Michezo

Kimetto na Chepchirchir kupigania ubingwa wa Shanghai Marathon

November 16th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa zamani wa Tokyo Marathon, Dennis Kimetto (mwaka 2013) na Sarah Chepchirchir (2017) wametoa ithibati ya kupigania ubingwa wa mbio za Shanghai Marathon nchini Uchina hapo Novemba 18, 2018.

Macho yatakuwa kwa Kimetto ambaye hajamaliza mbio za kilomita 42 tangu akamilishe London Marathon nchini Uingereza katika nafasi ya tisa mwezi Aprili mwaka 2016.

Alishikilia rekodi ya dunia ya marathon ya wanaume kwa kushinda Berlin Marathon mwaka 2015 kwa saa 2:02:57 hadi pale Mkenya mwenzake Eliud Kipchoge alipoivunja katika jiji hilo la Ujerumani mwezi Septemba mwaka 2018 na kuweka rekodi mpya ya saa 2:01:39. Hata hivyo, Kimetto amekuwa akisumbuliwa na jeraha na kujiondoa mara kadhaa mashindanoni ikiwa ni pamoja na katika Vienna Marathon nchini Austria mwezi Aprili mwaka huu wa 2018.

Licha ya kuwa Kimetto amekuwa akitatizika kukamilisha marathon, waandalizi wa Shanghai Marathon wanaamini ana uwezo sio tu wa kutwaa taji mwaka huu, bali pia kuvunja rekodi ya Shanghai Marathon ya saa 2:07:14 ambayo Mkenya Paul Lonyangata aliweka mwaka 2015. “Hata Kimetto anaweza kufuta rekodi ya kasi bora kuwahi kushuhudiwa katika ardhi ya Uchina ya saa 2:06:19 ambayo Mkenya Moses Mosop aliweka akishinda Xiamen Marathon 2015,” waandalizi hao wamesema na kuongeza kwamba lengo lake kubwa ni kukamilisha mbio hizi.

Wapinzani wake wakuu ni Mkenya Asbel Kipsang’ na Waethiopia Yitayal Atnafu, Seyefu Tura na Tsegaye Mekonnen.

Chepchirchir anatarajiwa kupata ushindani mkali kutoka kwa Mkenya Flomena Cheyech na Waethiopia Yebrgual Melese na Helen Tola Bekele. Rekodi ya Shanghai Marathon ya wanawake ya saa 2:21:52 inashikiliwa na Muethiopia Tigist Tufa.