Habari

Kimunya huru baada ya kesi ya unyakuzi kipande cha ardhi kufutiliwa mbali

May 21st, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha Bw Amos Kimunya aliachiliwa Jumatano katika kesi ya unyakuzi wa ardhi ya umma ambapo anadaiwa kuikabidhi umiliki kampuni ya kibinafsi alipokuwa mkurugenzi.

Bw Kimunya aliye pia Mbunge wa Kipipiri pamoja na Mkurugenzi wa Mashamba katika Wizara ya Ardhi Lilian Wangiri Njenga na mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya Midland Limited Junghae Wainaina, walishtakiwa kwa unyakuzi wa kipande cha ardhi ya umma.

Bw Kimunya alikabiliwa na mashtaka matatu ya kutumia mamlaka ya ofisi yake vibaya alipokuwa Waziri wa Ardhi na wakati huo huo akiwa Waziri wa Fedha mwaka 2005.

Walidaiwa kutekeleza ufisadi huo kati ya 2003 na 2006.

Inadaiwa aliipa kampuni ya Midland Ltd kiasi ekari 25 za kipande cha ardhi mali ya Wizara ya Kilimo.

Shamba hilo lilikuwa sehemu ya ekari 75 za Wizara ya Kilimo zilizokuwa zimetengwa kustawisha zao la viazi.

Shamba hilo liko katika Kaunti ya Nyandarua

Akiwaachilia watatu hao, hakimu mwandamizi Bw Felix Kombo alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kuamua “wana na kesi ya kujibu.”

Hakimu mwandamizi Felix Kombo. Picha/ Richard Munguti

Mahakama ilikashfu upande wa mashtaka kwa kuwasilisha ushahidi ambao haukulingana na mashtaka waliyofunguliwa washtakiwa hao watatu.

Bw Kimunya alishtakiwa kutofichua kwamba alikuwa mkurugenzi wa Midland na mwenye hisa mkuu kabla ya kipande hicho cha ardhi kupewa kampuni hiyo.

Mahakama iliwaondolea lawama ikisema washtakiwa hao “hawangefunguliwa mashtaka kwa mara ya kwanza.”

Baada ya kufikia uamuzi hawakuwa na makosa, hakimu alimtakia Lilian heri akielekea kustaafu mwaka huu wa 2020.

Pia hakimu aliamuru washtakiwa warudishiwe dhamana ya Sh1 milioni pesa taslimu walizokuwa wamelipa kortini.

Akizugumza na Taifa Leo, Bw Kimunya alisema ipo haja ya kusitisha kabisa kuwakamata wananchi wasio na hatia na kuwashtaki.

Alisema amekuwa akihudhuria mahakama kwa muda wa miaka mitano sasa ijapokuwa alijua hakuwa na makosa.

“Nilijua kinagaubaga sikuwa na makosa. Nimepotezewa muda mwingi na ilhali sikuwa na hatia,” alisikitika Bw Kimunya.

Alisema atawasiliana na mawakili wake kuamua ikiwa ataishtaki serikali alipwe fidia kwa kufunguliwa mashtaka ya uongo.

Hata hivyo alielezea furaha yake kwa “kuondolewa lawama na haki kutendeka.”