Michezo

Kimanzi aridhika na droo ya Kombe la Dunia

January 23rd, 2020 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

KOCHA wa Harambee Stars, Francis Kimanzi ametaja droo ya timu yake katika michuano ya kupigania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia la 2020 kuwa nafuu kwa kikosi chake.

Harambee Stars imepangiwa katika Kundi E pamoja na Rwanda, majirani Uganda na Mali, ambalo Kimanzi anatarajia vijana wake kuandikisha matokeo mazuri na kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

“Kwa kweli tumepangiwa katika kundi nafuu. Timu zote hapa zina nafasi sawa ya kufuzu. Mkikumbuka Uganda na Mali zote zilishiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, pamoja na sisi. Kadhalika Rwanda ni timu nzuri na kila mtu hapa atatakiwa kupigana vikali,” Kimanzi aliambia waandishi.

Kadhalika mkufunzi huyo alifurahia ratiba ya mechi hizo, pamoja na safari fupi kwenda Uganda na Rwanda.

“Safari za mbali wakati mwingi zinaweza kuathiri timu, lakini sisi hatutaenda mbali sana kama ambavyo imekuwa nyakati za awali, na hizi ni habari njema kwetu. Ratiba hii itatupa muda wa kutosha kujiandaa vyema, kwa sababu mechi nyingi zitachezwa dhidi ya majirani wetu eneo la Afrika Mashariki,” Kimanzi aliongeza.

Jumla ya mataifa 54 ya Afrika yatashiriki katika mechi hizi za mchujo kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa nchini Qatar mnamo 2022, lakini ni timu tano pekee zitakazowakilisha Afrika katika mashindano hayo.

Timu 10 za kwanza zitasonga mbele hadi raundi ya tatu na baadaye raundi ya mwisho ambayo itachezwa nyumbani na ugenini.