Habari MsetoSiasa

Kimani Ngunjri ajificha baada ya kuzindua 'Vuguvugu la Washenzi'

January 8th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Bahati Kimani Ngunjiri anasemekana kuwa mafichoni baada ya kubaini kuwa polisi wanamwinda, baada yake kuzindua vuguvugu la ‘Washenzi’ mjini Nakuru Jumanne.

Mbunge huyo Jumanne adhuhuri aliongoza maandamano mjini humo, akimkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa matamshi yake kuwa viongozi wanaomsukuma kuidhinisha miradi ya maendeleo eneo la Mlima Kenya ni ‘Washenzi’.

Kulingana na madai ambayo yamekuwa yakisambaa, mbunge huyo alitoroka kupitia mlango wa nyuma wa hoteli ya Kokeb iliyoko kati ya mji wa Nakuru amapo alikuwa akihutubia kikundi cha vijana walipoandamana, baada ya kupata fununu kuwa polisi walikuwa wakija kumkamata.

Kamanda wa polisi kaunti ya Nakuru Hassan Barua na OCPD wa Nakuru Samuel Obara wanasemekana kuongoza kikosi cha polisi wanaomsaka mbunge huyo.

Magari manne ya polisi yanasemekana kutolewa kuhakikisha kuwa amekamatwa.

Mnamo Januari 6, Bw Ngunjiri alimtaka Rais Kenyatta kujiuzulu na kuitisha uchaguzi mpya wa Urais ikiwa ameshindwa kuendesha taifa.

Akizungumza na wanahabari mjini Nakuru, mbunge huyo alisema Rais ‘ametupilia’ watu wake, akisema jamii ya Agikuyu imekuwa ikiteseka ndani ya mamlaka ya Jubilee.

Matamshi yake yalikuja baada ya mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria aidha kutoa madai kuwa eneo la Mlima Kenya ambapo ndipo ngome ya Rais hakuna maendeleo yoyote, ilhali Rais anazindua maendeleo katika kona nyingine za Kenya.

Lakini akiwajibu viongozi hao alipokuwa eneo la Pwani Jumatatu, Rais aliwataja kuwa ‘Washenzi’, matamshi ambayo yameibua hisia kali.