Michezo

Kimanzi ambwaga Kerr kutwaa Tuzo ya Kocha Bora wa Februari

April 11th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Mathare United Francis Kimanzi amembwaga mwenzake wa Gor Dylan Kerr kwa Tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi Februari 2018.

Hii ni kutokana na mwanzo wa kuridhisha katika msimu huu kwa kocha huyo aliyepokea mafunzo yake nchini Uholanzi. Kimanzi alimenyana na Kerr katika debe la kura, na mwishowe kufanikiwa kumshinda, ila kwa kura chache.

Kimanzi aliisaidia Mathare kupata ushindi katika mechi tatu na kutoka sare mechi moja mwezi Februari, rekodi inayosawiana na ya Kerr, ambaye alipoteza tuzo hiyo kwa kura mbili pekee.

Kerr, kwa upande wake, aliisaidia Gor Mahia kuwapiga Nakumatt, Zoo FC na Kariobangi Sharks kisha akatoka sare katika mechi yake ya mwisho mwezi huo dhidi ya Tusker katika mechi iliyokosa bao hata moja.

Kimanzi alishinda tuzo hiyo mwaka 2017 baada ya kuiongoza Mathare kwa mwanzo mpya ligini kabla ya kuishiwa na pumzi na kudidimia mwishoni mwa ligi.