimi ni mtoto mdogo wa kuchezewa,” mrembo alimwambia jamaa na kunyamaza.

Inasemekana demu aliandaa mlo na polo akaanza kula.

“Switi mbona umekimya hivyo?” polo allimuuliza kidosho.

Inadaiwa kwamba kipusa alikuwa akisubiri saa ya ‘curfew’ ifike ndiposa atekeleze adhabu yake.

Duru zinasema zilipogonga saa tano usiku demu alilipuka.

“Unataka kulala kwa nani?” kidosho alimuuliza polo huku akipaza sauti.

Polo alibaki mdomo wazi.

“Umeshakula. Kamata njia nenda kwako mara moja,” demu alimfokea.

Jamaa alimshawishi mrembo atulie ili wasuluhishe mambo kwa utulivu. “Switi ‘curfew’ imeanza. Tutatue mambo kwa utulivu,” alirai.

Kidosho hakutaka kusikia lolote kutoka kwake. “Switi wako ni nani? Toka kwa nyumba yangu haraka,” aliwaka.

Jamaa hakuwa na jingine ila kusalimu amri. “Lala hapo kwa mlango. Kukipambazuka rudi kwako,” demu alifoka.

Inadaiwa polo alilazimika kuvumilia baridi hadi asubuhi.