Kimataifa

Kimbunga Kenneth chafyeka watano Msumbiji

April 29th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MAFURIKO makubwa jana yaliendelea kushuhudiwa katika baadhi ya sehemu za Msumbiji, huku mamlaka ya serikali yakisema kuwa idadi ya waliofariki imeongezeka na kufikia watu watano kutokana na Kimbunga Kenneth.

Kimbunga hicho kilianza kuyakumba baadhi ya maeneo siku tatu zilizopita, ambapo serikali imekuwa ikitoa tahadhari kwa raia kuhamia maeneo salama.

Kimbunga hicho kinaikumba nchi hiyo wiki sita baada ya athari za Kimbunga Ildai.

Idara za utabiri wa hali ya hewa zimesema kuwa madhara ya kimbunga hicho, huenda yakazidi yale ya Kimbunga Ildai kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha. Kimbunga hicho kinakisiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 600.

Mvua kubwa jana iliendelea kunyesha katika mji wa Pemba, hali iliyoufanya kupoteza umeme. Ilibidi serikali kutuma vikosi vya uokoaji katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo.

Kulingana na mamlaka, karibu watu 700,000 wamo katika hatari ya kuathiriwa na mafuriko hayo, hasa katika maeneo ya mashambani. Baadhi ya mito pia imeripotiwa kuvunja kingo zake.

Wakazi wengi walisema kuwa hawajawahi kushuhudia mafuriko makubwa kama hayo.

“Sijawahi kuona mafuriko makubwa kiasi hiki,” akasema Michael Fernado, ambaye ni mkazi.

Picha za angani zilizotolewa mnamo Jumamosi zilonyesha miji kadhaa ya mkoa wa Cabo Delgado, katika eneo la Pwani ikiwa imefurika.

“Makazi yote yamefurika katika miji hiyo,” akasema Saviano Abreu, ambaye ni msemaji wa Shirika la Kutoa Misaada ya Dharura la Umoja wa Mataifa (UN).

Familia nyingi zimelazimika kutembea ndani ya maji kuondoka katika maeneo yaliyoathiriwa, kwani nyumba nvingi zimejengwa kwa udongo.

Hii ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kukumbwa na vimbunga viwili vikubwa kwa wakati mmoja. Watalamu wa masuala hali ya anga, wamehusisha vimbunga hivyo na mabadiliko ya hali ya anga.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa itachukua muda mrefu kurejesha hali ya kawaida mjini humo kutokana na uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho.

Jamii zilizoathiriwa sana ni Macomia, Quissanga na Mocimboa da Praia.

Karibu makazi 3,500 katika baadhi ya sehemu za Cabo Delgadi yaliharibiwa kabisa, ambapo baadhi ya barabara ziliharibiwa na daraja moja kusombwa na maji. Baadhi ya shule na vituo vya afya pia vimeharibiwa.