Habari za Kaunti

Kimemramba Nassir! KRA yaendea kituo chake cha redio

May 30th, 2024 2 min read

NA WAANDISHI WETU

GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, ameshutumu uongozi wa Kenya Kwanza akidai wanatishia kufunga biashara yake ya utangazaji habari kutokana na msimamo wake wa kupiga marufuku muguka.

Alitoa hisia hizo baada ya maafisa waliokuwa na vitambulisho vya Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) kuvamia afisi za Radio Rahma, ambayo anaimiliki jijini Mombasa, Jumatano asubuhi.

Alikosoa serikali kwa kile alichodai kuwa ni vitisho kwa viongozi ambao wamepiga marufuku uuzaji wa ‘dawa hiyo ya kulevya’ katika kaunti zao.

“Walikuja Radio Rahma, walitaka kuchukua vifaa. Nimezungumza na wakuu wa KRA na hakuna aliyethibitisha kuwatuma watu hawa hapa,” akaongeza Bw Nassir.

Duru kutoka KRA zilithibitisha kuwa maafisa hao walikuwa ni wafanyakazi wa shirika hilo la serikali.

Kulingana na afisa mkuu wa KRA ambaye alizungumza na Taifa Leo kwa sharti la kutotajwa jina akihofia kuadhibiwa, maafisa hao walikuwa wametumwa kutoka Nairobi na walikuwa wamekuja kufuatilia malimbikizi ya ushuru yanayosubiri kulipwa na kituo hicho cha redio.

“Ni tatizo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu na kile ninachojua, ni maafisa kutoka Nairobi walioenda hapo kujaribu kujua hatua zilizopigwa kuhusu ushuru ambao haujakamilishwa na kituo hicho,” alisema afisa huyo.

Bw Nassir, ambaye ni mwanachama wa ODM, hata hivyo alisisitiza kuwa utawala wake utapambana na matumizi ya muguka hadi mwisho. Aliandamana na Naibu Gavana Francis Thoya, Naibu Gavana wa Taita Taveta Christine Kilalo, Wabunge Mishi Mboko (Likoni) na Rashid Bedzimba (Kisauni), Maspika wa Mabunge ya Kaunti Teddy Mwambire (Kilifi) na Aharub Khatri (Mombasa).

“Hatutaogopa. Ikiwa italazimu kufunga biashara zetu, fanya hivyo. Ikiwa unafikiri redio hii imekuwa ikitangaza zaidi kuhusu madhara ya muguka, ifunge tu. Nina hakika kuliko wakati mwingine wowote kuna washawishi wanaotaka maisha ya watoto wetu kuharibiwa na bidhaa hii,” akaongeza.

Mahakama Kuu ya Embu ilitoa maagizo ya muda mnamo Jumanne, ambayo yaliondoa marufuku iliyowekwa na Kaunti za Mombasa, Kilifi na Taita Taveta dhidi ya muguka, ikisubiri kusikizwa kwa kesi ya kupinga marufuku hiyo.

Huku hayo yakijiri, mvutano ulizuka eneo la Bonje jijini Mombasa wakati maafisa wa usalama wa kaunti walipojaribu kuwazuia wafanyabiashara wa muguka kuingia jijini.

Malumbano yalizuka baina ya pande hizo mbili, huku maafisa wa kaunti wakisisitiza kuwa wanasubiri kupewa maagizo ya mahakama.

Wafanyabiashara hao kwa upande mwingine walitaka kupeleka bidhaa zao sokoni wakidai zitaharibika wakichelewa.

Baadhi walirushiana ngumi na hatimaye maafisa wa kaunti wakalazimika kuondoa magari yao ambayo walikuwa wametumia kuziba barabara na kutatiza usafiri.

Mmoja wa maafisa wa kaunti alionekana baadaye akiwa na nguo zilizochanika kutokana na fujo hizo zilizochukua dakika chache.

Muda mfupi baadaye, madereva wa malori waliingia jijini na kupeleka bidhaa zao sokoni Kongowea ambapo tayari wanunuzi wa jumla walikuwa wakisubiri.

Ripoti za Winnie Atieno, Anthony Kitimo na Kevin Mutai